KADA wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Ally Kibao, aliyedaiwa kufungwa pingu kisha kushushwa katika basi Ijumaa iliyopita mkoani Dar es Salaam, amepatikana akiwa amefariki dunia.
Kukiwa na utata kuhusu chanzo cha kifo cha Mjumbe huyo wa Sekretarieti ya CHADEMA Taifa na Msaidizi wa Katibu Mkuu, jana kulitokea mvutano mkali kati ya viongozi wa CHADEMA na Jeshi la Polisi kwenye mlango wa chumba cha kuhifadhi maiti (mochwari) cha Hospitali ya Rufani ya Mkoa Mwananyamala ulikohifadhiwa mwili wake.
Kibao anadaiwa kuwa jioni ya Septemba 6 mwaka huu, maeneo ya Kibo Complex Tegeta, Dar es Salaam, akiwa safarini kuelekea nyumbani kwake Sahare, mkoani Tanga na basi la Tashrif, alishushwa katika basi hilo na watu waliokuwa na bunduki.
Juzi Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime alisema wanafuatilia tukio hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika Hospitali ya Rufani ya Mwananyamala walikokwenda kutambua na kufanyia uchunguzi mwili wa marehemu, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, alisema wanatarajia kufungua kesi ili ukweli wa jambo hilo ufahamike na wahusika wachukuliwe hatua za kisheria.
Mbowe alisema uamuzi wa kufungua kesi umekuja baada ya kujiridhisha kuwa Kibao aliuawa.
Alidai kuwa hata mazingira ya kuchukuliwa kwa kada wao huyo yanaonesha kuwa alichukuliwa na vyombo vya dola kwa sababu mashuhuda waliokuwapo, waliwaona watu hao walikuwa wameshika silaha za moto (bunduki) wakiingia katika basi na kumchukua.
"Sisi kama chama tunaendelea kushauriana viongozi pamoja na familia ili katika hatua za baadaye tuone tunaweza kuchukua hatua gani za kisheria kwa sababu mtu huyu ameuawa na hatuwezi kuruhusu hali hii ikaendelea," alisema Mbowe.
Alisema kuwa baada ya kupata taarifa za kifo, walishauriana na ndugu wa marehemu na kukubaliana na mwanasheria wa chama ashiriki katika kufanyia uchunguzi mwili.
Alisema matokeo ya uchunguzi yameonesha kuwa Kibao aliuawa kwa kupigwa na kumwagiwa tindikali usoni.
"Sasa polisi ambao ndiyo watuhumiwa namba moja katika jambo hili na ndiyo wenye wajibu wa kulinda watu wa taifa hili, ni vigumu wao wenyewe kujichunguza, hivyo tunahitaji polisi pamoja na vyombo vingine vya usalama watoe ushirikiano kwa chama na familia, ili haki ipatikane na waliohusika wafikishwe kwenye vyombo vya sheria," alisema.
Mbowe alisema kuna mambo mengine ambayo bado yanafanyiwa uchunguzi na wanasubiri taarifa rasmi ya hospitali ambayo inatarajiwa kutolewa leo.
Alitoa angalizo kuwa kama taarifa hiyo itakuwa tofauti na vile wanavyotarajia, wataipinga kwa kuwa mawakili wa chama chao wanajua ukweli kwa kuwa walishiriki katika hatua zote za uchunguzi.
Mbowe alitoa pole kwa familia ya marehemu, ndugu jamaa na marafiki na wanachama wa CHADEMA kwa kupata msiba huo.
Wakati uchunguzi wa mwili wa marehemu ukiendelea katika chumba cha kuhifadhi maiti hospitalini huko, vilio na majonzi vilisikika kutoka kwa wanachama wa chama hicho.
Baadhi ya wanachama walisika wakitoa lawama kwa Jeshi la Polisi, wakidai linahusika na vitendo vya kikatili dhidi ya wanachama, wanaharakati na Watanzania.
VURUGU MOCHWARI
Ilipotimu saa 6: 56 mchana, kulitokea mvutano mkali baina ya polisi waliokuwa ndani ya chumba cha kuhifadhi maiti na viongozi wa CHADEMA, akiwamo aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob.
Mvutano huo ulidumu kwa takribani dakika 20 baada ya madaktari kumzuia Mwanasheria wa CHADEMA kuingia ndani ya chumba hicho, wakidai kuwa tayari kulikuwa na mwanasheria mwingine ndani ya chumba hicho.
CHADEMA ilipinga kauli hiyo na kusisitiza kuwa hawamfahamu wakili aliyekuwa ndani ya mochwari, kwamba wakili wao ni yule aliyesimama nje ya mlango.
Baada ya mvutano huo, uongozi wa hospitali pamoja na polisi walimruhusu wakili huyo kuingia ndani.
Chama cha ACT Wazalendo kimelaani taarifa za kutekwa na kuuawa kada huyo, kikisema kitendo hicho kinahusishwa na vyombo vya ulinzi na usalama.
Kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa na chama hicho jana, Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani, Dahlia Hassan alieleza kuwa chama hicho kimepokea kwa masikitiko taarifa hizo; kifo cha kada huyo kinaongeza idadi ya matukio ya utekaji, utesaji na mauaji ya raia nchini ambayo yanahusishwa na vyombo vya ulinzi na usalama.
Hivyo, kilimtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Camillus Wambura kuwaeleza wananchi wanaohusika na vitendo hivyo na Bunge liunde kamati maalum ya kuchunguza mauaji yote.
Kiongozi wa chama hicho, Doroth Semu, ambaye alikuwapo hospitalini kutambua mwili, alisema anasikitishwa na ukimya wa Jeshi la Polisi kuwafichua watekelezaji wa matukio hayo.
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla, pia ametoa pole kwa CHADEMA kufuatia kifo cha kada huyo.
"Sisi vyama vya siasa linapokuja suala la ubinadamu siasa unaweka kando. Niombe Jeshi la Polisi litimize wajibu wake wa uchunguzi wa jambo hili," alisema Makalla.
Makalla alitoa pole hizo wakati akihutubia wananchi wa Wilaya ya Simanjiro katika eneo la Mirerani, ikiwa ni sehemu ya ziara yake mikoa ya Arusha na Manyara.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED