IGP Wambura atabiri polisi kuwa jeshi bora duniani

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 06:20 PM May 24 2024
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Camillus Wambura.
Picha: Vitus Audax
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Camillus Wambura.

MKUU wa Jeshi la Polisi Nchini Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Camillus Wambura amesema Jeshi hilo limelenga kuendelea kuwa bora kiutendaji na kufika nafasi ya kwanza kati ya majeshi bora duniani.

IGP Wambura ametoa kauli hiyo mapema leo wakati wa utoaji wa Nishani kwa Maofisa,Wakaguzi pamoja na Askari wa vyeo mbalimbali 32 kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa na kueleza kuwa maboresho makubwa yanaendelea ili kufikia hatua hiyo.

Amesema miongoni mwa maboresho hayo ni pamoja na kufanyia kazi maelekezo ya Tume ya Haki Jinai pamoja na serikali na kuacha kufanya kazi kwa mazoea,kubadilika kiutendaji na kifikra ili kuhakikisha Jeshi hilo linafuata weledi ni misingi yake.

Vilevile amesema, serikali imeendelea kutambua mchango wa Jeshi hilo kwa kuendelea kuboresha maslahi ya watumishi, kuongeza ajira pamoja na ujenzi na maboresho ya miundombinu ya Jeshi hilo.

"Kwa hatua hii ya kutunukiwa nishani, Rais Samia Suluhu Hassan ameweka alama isiyofutika katika mioyo ya Askari wetu kwa ishara ya kutambua michango na kazi nzuri zinazofanywa na Jeshi la Polisi nchini tunashukuru saana,"amesema Wambura

"Tulikuwa na ombwe kubwa la upandishwaji vyeo kwa muda mrefu sana lakini kwa kipindi hiki Askari wamepandishwa vyeo katika ngazi mbalimbali sambamba na utolewaji wa ajira ambazo zimekuwa zikitolewa kila mara lengo likiwa ni kuongeza nguvu kazi katika jeshi letu hivyo tukahakikishe tunatoa huduma bora kwa mtejea bila kujali ni mteja wa ndani au wa nje antendewe haki kwa stahaa na stahiki yake ili tuhakikishe tunafika katika ngazi za juu katika majeshi bora duniani," amesema Wambura.

Amesema ipo siku hata kama siyo leo, Jeshi hilo litakuwa jeshi bora duniani kwani maono ya Rais na serikali katika  kulisuka yanalenga kulifanya kuwa bora Duniani.

Akizungumza kwa niaba ya Askari waliopokea nishani, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Wilibroad Mutafungwa amesema nishani hizo zitawaongezea morali, nidhamu na uwajibikaji katika utendaji kazi na kuahidi kuendelea kusimamia na kutekeleza majukumu katika weledi na misingi ya Jeshi hilo.

"Tunaomba hatua hii iwe endelevu kwa kuendelea kutoa nishani hizi kwa kutambua majukumu na uwezo wa Askari katika utumishi hali inayoongeza chachu katika utumishi,"amesema DCP Mutafungwa.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda amesema amani na usalama nchini imeendelea kuimarika kutokana na kazi inayofanywa na Jeshi hilo kupitia IGP Wambura pamoja na viongozi wake ngazi za mikoa.

"Mkoa wa Mwanza una utulivu ambao ni matokeo ya kazi nzuri ya jeshi la Polisi kwani kwa Mkoa huu ukiwa salama mikoa yote ya Kanda ya Ziwa IPO salama kutokana kuwa mipango yote inaanzia hapa na kupelekwa kwenye mikoa mingine hivyo hali ya usimamizi iendelee hivyohivyo,"amesema Mtanda.