JESHI la Polisi Tanzania limeshtukia mipango ovu ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ya kufanya vikao vya kujaribu kuhamasisha vurugu, likisema wote wanaotaka kufanya uharamia huo watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.
Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania David Misime, amesema hayo leo ikiwa ni mwendelezo wa kutoa elimu kwa Watanzania wakiwemo wanasiasa juu ya kulinda amani na utulivu wa nchi kama njia ya kujiletea maendeleo, badala ya kupanga njama za kuleta vurugu ili kuichafua nchi.
“Jeshi la Polisi liunatoa onyo kali kwa yeyote atakayeendelea kuratibu, kuhamasisha na kushiriki katika uhalifu huo wa kupangwa ambao lengo lake ni kutaka kuvuruga amani ya nchi yetu baada ya kushindwa kwa mikakati yao. Watu hao watashughulikiwa ipasavyo kwa mujibu wa sheria za nchi.
“Jeshi la Polisi linapenda kusisitiza atakayefika kituo chochote cha Polisi kwa nia ovu tumejiandaa na atashughulikiwa ipasavyo kwa mujibu wa sheria,” Alisema Misime.
Kwa mujibu wa Polisi, Chadema hawajaridhishwa na uamuzi wa Mahakama Kuu, juu ya uamuzi wa shauri la lililowasilishwa mbele yake ambapo miongoni mwa maamuzi hayo ni pamoja na kutoa amri kwa Jeshi la Polisi kufanya upelelezi kujua mahali walipo viongozi wa Baraza la Chadema (BAVICHA), Wilaya ya Temeke, Deusdedit Soka na wenzake wawili, hali iliyowafanya viongozi wa chama hicho kufanya vikao kwa njia ya kieletroniki (Zoom) na kukubaliana kwa vile hawajaridhika na maamuzi ya mahakama.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED