SHULE ya Sekondari Etaro, iliyopo Musoma Vijijini mkoani Mara, inatarajiwa kuanzisha somo la Sayansi ya Kompyuta ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuanzisha kidato sita mchapuo wa sayansi jimboni humo.
Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo amesema, jimbo hilo lina sekondari 28, huku za serikali zikiwa ni 26 lakini za kidato cha tano na sita zikiwa chache.
"Etaro Sekondari ina maabara ya kemia na baiolojia ambazo zote zinatumika, huku maabara ya fizikia ikiendelea kukamilishwa
ujenzi wake ambao unachangiwa na wanavijiji, mbunge wa jimbo na Mfuko wa Jimbo," amesema Prof. Muhongo.
Ameongeza kuwa sekondari hiyo ina kompyuta 25 zilizonunuliwa na wafadhili aliowataja kwa jina la Northern Illinois University ya USA, huku fedha za ufungaji wa mtandao zikitolewa na wafadhili hao.
"Mimi kama mbunge wa jimbo ninaendelea kuhamasisha na kuchangia ujenzi wa maabara tatu kwa kila sekondari ya kata kwa malengo yakiwa ni kuboresha uelewa na ufaulu katika masomo ya sayansi," amesema.
Amesema, anataka kuhakikisha jimbo linaongeza idadi ya sekondari zenye vidato vya vya tano na sita vya masomo ya sayansi, na kwamba Etaro Sekondari nayo inatayarishwa kuwa na vidato hivyo.
"Kwa sasa tuna sekondari ya kidato cha tano na sita moja ambayo ni Kasoma lakini haina mkondo wa masomo ya sayansi. ipo katika Kijiji cha Kaboni, hivyo tunaendelea na mkakati wa kuongeza nyingine za mchepuo wa sayansi," amesema.
Amefafanua kuwa lengo lao ni kushirikiana na serikali kuongeza idadi ya sekondari za kidato cha tano na sita huku mkazi ukiwa kwenye uanzishwaji wa vidato hivyo.
"Mwaka huu tumepata usajili wa "high schools" mbili ambazo ni Suguti High School michepuo mitatu ya PCM, PCB na CBG) ya masomo ya sayansi," amessema.
Ametaja sekondari nyingine kuwa ni Mugango ambayo itakuwa na mchepuo wa CBG wa masomo ya sayansi na kwamba mradi wa ujenzi wa maabara tatu za masomo ya sayansi (fizikia, kemia na bailojia unaendelea katika sekondari mbalimbali.
"Tunaishukuru serikali kuendelea kutupatia fedha, kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya elimu ya sayansi kwenye shule zetu, lakini pia na Northern Illinois University ya USA kwa ushirikiano wake wa kuboresha miundombinu ya elimu ya Etaro Sekondari," amesema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED