Bodaboda wakumbushwa kutimiza wajibu kisheria

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:44 AM Apr 28 2024
Meneja wa TRA Mkoa wa Kagera, Castro John.
PICHA: MAKTABA
Meneja wa TRA Mkoa wa Kagera, Castro John.

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imesema mabadiliko ya sheria yaliyofanyika Julai 2023 yanataka wafanyabiashara na wamiliki wa pikipiki maarufu kama bodaboda kulipia Sh. 65,000 kama kodi ya shughuli za usafirishaji wanazozifanya.

Kauli hiyo ilitolewa na Meneja wa TRA Mkoa wa Kagera, Castro John, wakati akitoa taarifa ya robo mwaka katika ukusanyaji wa mapato kwa mkoa huo.

Amesema bodaboda wamekuwa wakifanya shughuli zao bila kutoa kodi kama wafanyabiashara wengine ambao wanafanyiwa makadirio ya uzalishaji shughuli zao kwa mwaka.

Amesema kodi hiyo inatakiwa kulipiwa kwa awamu nne, ambapo robo moja ya mwaka mfanyabiashara huyo atalipa Sh. 16,200.

“Tumekuwa tukizungumzia suala hili kupitia vikao, lakini mwitikio wa bodaboda kuja kufanyiwa makadirio ni kidogo, na tayari sheria imeshapitishwa na siyo lazima mtu alipe kwa pamoja, ataweza kulipia kidogo kidogo hadi anakamilisha malipo ya mwaka,” amesema John.

Amesema endapo malipo yakikamilika atapatiwa utambulisho wa chombo chake kwa kupewa stika ya mapato ilifanyiwa makadirio.

John amesema jambo lingine ambalo limekuwa tatizo katika kwa vyombo vya moto ni ubadilishaji umiliki pindi chombo kimeuzwa.

Amesema kufanya hivyo ni kumwepushia malalamiko mmiliki wa pili endapo chombo hicho kilikuwa kikifanya au kitafanya uhalifu.

“Hii inasaidia kwani kumekuwa na malalamiko kwa watu kuwa, pikipiki imekamatwa ikifanya uhalifu sehemu na umiliki unasoma yule mtu wa kwanza au mtu ameinunua pikipiki inakwenda kufanya uhalifu,” amesema Castro.

John amesema kinachotakiwa ni kubadilisha vitu kama mkataba, unaoambatana na kadi na uhamisho wa umiliki.