Kilimo cha mwani kuwekewa mkakati kuinua vipato

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 06:50 AM Apr 20 2024
Kilimo cha mwani.
Picha: Maktaba
Kilimo cha mwani.

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imesema imejipanga kuendeleza njia za kitaalamu za ukulima wa mwani kuongeza uzalishaji pamoja na kuinua kipato cha wakulima wa zao hilo nchini.

Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Uvuvi na Mazao ya Baharini, Dk. Salum Sudi Hamed, alisema hayo jana Muongoni, Mkoa wa Kusini Unguja wakati akikabidhi boti ya kuvunia mwani iliyotolewa na Taasisi ya The Nature Conservancy (TNC), inayoshughulika na utunzaji wa mazingira ya kimataifa ikiwa ni kuelekea shamrashamra za sherehe za Muungano ambazo hufanyika kila mwaka April 26.

Alisema zao la mwani linafaida kubwa katika ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja na taifa hivyo serikali itashirikiana na wadau wa maendeleo kutafuta njia mbadala za kuwasaidia wakulima wa zao hilo ili kujiongezea kipato.

Aidha, alisema moja ya mkakati wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi, wakulima wanaongeza uzalishaji wa zao la mwani Wizara inaendelea kutoa elimu kwa wakulima kuwafundisha njia za kitaalamu pamoja na kuwapatia vifaa vya kitaalamu lengo kuona wakulima hao wanafanya kazi zao kwa urahisi na njia za kitaalamu.

Aliwataka wakulima kutunza mazingira wakati wanapofanya shughuli za kilimo hicho ili kukabiliana na ma mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumzia kuhusu bei ya mwani, Mkurugenzi Salum alisema wizara inaendelea na ujenzi wa kiwanda cha kusarifu mwani na ujenzi utakapomalizika wananchi watakuwa na sehemu maalum ya kuuza bidhaa ya mwani.

Mwakilishi kutoka taasisi ya TNC, Ayubu Misheli Singoye, alisema lengo la kutoa boti kwa wakulima wa zao la mwani katika Kijiji Cha Muongoni ni kurahisisha shughuli za uvunaji wa zao hilo wakati wa mavuno kwa wakulima.

Alisema taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwamo Zanzibar kutoa elimu ya utumzaji wa mazingira ya bahari kuona shughuli za kilimo cha mwani hakiathiri mazingira ya bahari.