Bunge lataka mashirika mzigo yafutwe

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 11:00 AM Apr 24 2024
SPIKA wa Bunge, Dk. Tulia Ackson.
PICHA: MAKTABA
SPIKA wa Bunge, Dk. Tulia Ackson.

SPIKA wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, ameitaka serikali kupitia Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji kukamilisha michakato ya kuunganisha na kufuta baadhi ya mashirika ya umma kisha kuuwasilisha bungeni kwa ajili ya kuvunjwa na kupitisha sheria mpya.

Dk. Tulia ametoa kauli hiyo bungeni wakati wa kupitisha makaridirio ya mapato na matumizi ya ofisi hiyo kwa mwaka 2024/25 na kusisitiza kuwa kwa sasa serikali haitakiwi kuthibitisha kufutwa kwa mashirika hayo kwa kuwa bado sheria  zilizopitishwa na bunge kuhusu kuanzishwa kwayo haijabatilishwa.

Spika ametoa kauli hiyo baada ya hoja iliyoibuliwa na Mbunge wa Kisesa (CCM),  Luhaga Mpina, kuhusu wizara hiyo kutaja kufutwa kwa mashirika ya umma manne na kuunganishwa mengine 16 ilihali Bunge halikushirikishwa katika mchakato huo.

Amesema  kama shirika lilianzishwa na sheria ya bunge  haliwezi kufutwa kwa mchakato nje ya bunge na kutolea mfano Tume ya Mipango kuwa ilifutwa na kurejeshwa bungeni, hivyo lazima taratibu zifuatwe.

“Hoja ya Mbunge Mpina ina mantiki maana katika ule uhalisia maelezo kama ya kamati namna yalivyoandikwa hapa na ufafanuzi ulioutoa hapa na hata mimi nilipoliona tangazo niliamini kwamba mko katika kupima shirika lipi litafutwa na yapi yataunganishwa,” amesema.

Aliitaka wizara hiyo pindi itakapokuwa imejiridhisha ipeleke sheria bungeni ili lifute sheria ya mashirika husika kupitia sababu zitakazowasilishwa bungeni hapo.

“Ili isilete mkanganyiko kauli ni kuwa wizara imetoa taarifa kuwa kuna hiyo nia ya kufuta kwahiyo mashirika yajieleze kama yanaona yana umuhimu au mengine yaungane na mambo kama hayo ili isionekane kama kuna utaratibu nje na utaratibu uliowekwa kisheria tulioutunga sisi wenyewe,” amesema Dk. Tulia.

Awali, akijibu hoja zilizoibuka bungeni, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof.Kitila Mkumbo, ametaja sababu za kufutwa kwa baadhi ya mashirika ya umma na mengine kuunganishwa kuwa ni pamoja na kujiendesha kwa hasara.

“Mfano mashirika yanakusanya Sh. trilioni 1.07 lakini yanatumia zaidi ya Sh. trilioni tatu, hivyo tukaona lazima yafanyiwe mabadiliko. Tuliyaunganisha  16 na kufuta manne na michakato kwa mengine bado inaendelea,” amesema Prof. Mkumbo.

Aidha, amelihakikishia bunge kuwa wafanyakazi katika mashirika yanayofutwa watapangiwa maeneo mengine ya kufanya kazi kutokani na taifa kuwa na uhitaji mkubwa wa watumishi hivyo hakuna atakaye kosa kasi kwa kufutwa au kuunganishwa kwa mashirika.

MIKAKATI KUWAINUA VIJANA

Miongoni mwa hoja zilizoibuka katika mjadala huo ni pamoja na mkakati wa kuwashirikisha vijana katika fursa mbalimbali za mipango na uwekezaji ambao walitajwa kutengwa licha ya kuwa zaidi ya asilimia 76 ya Watanzania.

Hoja hiyo imeibuliwa na Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Ng'wasi Kamani, na Mbunge wa Viti Maalum (CHADEMA), Sophia Mwakagenda,  waliotaka mikakati ya ushirikishwaji wa vijana ili kuwasaidia kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira.

“Kwa sasa asilimia kubwa ya Watanzania ni vijana kwa mujibu wa Sensa ya mwaka 2022 na wizara hii imesimama kati ya masuala muhimu ya kilimo, utalii, viwanda, uchukuzi na uchimbaji madini. Sasa ni vyema mipango yake ionyeshe namna ya kuwainua vijana ili washiriki kufikia maendeleo hayo,” amesema Kamani.

“Yawekwe mazingira mazuri kwa ajili ya kuwaunganisha vijana na wizara hii muhimu ikiwa ni pamoja na kupewa msingi mzuri wa kushiri, kujengewa uwezo wa kiuwekezaji katika sekta mbalimbali ili wawe sehemu ya kuliinua taifa hili kiuchuni,” amesema Mwakagenda.

Kutokana na hoja hizo, Prof. Mkumbo amelihakikishia Bunge hilo kuwa vijana watazingatiwa katika kujenga uchumi jumuishi kutokana na kuwa ni nguvu kazi, hivyo baada ya kufanya tathimini ya rasilimali watu na kupata picha waliopo na mahitaji pamoja na shirikishwa katika miradi ya kilimo na mifugo ya BBT, vijana watazidi kushirikishwa kikamilifu.