CP Kaganda awataka Trafki kusimamia majukumu yao ipasavyo

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:40 PM Jun 21 2024
Kamishna wa Usimamizi Rasilimali Watu na Utawala, Jeshi la Polisi, CP, Suzan Kaganda akipeana mikono na Mkurugenzi wa Uendeshaji, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Anselim Peter mara baada ya kufungua kikao kazi baina ya WCF na Makamanda wa Polisi.
Picha:Mpigapicha Wetu
Kamishna wa Usimamizi Rasilimali Watu na Utawala, Jeshi la Polisi, CP, Suzan Kaganda akipeana mikono na Mkurugenzi wa Uendeshaji, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Anselim Peter mara baada ya kufungua kikao kazi baina ya WCF na Makamanda wa Polisi.

KAMISHNA wa Utawala na Rasilimali Watu Jeshi la Polisi, CP, Suzan Kaganda amewataka Makamanda wa Polisi wa Usalama Barabarani nchini (DTOs) kusimamia majukumu yao ipasavyo wakati wa kujaza fomu ya taarifa ya ajali za barabarani.

CP. Kaganda ametoa maelekezo hayo jijini Arusha Leo Juni 21, 2024, wakati akifungua kikao kazi cha Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) na Makamanda hao kutoka mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Tanga kuhusu shughuli za mfuko huo na umuhimu Jeshi la Polisi katika uchakataji madai ya fidia kwa mfanyakazi aliyepata ajali hususan ya barabarani.

“Ninyi DTOs mnapaswa kuwa na weledi katika kufikia malengo tarajiwa, niwatake mkawasimamie vema wale walio chini yenu, kulikuwa na changamoto hususan zile fomu zinazotoka Jeshi la Polisi ili kuwawezesha WCF kutoa huduma.” amesema.

Amefafanua kuhusu hitaji la fomu ya taarifa ya tukio la ajali, Mwanasheria wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, SSP Deus Sokoni alisema, Fomu namba 90 inatamkwa kwenye Kanuni za WCF, na Jeshi la Polisi linawajibu wa kusimamia kwa ukamilifu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uendeshaji Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Anselim Peter, amesema shughuli kubwa ya WCF ni kulipa fidia kwa mfanyakazi anayeumia, kuugua ama kufariki kutokana na kazi, na kwa sababu hiyo Mfuko unahitaji ushirikiano na taasisi nyingine za Serikali ikiwemo Jeshi la Polisi ili uweze kutekeleza vema majukumu yake.

Makamanda wa Usalama Barabarani wakiwa katika kikao kazi cha Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF).

Aidha, Meneja Usimamizi Ulipaji Fidia WCF,Rehema Kabongo amesema, mafunzo hayo ni jitihada za mfuko kuwajengea uwezo wadau mbalimbali ikiwemo Jeshi la Polisi.

“Mkishaelewa majukumu ya WCF, itawasaidia kujua umuhimu wa fomu ya taarifa ya Jeshi la Plisi pale mfanyakazi anapopata ajali akiwa kazini na hivyo kusaidia uchakataji malipo ya fidia.” amefafanua.