Bil. 190.7/- kuimarisha elimu sekondari Zanzibar

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:54 AM May 25 2024
news
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Elimu na mafunzo ya Amali Zanzibar, Lela Muhamed Mussa akiwasili katika viwanja vya Baraza la wawakilishi Zanzibar leo Tarehe 24,Mei 2024 Kuwasilisha Hotuba ya Makadirio ya Bajeti ya Wizara hiyo ya mwaka 2024-2025.

WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, imepanga kutumia Sh. bilioni 190.7 katika kuimarisha programu ya elimu ya sekondari.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Lela Muhamed Mussa, aliyasema hayo jana wakati akiwasilisha bajeti ya Mwaka wa Fedha wa 2024/25.

Alisema, kati ya fedha hizo Sh. 107,410,933,000 ni kwa ajili ya kazi za kawaida zikiwamo Sh. bilioni 13.6 kwa ajili ya matumizi mengine na Sh. bilioni 83.2 kwa kazi za maendeleo. 

Lela alisema hadi kufikia Aprili, mwaka huu, jumla ya Sh. bilioni 156.4 sawa na asilimia 82 zilipatikana. 

Alisema mapendekezo hayo yanaimarisha uongozi na usimamizi wa elimu katika ngazi zote za elimu zikiwamo skuli, wilaya, mkoa na wizara. 

Pia alisema fedha hzi zinalenga kuimarisha mfumo wa tathmini ya maendeleo ya elimu ya wanafunzi katika ngazi zote za elimu na kupandisha ufaulu wao kuimarisha miundonmbinu ya elimu. 

Aidha, alisema malengo mengine ni kujenga madarasa 1,500 kupitia ujenzi wa shule za ghorofa, shule za chini na kukamilisha madarasa yaliyoanzishwa na wananchi kwa Unguja na Pemba, nyumba 20 za walimu, ofisi ya wizara, ofisi nne za elimu wilaya, vyoo 300, dakhalia nane zikiwamo dakhalia za wanaume za Chwaka, Tumbe na Paje Mtule pamoja na kuzifanyia ukarabati mkubwa na mdogo skuli 100 za msingi na sekondari. Pia kujenga karakana elimu ya amali. 

"Skuli (shule 33 za sekondari Unguja na Pemba, karakana tatu kwa kila wilaya na kujenga uzio katika Skuli ya Sekondari ya Hasnuu Makame na Mohamed Juma Pindua kujengwa," alisema.  

Alisema kipaumbele kingine ni kuimarisha matumizi ya tekonolojia katika kufundishia na kujifunzia kwa kuziunganisha na mkonga wa taifa taaasi za elimu zikiwemo; skuli 217 za sekondari, vituo vya walimu 12 na vituo vya ubunifu wa kisayansi (hubs) 22 pamoja na kuzipatia vifaa vya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA). 

Waziri huyo alisema katika kuendelea kutekeleza mtaala mpya wa umahiri kwakuwapatia walimu mafunzo na vifaa vya kujifunzia na kufundishia vikiwemo vya Watoto wenye mahitaji maalumu.  

"Kuimarisha Mafunzo ya Ufundi na Amali kwa vyuo vitano vya Mafunzo ya Amali, utanuzi wa Chuo cha Karume (KIST) na ujenzi wa chuo cha ubaharia na kuzipatia vifaa," alisema. 

Pia alisema fursa ya upatikanaji wa mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu Zanzibar kuanzia ngazi ya diploma pamoja na kuanza mradi wa kujenga kampasi ya kudumu ya Chuo cha IIT Madrasa; Ujenzi wa Jengo la Skuli ya kilimo, Jengo la maabara ya Sayansi ya kisasa - SUZA, Ujenzi wa skuli ya Afya, skuli ya meno na kliniki yake -SUZA. 

Kipaumbele kingine, alisema ni kuimarisha huduma za maktaba kwa kuanza kujenga na kuimarisha maktaba mpya ya kisasa pamoja na maktaba mtandao (e-library).