JESHI la Magereza nchini limeanza kutumia nishati safi ya kupikia katika magereza yake mbalimbali nchini ili kusaidia kupunguza uchafuzi wa mazingira na kundokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini, Kamishna Jenerali Jeremiah Katungu, alisema hayo jana wakati wa Baraza la mwisho la Maofisa Magereza na askari wa jeshi hilo lililofanyika Msalato, Dodoma.
Alisema kuanza kutumia kwa nishati safi ya kupikia katika Magereza mbalimbali nchini ni moja ya mafanikio makubwa waliyopata jeshi hilo ndani ya utekelezaji wa majukumu yao kwa mwaka 2024.
"Haya ni mafanikio makubwa sana tumeyapata katika mwaka 2024, tunaendelea kuboresha ili kuhakikisha nishati safi ya kupikia inatumika katika magereza mbalimbali hapa nchini," alisema Kamishna Jenerali.
Alisema pia jeshi hilo limeanza kutumia mfumo wa Ofisi Mtandao (E-Office) kwa makao makuu kwa ajili ya kusikiliza kesi za wafungwa na mahabusu kwa njia ya mtandao.
Kamishna Jenerali Katungu alisema hiyo ni hatua kubwa kwa jeshi hilo kwa sababu inarahisisha utendaji kazi wa jeshi na inachangia kupunguza msongamano wa mahabusu katika maeneo mbalimbali nchini.
Kutokana na mafanikio hayo, Kamishna Jenerali Katungu alishukuru serikali kutokana na uwekezaji unaofanywa ndani ya jeshi hilo na kufanya kazi zake kwa ufanisi.
Akielezea tathmini ya jeshi hilo kwa mwaka 2024, alisema kwenye mafanikio waliyopata ni pamoja na kupungua msongamano wa wafungwa na mahabusu gerezani, ikiwa ni matokeo ya ushirikiano mzuri uliopo baina ya vyombo vya haki jinai ikiwamo Mahakama, Jeshi la Polisi, Idara ya Uhamiaji, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka na wadau wengine.
Alisema, mafanikio mengine ni pamoja na programu za urekebishaji magerezani kwa wafungwa zikihusisha, ushauri nasihi, kilimo, utunzaji wa mazingira, michezo na urasimishaji wa ujuzi kwa Mamlaka ya Ufundi Stadi VETA na kutoa vyeti kwa wafungwa.
Pia, alihimiza ushirikiano, umoja na upendo miongoni mwa maofisa na akitumia fursa hiyo kuwakumbusha kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga kura, ili wapate fursa ya kuchagua viongozi katika Uchaguzi Mkuu 2025.
Awali, akimkaribisha Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini, Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza (CP) Nicodemus Tenga, alimshukuru CGP Katungu kwa kuandaa Baraza hilo ili kutoa tathmini ya utendaji wa Jeshi kwa mwaka mzima na kuwataka watendaji wote kufanya kazi kwa juhudi na maarifa ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED