Dk. Rose kutoa mabati 100 ujenzi wa ofisi za CCM Kilombero

By Frank Monyo , Nipashe
Published at 08:49 AM Apr 25 2024
Mwenyekiti wa Wazazi CCM Mkoa wa Morogoro, Dk. Rose Rwakatare, katikati akipata maelezo ya ujenzi wa ofisi za CCM Wilaya ya Kilombero kutoka kwa Katibu wa chama hicho Wilaya, Joseph Mwambeleko,kushoto Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kilombero, Mohamed Msuya.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mwenyekiti wa Wazazi CCM Mkoa wa Morogoro, Dk. Rose Rwakatare, katikati akipata maelezo ya ujenzi wa ofisi za CCM Wilaya ya Kilombero kutoka kwa Katibu wa chama hicho Wilaya, Joseph Mwambeleko,kushoto Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kilombero, Mohamed Msuya.

MWENYEKITI wa Wazazi CCM Mkoa wa Morogoro, Dk. Rose Rwakatare, ameahidi kutoa mabati 100 kwaajili ya ujenzi wa ofisi ya chama hicho Wilaya ya Kilombero inayoendelea kujengwa ambayo itagharimu milioni 250.

Alitoa ahadi hiyo jana mara baada ya kutembelea ofisi hiyo kuangalia maendeleo ya ujenzi wake alipokuwa kwenye ziara yake ya kukagua athari za mafuriko katika Wilaya hiyo.

Kwenye ziara yake hiyo, Dk. Rose alitoa msaada wa tani tano za mchele kwa waathirika wa mafuko wa Jimbo la Mlimba mkoani humo.

Akizungumza kwenye eneo la ujenzi wa jengo hilo, Dk. Rose aliwapongeza viongozi wa chama hicho mkoa wa Morogoro kutokana na kasi ya ujenzi huo unaoenda kwa kasi kubwa.

“Mara ya mwisho kufika hapa ujenzi ulikuwa haujaanza na mimi kama mwenyekiti wa wazazi wa Mkoa nitatoa mabati 100 kwaajili ya kupaua nawaomba wanachama wengine wajitokeze kuchangia jengo hili kwasababu hiki ni chama chetu wote,” alisema Dk. Rose

Alisema jengo hilo litakuwa na manufaa makubwa kwa chama hicho na kwamba iwapo wanachama wengine watajitokeza kwa wingi kutoa michango yao linaweza kukamilika mwishoni mwa mwaka huu.

Naye Katibu wa CCM Wilaya ya Kilombero, Joseph Mwambeleko, alimshukuru Dk. Rose kwa kutembelea maendeleo ya ujenzi wa ofisi ya chama na msaada wa mabati 100 ambao wameahidi kuutoa.

Aliwaomba wanachama wa chama hicho na wadau wa maendeleo nchini kuchangia ujenzi huo na kwamba misaada hiyo haiku kwaajili ya mgtu binafsi bali kwaajili ya chama chao.

“Chama chetu kitajengwa na nguvu ya wanachama kwa hiyo nawaomba wenye nia ya kutaka kusaidia wasiogope kitu chochote kwasababu hawamchangii mtu wanakichangia chama chao,” alisema

Alisema jengo hilo linajengwa kwa nguvu za wanachama na marafiki wa chama hicho ambao chama kimewaandikia barua ya shukrani kutambua mchango wao.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kilombero, Mohamed Msuya, aliwaomba wadau wa maendeleo Wilaya ya Kilombero kuendelea kuchangia ujenzi wa ofisi za chama hicho.

“Wakati wa uchaguzi mwaka juzi niliahidi kwamba kipaumbele change ni kujenga ofisi za chama na leo nafurahi sana kuona jengo limesimama nab ado asilimia ndogo tu likamilike kwa hiyo wanachama waje watusaidia kumalizia ujenzi,” alisema

“Huu si wakati wa uchaguzi, uchaguzi ni 2025 kwa hiyo watu wasiogope kuja kuchangia ujenzi wa jengo la chama chao, nawahakikishia kuwa wote watakaokuja tutawalinda,” alisema Msuya