BALOZI wa Tanzania nchini China, Khamis Omar, amesema kuwa Mkutano wa Nne wa Ushirikiano wa China-Afrika (FOCAC) utaimarisha ushirikiano na una fursa nyingi kwa maendeleo ya Watanzania.
Katika mahojiano maalum na Kituo cha Televisheni cha China cha CGTN, yaliyofanyika jana kuhusu matarajio yake juu ya mkutano huo na manufaa ya moja kwa moja kwa Watanzania, alisema utaendeleza pale walipoishia mwaka 2021 huku sekta za miundombinu, kilimo cha kisasa na teknolojia vikiwa kipaumbele.
Rais Samia yupo nchini China kwa ziara ya siku tano kuanzia Septemba 2 hadi 6, mwaka huu na tayari amefanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais Xi Jinping, ya kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo.
Balozi huyo alisema mjadala mkubwa ni kwenye uchumi, uhusiano kati ya watu, maendeleo,teknolojia masuala ya kimataifa, usalama na nishati safi.
"Tangu jukwaa hili lilipoanzishwa mwaka 2000, huu utakuwa mkutano wa nne wa FOCAC, na kila mtu ana matarajio makubwa kwa jukwaa hili, kwa sababu linakutanisha tena wakuu wa nchi na serikali kutoka Afrika na China, wanakutana na Rais Xi Jinping hapa. Watakuwa wenyeji na kujadili ushirikiano kati ya Bara la Afrika na China," alisema Balozi Omar.
Alisema uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na China umekuwapo tangu 1964, ikiwa ni miongo sita sasa ambao ulianza kwa kuwa na aina moja ya idiolojia sawa, imani sawa kuhakikisha uhuru wa nchi zote, mamlaka na umoja wa eneo, kujitolea kwetu dhidi ya ukoloni na ushirikiano.
"Uhusiano huo ulizidi kukua hadi kuwa uhusiano wa chama kwa chama, ushirikiano wa kiuchumi, uhusiano kati ya watu, na nyanja nyingine muhimu pia," alisema.
Alisema mwaka 2022 marais wa Tanzania na China walikubaliana kuimarisha uhusiano huo na kuwa wa kina zaidi kwa manufaa ya pande zote.
"Kuna maeneo muhimu matatu au manne. Moja ni kuhusu maendeleo ya miundombinu, wakati mwingine tunapozungumzia China na Tanzania, jambo la kwanza linalokuja akilini mwangu kama mimi mzee ni reli ya TAZARA.
"Hii ilikuwa mwanzo wa ushirikiano mkubwa wa miundombinu. Na tunavyofahamu, miundombinu ni muhimu sana kwa kufungua uchumi wa nchi yoyote, kuunganisha maeneo ya uzalishaji na masoko, kuunganisha nchi na sehemu nyingine za dunia,"alisema.
Alisema eneo la pili litakuwa upande wa uzalishaji, China, hata wakati wa miaka ya 1960 hadi sasa, imekuwa ikisaidia Tanzania katika maeneo ya uzalishaji, kilimo, utengenezaji.
Aidha, alisema kwa sasa kuna nguvu ya sekta binafsi pande zote mbili kwa kuwa kuna kampuni za Kichina zinazokuja Tanzania kwa ajili ya uwekezaji.
"China imekuwa mshirika wetu mkuu wa kibiashara, naona kwa miaka minane au tisa iliyopita. China ndiyo nambari moja kama mshirika wa kibiashara na tunavyofahamu, biashara ni muhimu sana kwa ustawi,bila kusahau sekta ya utalii," alisema.
Pia jana Rais Samia na Rais wa Zambia,Haikande Hichilema, wameshuhudia utiaji saini wa Hati za Makubaliano ya Uboreshaji wa Reli ya TAZARA.
Maeneo mengine ya kipaumbele kwenye mkutano huo ni uendelezaji wa miundombinu, kukuza uwekezaji, uendelezaji wa viwanda, kilimo cha kisasa, amani na usalama.
Aidha, Rais Samia anatarajia kuwa miongoni mwa wakuu wa nchi watakaohutubia ufunguzi wa mkutano wa FOCAC akizungumza kwa niaba ya ukanda wa Afrika Mashariki.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED