MKUU wa Wilaya ya Longido, Salum Kali, ameanza kazi kwa kasi huku akisema watendaji wa serikali ni wauuzaji wa duka la Chama Cha Mapinduzi ambalo lina wajibu wa kuwatumikia Watanzania na kuwaletea maendeleo.
Akizungumza kwenye mkutano wa Katibu wa NEC, Itikadi,Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi, Amos Makalla, alisema ofisi ya Mkuu wa Wilaya ndio ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania,na kwmaba itakuwa wazi saa 24.
"Nawaomba mnipokee sana,mimi ni zao lenu la CCM,CCM ndio wenye serikali,sisi ni wauzaji wa duka ambalo ni mali ya Chama Cha Mapinduzi,"alisema.
Alisema atafanyakazi kwa ushirikiano na wananchi wa wilaya hiyo katika kufikia malengo na utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi.
"Ninawaomba mtembee kifua,ofisi yangu ndio ofisi ya Rais,Amiri Jeshi Mkuu, Mwenyekiti wa CCM Taifa...mtembee kifua mbele mimi nipo,huko mliko nitakuja,huko ndipo waliko watu,nitatoa namba yangu ya simu kila mwananchi awe nayo,"alisema Kali.
DC Kali aliteuliwa Septemba mosi,mwaka huu, akichukua nafasi ya Marco Ng'umbi, ambaye siku moja kabla ya kuondolewa ilisambaa picha jongefu ya dakika 1.32 akiwaeleza watu aliowataja kuwa ni madiwani wa wilaya hiyo kuwa ushindi wao sio kwa ujanja wao bali ulitokana na nguvu ya serikali mwaka 2020.
Alisema waliopita bila kupingwa ni kazi kubwa iliyofanywa na serikali na si kutokana na ubora wa kila mmoja wao.
Kauli hiyo ilizua mjadala mkali kwenye mitandao ya kijamii.
Jana,Makalla akiongea na viongozi wa CCM mkoani Arusha,alisema chama hicho kinashinda uchaguzi kwa haki na sio kubebwa bebwa,na kwamba maneno ya DC huyo ni yake na chama hakiyatambui.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED