Fahamu yaliyozungumzwa na familia kuhusu Gardner

By Restuta James , Nipashe
Published at 09:55 AM Apr 23 2024
Waombolezaji wakishusha jeneza lenye mwili wa mtangazaji wa Clouds Media Group,  marehemu Garner G Habash, kwa ajili ya kuagwa katika viwanja vya Klabu ya Leaders, jijini Dar as Salaam.
PICHA: MIRAJI MSALA
Waombolezaji wakishusha jeneza lenye mwili wa mtangazaji wa Clouds Media Group, marehemu Garner G Habash, kwa ajili ya kuagwa katika viwanja vya Klabu ya Leaders, jijini Dar as Salaam.

MWILI wa aliyekuwa mtangazaji wa Clouds FM, Gardner Habashi (51), unatarajiwa kuzikwa leo katika kijiji cha Kikelelwa, Tarakea, Rombo mkoani Kilimanjaro, baada ya kuagwa jana Dar es Salaam, huku familia Ikimwelezea kuwa alikuwa mtu mwenye huruma ambaye aliwasisitiza kufanya kazi kwa bidii.

Akitoa salamu za familia katika viwanja vya Leaders, Dk. Celine Mandara, amesema Gardner alikuwa msaada kwa ndugu na jamaa zake na mwenyeji wa wale waliokuwa wanakuja mjini kutafuta kazi au maisha.

“Kipekee kama familia tunamshukuru sana Mungu kwa kuwa na Gardner na jamii kwa ujumla imefaidika na maisha yake. Pamoja na utumishi kwa jamii, katika ngazi ya familia alikuwa na wingi wa huruma hususani kwa wanawake. Alipenda wasionewe ila wajaliwe (wathaminiwe) sana. Alisisitiza sana kufanya kazi kwa bidii bila visingizio ili ndoto zitimie,” amesema Dk. Mandara. 

“Pia alikuwa mwenyeji kwa ndugu waliokuja kutafuta maisha hapa mjini na aliweza kuwaunganisha watu wengi. Alishughulika na shida na mahitaji yao kama yake. Sisi kama wadogo zake, tulifaidi sana msaada wa kifedha aliokuwa anatupatia. Dunia inaweza kumtambua vinginevyo lakini sisi kama ndugu zake tunamtambua kama msaada, destiny helper (msaada wa hatima) kwetu na anayejituma sana,” ameongeza. 

Katika salamu zake, Rais Samia Suluhu Hassan ameandika: “Ninatoa pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki na wafanyakazi wa Clouds Media Group kwa kuondokewa na ndugu yetu, Gardner Gabriel Habash. Mchango wa Gardner kwenye ustawi wa sekta ya habari nchini ni mkubwa, na amekuwa mnasihi wa vijana wengi. Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema. Amina.”

Kabla ya kuagwa na umma katika viwanja vya Leaders, mwili wake ulipelekwa katika Kanisa la Kiinjili la Kulutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Mbezi Beach, ambako ilifanyika ibada maalumu iliyohudhuriwa na umati mkubwa wa watu.

Baadhi ya viongozi walioshiriki msiba huo jana ni Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Maryprisca Mahundi, ambaye ametoa salamu za wizara akimtaka mtoto wa marehemu, Karen, kutojihisi mpweke kwa kuwa baba yake amemwacha mashangazi kutokana na baba alivyoishi na watu.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amepongeza mshikamano ulioonyeshwa na watu wa makundi mbalimbali na kushauri kwamba ni vyema kushirikiana zaidi pindi mtu anapougua ili aone upendo wa wanaomzunguka.

Msiba wa Gardner umehudhuriwa na wakurugenzi, wakuu wa mikoa na wilaya, viongozi mbalimbali wa dini, wakiwamo masheikh, maaskofu na wachungaji. Miongoni mwao ni Mtume Boniface Mwamposa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda.

Mwili wake ulisafirishwa jana kwa ndege Kwenda Kilimanjaro kwa ajili ya maziko ambayo yatafanyika leo.