Askari uhifadhi wapigwa msasa biashara haramu wanyamapori

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 06:44 AM May 04 2024
Pembe za ndovu zilizo kamatwa baada ya wawindaji haramu kuua wanyama hao.
Picha: Mtandaoni
Pembe za ndovu zilizo kamatwa baada ya wawindaji haramu kuua wanyama hao.

SHIRIKA la World Wildlife Fund (WWF), limeanza kuwapiga msasa askari wa Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Enduimet (WMA) na Wilaya ya Longido, mkoani Arusha kuhusu namna bora ya kukabiliana na biashara haramu ya wanyamapori na kuheshimu haki za binadamu.

Askari 38 kutoka Enduimet WMA na Jumuiya mpya ya Uhifadhi ya LOKEEN-NATRON, wanajifua kwa wiki nne kuhusu ukamataji salama wa watuhumiwa ili kuwezesha kusaidia kesi mahakamani kuwa na ushahidi wa uhakika usioacha shaka ndani yake.

Meneja Mradi wa WWF, Gasto Mushi, alisema jana kuwa mradi huo unalenga kuiwezesha jamii kujishughulisha na shughuli za uzalishaji mali, kutoa mafunzo ya ulinzi wa wanyamapori, kutoa elimu kwa jamii kupitia klabu za mazingira shuleni na kuboresha ushirikianao na ujirani mwema kati ya Tanzania na Kenya. 

"Tunatarajia kupitia mafunzo haya ambayo askari wetu wamepatiwa, yatakuwa chachu ya kuwawezesha kutokomeza biashara haramu ya wanyamapori katika eneo la Enduiment na Wilaya nzima ya Longido, kwani kwa mafunzo haya, matukio yatakuwa yakiripotiwa kabla hayajatokea au uhalifu kufanyika," alisema Mushi.

Mafunzo hayo yanaendeshwa na WWF, kupitia miradi miwili IWT (Illegal Wildlife Trade) na BMZ Unganisha. 

Kwa mujibu wa Mushi, miongoni mwa mafunzo waliyopatiwa askari hao ni pamoja na elimu juu ya biashara haramu ya wanyamapori na namna ya kuendesha operesheni mbalimbali.

 Imo pia elimu juu ya biashara haramu ya mihadarati, mafunzo ya ukamataji salama wa watuhumiwa ili kuweza kusaidia kesi katika mahakama, elimu ya rushwa, utaratibu wa ukusanyaji wa vidhibiti mbalimbali, elimu ya haki za binadamu, ukusanyaji wa kodi pamoja na udhibiti wa mipaka. 

Aidha, Mwenyekiti wa Enduimet WMA, Parsanga Mollel, aliomba wafadhili waliowezesha mafunzo hayo kwa askari, kuyafanya kuwa endelevu huku akiwapongeza  askari hao kwa kuhitimu mafunzo yao, akiwataka kuyafanyia kazi ili yawe na manufaa kwa jamii ya Longido na taifa zima.

 "Naomba niwajulishe kuwa mafunzo mliyoyapata ni bahati kwani kuna wengine waliyo tamani lakini hawajapata, hivyo niwape hongera na mkayafanyie kazi yote mliyo fundishwa kikubwa mkawe na heshima kwani hakuna kazi bila heshima," alisisitiza Mollel.

 Akifunga mafunzo hayo, Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Longido, Mwazani Mohamed, alisema mafunzo hayo yameandaliwa kimkakati ili kuwaongezea ujuzi, nidhamu, ufahamu na uelewa wa namna bora ya kutatua changamoto ambazo zimekuwa zikizunguka eneo la Enduimet WMA.

 "Tunatarajia kupata matokeo chanya kutokana na mafunzo kutoka idara mbalimbali waliyo patiwa askari, lakini pia ni muhimu kuwasaidia wananchi kufikia malengo katika uhifadhi na ufugaji na hii itasaidia kupunguza migongano baina ya binadamu na wanyama," alisema.