HASIRA za Yanga kutolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi, jana ziliishia kwa Copco FC, ilipoibugiza mabao 5-0 katika mchezo wa raundi ya tatu Kombe la FA uliochezwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.
Mabao ya Yanga kwenye mchezo huo yalifungwa na Shekhan Ibrahim, Prince Dube, Maxi Nzengeli, Duke Abuya na Mudathir Yahaya.
Copco, yenye maskani yake jijini Mwanza ilionekana kuidhibiti Yanga kipindi cha kwanza iliporuhusu bao moja tu, lakini ilishindwa kabisa kufanya hivyo kipindi cha pili na kuruhusu mvua ya mabao.
Katika mchezo huo, ilishuhudiwa Yanga ikimchezesha kwa mara ya kwanza beki wake, Israel Mwenda huku Jonas Mkude akianza kipindi cha kwanza kama beki wa kati.
Yanga ilifanikiwa kupata bao la kwanza dakika ya 35 lililofungwa kwa kichwa na Shekhan aliyeruka juu mbele ya wachezaji watatu wa Copco na kupiga kichwa mpira wa kona uliopigwa na Farid Mussa lililodumu hadi mapumziko.
Kwa dakika zote 45 za kwanza, kipa wa Yanga, Aboutwalib Mshery ni kama alikuwa yuko likizo, kwani alidaka mpira mara mbili tu ambayo yote haikuwa na madhara yoyote.
Kazi nzuri iliyofanywa na Mkude akipeleka mpira kwa Mwenda ambaye aliupiga mpira mrefu kwa Dube ilizaa bao lililofungwa na Mzimbabwe huyo baada ya kumtoka beki, Amos Mgeta na kuukwamisha mpira wavuni dakika ya 57.
Nzengeli aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Abobakar Salum alifunga bao la tatu kwa mkwaju wa penalti dakika ya 68, baada ya yeye mwenyewe kuangushwa ndani ya eneo la hatari.
Kama vile haitoshi, Abuya alipachika bao la nne kwa kichwa akiunganisha krosi kutoka wingi ya kushoto iliyomiminwa na Nickson Kibabage dakika ya 77, kabla ya Mudathir ambaye naye aliingia kipindi cha pili kupigilia bao la tano akifunga pia kwa kichwa kufuatia krosi ya Mwenda.
Yanga walikuwa na nafasi ya kupata ushindi mkubwa zaidi kama kiungo wake Aziz Ki angezitumia vyema nafasi alizopata katika dakika za 14 na 15.
Matokeo hayo sasa yanaitupa nje ya mashindano Copco FC huku Yanga ikisonga mbele.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED