Migahawa yatakiwa kuweka vyakula vinavyoimarisha afya

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 10:02 AM Jan 04 2025
Makamu wa Pili mstaafu Balozi Seif Ali Iddi.
Picha:Mtandao
Makamu wa Pili mstaafu Balozi Seif Ali Iddi.

MAKAMU wa Pili mstaafu Balozi Seif Ali Iddi, amesema migahawa inayotoa huduma za chakula lazima ihakikishe inaweka vyakula vitakavyoimarisha afya za wananchi ili kupunguza maradhi.

Aliyasema hayo huko Bweni nje ya mji wa Zanzibar wakati akizindua eneo la biashara na michezo na eneo hilo litakuwa linatoa huduma mbalimbali ikiwamo za chakula ambalo limejengwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF).

Balozi Seif aliwataka wafanyabiashara watakaouza vyakula katika migahawa hiyo kuhakikisha wanauza vyakula safi vinavyoimarisha afya za wananchi na sio vinavyotoa afya za wananchi.

“Wale wanatakaohuduma katika migahawa hii mpike vyakula vinavyoimarisha afya zetu ili ziendelee kuwa imara na kupunguza maradhi,” alisema.

Alisema eneo hilo ambalo lina viwanja vya michezo litasaidia kuimarisha afya za wananchi kwa kufanya mazoezi ambayo ni muhimu katika kuimarisha afya za wananchi.

Aidha, alisema uwapo wa eneo hilo wazazi wataondokana na hofu kwa kuwa watoto wao watakuwa wanacheza katika sehemu salama.

Aliipongeza ZSSF kwa kujitahidi kukuza uchumi na kujenga maeneo ambayo yanatoa huduma mbalimbali kwa wananchi na kuwataka kutafuta maeneo mengine kwa ajili ya uwekezaji.

Alisema serikali kupitia taasisi zake zinajitahidi kuwekeza ili kuwarahisishia wananchi wake mahitaji mbalimbali ya kuondoa umaskini.

Naye Waziri wa Fedha, Dk. Saada Salum Mkuya, alisema licha ya kazi ya Wizara ya Fedha kuangalia sera ya fedha na uchumi, lakini ZSSF ndio inayowapa jeuri kwa sababu kazi ya mfuko huo ni kuwekeza fedha zinazokwenda kunufaisha wastaafu.

Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk. Malik Akili, alisema lengo la uzalishaji na miradi hiyo ni endelevu na alitaka taasisi zisizo za kiserikali kuwekeza katika mfumo wa huduma za jamii ili wananchi kupata maendeleo kwa sababu maendeleo yoyote ni gharama.