Maagizo sita kwa Ma-DC mfumo taarifa za watu wenye ulemavu

By Augusta Njoji , Nipashe Jumapili
Published at 12:33 PM Jan 26 2025
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
Picha: Mtandao
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, ametoa maagizo na maelekezo sita kuhusu mfumo wa taarifa za watu wenye ulemavu kwa wakuu wa wilaya ikiwamo kuhakikisha ofisi za ustawi wa jamii katika halmashauri zinawapokea, kuwasikiliza na kuwahudumia wananchi wenye ulemavu.

Amesema kwa mujibu wa matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, asilimia 11.2 ya watu wote nchini wana ulemavu wa aina fulani huku Zanzibar ikiwa na asilimia 11.4 ambapo idadi kubwa zaidi ni wanawake kwa asilimia 11.6 na asilimia 10.9 ya wanaume.

 Akizindua mfumo huo jana jijini hapa, Majaliwa alisema ni mara ya kwanza Tanzania kuuandaa na ni nyenzo muhimu kwa serikali, wadau wa maendeleo na watunga sera katika kupanga, kutekeleza, na kufuatilia maendeleo ya watu wenye ulemavu nchini.

Waziri Mkuu alisema matokeo ya sensa yanabainisha ulemavu wa kuona ndio unaoongoza ukiwa na asilimia tatu ya watu wote wenye ulemavu.

“Kiwango hiki kinafuatiwa na ulemavu wa kutembea asilimia 1.8 na ulemavu wa kusikia asilimia 1.1  na watu wenye ualbino asilimia 0.1,” alisema.

Majaliwa alizitaka taasisi zote za umma, sekta binafsi, asasi za kiraia na wadau wa maendeleo kushirikiana na serikali katika kutumia mfumo huo kikamilifu kwa kufanya muamuzi wenye vigezo vya kitakwimu katika kupanga na kufuatilia utekelezaji wa sera, mipango na afua mbalimbali zinazolenga kukuza na kuimarisha maendeleo ya watu wenye ulemavu.

Pia alisema Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania Bara (SHIVYAWATA) na Shirikisho la Jumuiya za Watu Wenye Ulemavu, Zanzibar (SHIJUWAZA) watumie takwimu hizo kuhuisha kanzidata zao.

“Taasisi zote zinazotoa huduma kwa watu wenye ulemavu tumieni takwimu hizi  katika kutayarisha programu za kuwawezesha na kuwajengea uwezo watu wenye ulemavu kutumia fursa mbalimbali zinazotolewa na serikali na wadau wa maendeleo kujiendeleza kiuchumi, kijamii na mazingira,” alisema.

Aliwataka wazazi na walezi wote wasiwafiche watoto na watu wenye ulemavu na wahakikishe wanafahamika mahali walipo pamoja na hali zao za ulemavu.

Alisema lengo ni kupata huduma stahiki huku akiwataka watekelezaji na wasimamizi wa miradi mbalimbali ya ujenzi wahakikishe uwapo wa miundombinu sahihi kwa ajili ya watu hao.