Mazao kupigwa mnada kwa televisheni

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:07 AM Jan 28 2025
Mkurugenzi Mkuu wa COPRA, Irene Mlola.
Picha: Mtandao
Mkurugenzi Mkuu wa COPRA, Irene Mlola.

MAMLAKA ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) imesisitiza mazao ya wakulima yatauzwa kufuata mfumo wa biashara wa minada ya kidigitali na stakabadhi ghalani kwa uwazi na haki kwa njia ya televisheni ili kuinua maisha yao kiuchumi.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa COPRA, Irene Mlola wakati akiwasilisha mwongozo wa biashara ya mazao ya ufuta, choroko, mbaazi, dengu na soya kwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha katika kikao cha wadau wa mazao hayo mkoani hapa. 

Irene, alisema katika kikao hicho kilichofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita kuwa mkulima atakapouza mazao yake kwa kufuata mifumo hiyo iliyowekwa na Serikali,  atakuwa huru kufuatilia akiwa katika kituo maalum au ghala kupitia televisheni na kushuhudia wanunuzi wakishindana kununua mzigo wake. 

Alisema uwazi huo utampa mkulima mkusanyaji mazao, fursa ya kuuza mazao yake kwa bei ya maslahi na endapo bei haitakuwa ya maslahi, mtunza mali anaweza kuamuru kusitisha kuuza mazao kusubiri bei itakayompa faida.

"Wakulima tumieni fursa ya kuuza mazao inayotolewa na serikali ni ya wazi na itawasaidia kupata faida kubwa kwa sababu inafanywa kwa uwazi," alisema Irene.

 Alisisitiza kuwa vipimo rasmi vinavyotambuliwa na wakala wa vipimo nchini, vitatumika kupima mali ya wakulima ili biashara ifanyike kwa haki na hakutakuwa na nafasi ya kufanyika udanganyifu na dhuluma kwa wakulima.

Kwa upande wake, Anamringi, aliahidi serikali ya mkoa huo kushirikiana na COPRA na taasisi zinazosimamia mwongozo wa biashara ili kumnufaisha mkulima.

Alisema kikao cha pamoja na wadau wa mazao hayo mkoani hapa, kitatoa muelekeo wa mikakati ya kufanya kuhakikisha wakulima wananufaika na bei za ununuzi kwa njia ya minada ya kidijitali.

"Nawashkuru sana COPRA kwa kuja Shinyanga kufanya kikao pamoja na serikali ya mkoa. Nawahakikishia wakulima wa mazao hayo watarajia mambo makubwa kwenye ununuzi na uuzaji wa mazao kwa njia ya minada," alisema.

 Aliwaagiza wakuu wa wilaya na wakurugenzi watendaji wa halmashauri za mkoa huo kushirikiana na COPRA, Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), Soko la Bidhaa Tanzania (TMX) na Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) kuhakikisha biashara ya mazao hayo inafanyika kwa mafanikio kwenye maeneo yao kwa kufuata mwongozo.

 Alisema lengo la serikali ni kuona wakulima wananufaika na kilimo cha mazao yanayolimwa kwenye maeneo yao na kukusanya kodi kwa kutoza ushuru.