CHADEMA, polisi zaingia mvutano mpya

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 07:14 AM Aug 31 2024
Naibu Kamishna (DCP) David Misime.

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Jeshi la Polisi vimeingia katika mvutano mpya baada ya kuwapo madai kuwa chama hicho kimepanga kufanya maandamano na kuvamia vituo vya polisi.

Wakati polisi ikidai hivyo, CHADEMA imeibuka na kulitaka jeshi hilo kuweka hadharani madai hayo kama kuna ushahidi. 

Taarifa iliyotolewa jana na Msemaji wa Jeshi hilo, Naibu Kamishna (DCP) David Misime, ilisema maandamano hayo yamepangwa kwa kile alichokiita kuwa baada ya CHADEMA kutoridhishwa na uamuzi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam.

Kutokana na madai hayo, Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itikadi, Uenezi na Mambo ya Nje CHADEMA, John Mrema, alisema wameichukulia kauli hiyo kwa uzito mkubwa.

“Agosti 10, mwaka huu, polisi walitoa kauli kama hiyo wakati vijana wakijiandaa kuadhimisha siku ya vijana mkoani Mbeya na baada ya kauli hiyo kutolewa na Kamishna Awadhi viongozi wetu walianza kukamatwa na wengine kuumizwa vibaya,” alisema.

Mrema alidai kuwa kauli hiyo hawawezi kuiacha kubaki hata kwa dakika moja kwa sababu ni ya uongo.

“Ni kauli ambayo ni hatari na kuhatarisha usalama wa viongozi na wanachama  wa CHADEMA. Kwa sababu tangu hukumu ya mahakama hakuna kikao chochote kilichofanyika kwa njia ya zoom au kawaida, hata kikao cha sekretarieti juzi hakikufanyika kwa sababu tulikuwa tumetawanyika nchini,” alisema.

Kutokana na hilo, Mrema alisema CHADEMA inalitaka Jeshi la Polisi lithibitishe kwa sababu ni jaribio la kunyanyapaa viongozi wa chama hicho  kufanywa kama wahalifu wakati hicho si chama cha kihalifu.

“Tunalitaka Jeshi la Polisi litoe ushahidi hadharani. Hatujafanya kikao chochote achilia mbali kupanga haya ambayo wanasema yamepangwa. Tunalaani kauli hii ya Jeshi la Polisi kwani ina nia ovu dhidi ya viongozi na wanachama,” alisema.

Alisema kauli hiyo wanaoona kama ni mkakati wa Jeshi la Polisi kuvuruga vikao vya ndani vya CHADEMA, ambapo wanajiandaa na uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

“Wanataka watuvuruge tusiweze kuandaa wagombea, tusiandae mawakala kwa ajili ya uandikishaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura na mawakala wa Daftari la Wakazi,”

“Tatu, tunalitaka Jeshi la Polisi watekeleze amri ya mahakama ya kuwarejesha kina soka mtaani, utekaji ni uhalifu kama mwingine.

“Mahakama imewapa amri waitekeleze, badala ya kutafuta visingizio kuwa CHADEMA wanaandaa vijana kuvamia vituo vya polisi. Kama polisi linaogopa vijana 20 basi lifumuliwe na kusukwa upya,” alisema.

Mrema alisema wanawataka wanachama wao wasiingie hofu na kama kuna tatizo la kipolisi wasisite kwenda vituo vya polisi na wanategemea watapewa huduma kama wananchi wengine.

“Kauli hii ya Jeshi la Polisi inawatisha wanachama wetu kwenda vituo hivyo hata kama wana jambo la kipolisi kwa kuhofia kukamatwa. Jambo la tano, Jeshi la Polisi liache tabia hiyo kuwaona viongozi na wanachama CHADEMA kama wahalifu. Polisi ifute kauli yake mara moja.

“Tunatoa wito kwa Amiri Jeshi Mkuu (Rais Samia Suluhu Hassan) alifumue Jeshi la Polisi na kulisuka upya, kwani intelejensia yake imedhibitika imefeli tena kama ilivyofeli awali, Mbeya.

Mrema alilitaka Jeshi la Polisi kuacha kufanya kazi kwa kile alichokiita, kutumia ramli ambayo ni chonganishi.

“Kama kuna mtu Jeshi la Polisi wanadhani anawapa taarifa za CHADEMA, anazidi kuwadanganya na kuwadhalilisha, ndio maana wanakurupuka na kutoa taarifa zisizo za ukweli,” alidai..

MADAI YA POLISI 

“Mahakama ilitoa uamuzi wake kuhusiana na shauri lililowasilishwa mbele yake ikiwamo kutoa amri kwa Jeshi la Polisi kufanya upelelezi kujua mahali walipo viongozi wa Baraza la Vijana CHADEMA (BAVICHA) Wilaya ya Temeke.

“Viongozi hao ni Deusdedit Soka na wenzake wawili. Jeshi la Polisi lilipokea amri hiyo na kuongeza nguvu katika upelelezi ambao lilishaanza toka awali baada ya kuripotiwa kwa viongozi hao,” alisema.

DCP Misime alidai kuwa baada ya uamuzi huo wa mahakama, Jeshi la Polisi limepata taarifa za uhakika za viongozi wa CHADEMA kufanya kikao kwa njia ya kieletroniki (zoom) na kukubaliana kwa vile hawajaridhika na uamuzi wa mahakama kwa sababu hayakuakisi malengo yao.

Kwa mujibu wa Misime, CHADEMA wamekubaliana waanze kuhamasisha wafuasi wao chinichini kufanya maandamano ya kuelekea maeneo mbalimbali pamoja na maofisini.

DCP Misime alidai kuwa wamekubaliana wahamasishe na kuunda vikundi vya vijana wapatao 20, ili wavamie vituo vya polisi vilivyoko jijini Dar es Salaam kwa wakati mmoja.

“Jeshi la Polisi linatoa onyo kali kwa yeyote atakayeendelea kuratibu, kuhamasisha na kushiriki katika uhalifu huo wa kupangwa ambao, lengo ni kutaka kuvuruga amani ya nchi yetu, baada ya kushindwa kwa  mikakati yao (atakayefanya hivyo) atashughulikiwa ipasavyo kwa mujibu wa sheria za nchi.

“Jeshi la Polisi lingependa kusisitiza atakayefika kituo cha polisi kwa nia ovu, tumejiandaa na atashughulikiwa ipasavyo kwa mujibu wa sheria,” alisema DCP Misime.

VIONGOZI WALIOTEKWA

Alisema baada ya hukumu ya mahakama kutoka, mawakili walitoa tamko kuwa watakata rufani, hivyo wamewaachia waendelee na hilo.

Mrema alidai, “Mahakama wakati huo huo inasema hakuna ushahidi kama wanashikiliwa na Jeshi la Polisi, lakini papo hapo inalitaka Jeshi la Polisi lichunguze, tangu lini mtuhumiwa akajichunguza mwenyewe na kuja na ukweli.”

Alisema CHADEMA kinasisitiza Rais Samia kuunda Tume ya Kimahakama ya Majaji kuchunguza tuhuma zote za watu kupotea, kuteswa na kutekwa.

 “Leo tunaambiwa watu 10 wamefukiwa kwa mganga. Kama mganga mmoja anaweza kufukia watu 10, fikiria tuna waganga wangapi, ni watanzania wangapi wamepoteza ndio maana tunasisitiza tume iundwe,” alisema.