ZIKIWA zimepita wiki kadhaa ikishuhudiwa kusambaa kwa picha jongefu za askari wa usalama barabarani wakipokea rushwa hadharani kisha kuchukuliwa hatua, hali ya namna hiyo ni ya kawaida kwa muda mrefu mkoani Kigoma na imekuwa kama utaratibu wa kawaida na halali.
Askari wa usalama wa barabarani kutumia vituo vya ukaguzi kama sehemu ya kitegauchumi wakitoza fedha kwa kila gari linalopita kinyume cha utaratibu huku wakiita utaratibu huo kuwa ni pesa ya ‘ushirikiano’.
Kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura Namba 329 marejeo ya mwaka 2022 kifungu namba 15, hatua yoyote ya kuahidi, kutoa, kupokea au kushawishi moja kwa moja au kupitia kwa wakala, kitu chochote cha thamani ili kupindisha utaratibu katika utoaji wa uamuzi inatafsiriwa kuwa ni rushwa.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) inataja rushwa ni hatua na athari ya ufisadi, ambayo ni mchakato wa kuvunja kwa makusudi utaratibu wa mfumo, kimaadili na kiutendaji kwa faida ya kibinafsi.
TAKUKURU inaenda mbali zaidi na kubainisha kuwa mbali na mafisadi kufanya kitendo kisicho halali, pia wanashinikiza au kulazimisha wengine kufanya vitendo kama hivyo.
KINACHOENDELEA
Katika safari ya kilometa 27 aliyoifanya mwandishi wa ripoti hii kutoka Kigoma Mjini mpaka eneo la Mkuti, kwenye vituo saba vya ukaguzi ambako anashuhudia kila kituo, msaidizi wa dereva anashuka kupeleka ‘makusanyo’ kwa askari na gari kuruhusiwa kupita bila kufanyiwa ukaguzi.
Fedha anazozibaini zikitolewa katika kila kituo ni kuanzia Sh.2,000 mpaka 5,000, bila maandishi yoyote wala risiti hali inayotajwa kuwa sehemu ya upotevu wa mapato ya serikali kwa kuwa fedha hizo zinaishia katika mifuko ya watu.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Umoja wa Wasafirishaji Kigoma (KIBOTA), zaidi ya magari 1,190 yanalazimika kutoa hongo kila yapitapo kwenye kila kizuizi.
Magari hayo yanajumuisha daladala 867, mabasi madogo 123, michomoko na Toyota Wish 200 pamoja na magari binafsi yanayofanya safari kati ya wilaya za Kigoma, Kasulu, na Uvinza.
Kwa hesabu ya kila gari kutozwa wastani wa Sh.2,000 kwa kila kituo katika vituo saba ni sawa na Sh.14,000 na magari 1,190 kwa hesabu hiyo, yanatoa zaidi ya Sh. milioni 16.6 kwa siku, kwa mwezi zaidi ya Sh. milioni 499.8 ambazo haziingii katika mifumo rasmi ya ukusanyaji mapato.
Fedha hiyo ambayo hupotea kila siku katika vizuizi vya ukaguzi vya polisi wa usalama barabarani vilivyoko barabara kuu iendayo Kasulu kutoka Kigoma Mjini kwa siku moja, ingeweza kutumika kujenga darasa moja la shule ya msingi lenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 40 na kupunguza uhaba wa madarasa unaoikumba jamii ya mkoa huo.
Aidha, fedha hiyo kama ingekuwa kwenye ukusanyaji wa utaratibu maalum na wa kisheria, ingeweza kutumika kufanya marekebisho ya barabara hizo.
Kwa kipindi cha mwaka 2022 hadi 2024, Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Kigoma umeeleza kutumia zaidi ya Sh. milioni 17 katika marekebisho ya miundombinu ya barabara iliyoharibiwa ikiwamo uharibifu wa tabaka la juu la lami na uharibifu wa makalavati na mitaro.
Katibu wa KIBOTA, Nuru Hussein, anakiri barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 90, kilometa 27 za awali kuna zaidi ya vizuizi saba.
Anasema katika barabara hiyo, kuna vituo vya ukaguzi vya Stendi Mpya ndani na nje - kwa Mganza (Kazegunga), Nyangwe, Simbo, Mkuti na Baraka Sekondari. Vyote hivyo vimo ndani ya kilomita 27 kutoka Kigoma Mjini sambamba na magari ya ukaguzi wa madeni huku eneo la Kazegunga likigeuka kuwa sehemu maarufu ya ukaguzi unaotawaliwa na rushwa.
“Katika kila kizuizi na gari la ukaguzi, kila gari hulazimika kutoa kati ya Sh. 2,000 hadi 5,000 kama pesa ya ushirikiano, hii ni mbali na ushuru wa kawaida, kwa hiyo kwa siku dereva anaweza kutoa kati ya Sh. 15,000 na 20,000 ya ‘ushirikiano’. Hii inatuumiza sana” anasema.
Madereva, anasema halazimika kutoa pesa hizo ili kuepuka usumbufu au adhabu zisizo za haki kwa kuwa madereva wanaoshindwa kutoa fedha hizo, mara nyingi hukumbwa na adhabu kubwa kama faini au kucheleweshwa safari, hali inayowaathiri kiuchumi, huku baadhi ya madereva wakilazimika kujaza abiria kupita kiasi ili kufidia gharama hizo.
Katibu huyo anasisitiza kuwa katika barua yao ya Mei 30, 2024 yenye kumbu Na KBT/KG/ML/VOL/30/2024 kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma walilalamika kuhusu ongezeko la vizuizi vya polisi katika barabara hiyo.
Anasema katika barua hiyo, waliomba kupunguzwa kwa vizuizi kwa madai kuwa ongezeko lake ni ishara ya kukithiri kwa rushwa ambayo dereva na kondakta wanapaswa kulipa.
Katika uchunguzi huo, mwandishi anabaini utaratibu huo ni wa kawaida na uliozoeleka kwa wasafirishaji hao. Katika kituo cha kwanza, kondakta anaonekana kushuka mkononi akiwa ameshikilia kitu na kwenda kwa askari ambaye anapokea kama salamu na kuruhusu gari kupita.
Kinachobainika pia katika vizuizi hivi, kuna kiwango maalum wanachokihitaji askari hao kwa kuwa katika kituo kimoja, mwandishi licha ya kutokusikia sauti ya kinachozungumzwa, anabaini askari akichukua fedha kisha kurejesha chenji.
Mwenyekiti wa daladala, maarufu kama michomoko, Sinda Zacharia, anasema suala hilo limedumu kwa zaidi ya miaka 10 na hakuna mabadiliko yoyote, hata yakitokea hudumu kwa muda mfupi.
“Imefika hatua tumezoea hii hali. Tuwe na hela tusiwe nazo tunafanya maandalizi ya fedha ya ‘ushirikiano’ ili asubuhi tukipita tuwaachie kwa sababu tusipofanya hivyo hali inakuwa mbaya barabarani.
“Matrafiki wana daftari la orodha ya madereva wanaopita katika barabara hiyo. Wanaweka kumbukumbu nani kalipa na nani hajalipa. Ambaye amelipa anaachiwa huru ambaye hajalipa anapaswa kulipa au la ataandikiwa faini hata kama kosa lake ni la kupewa elimu ili kumkomesha na kumrejesha kwenye pesa ya ‘ushirikiano,” anasema kiongozi huyo.
Msimamizi wa usafirishaji mkoa (jina linahifadhiwa kwa sababu za kiusalama), anasema rushwa kati ya madereva na makondakta na trafiki iko pia kwa mabasi yanayofanya safari nje ya mkoa. Basi haliruhusiwi kuondoka bila kuacha Sh. 20,000 kwa askari anayefanya ukaguzi.
“Ukifika stendi saa 10:00 alfajiri utaona hiki ninachokisema. Askari anakaa ndani ya gari hashuki, anasubiri kupelekewa Sh. 20,000 ndipo anashuka na kufanya ukaguzi abiria wakiwa wameshapanda mabasi,” anabainisha.
Pia anasema kwa mabasi ambayo yanashindwa kulipa, abiria wanashushwa na kufaulishwa kwenye mabasi mengine, hivyo kutokuruhusiwa kuendelea na safari.
RPC ANENA
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Philemon Makungu anasema tuhuma hizo hazijafikishwa ofisini kwake na kwamba atalifanyia kazi kubaini ukweli wake.
“Kila mtu atimize wajibu wake badala ya kutuhumiana. Kama yupo mwenye kuthibitisha hilo anapaswa kutoa taarifa ili sheria ichukua mkondo wake kwa kuwa usalama barabarani unaongozwa na sheria,” anasema Makungu.
Kuhusu ongezeko la vizuizi, anasisitiza kuwa vinaboresha hali ya ulinzi na usalama barabarani na vimesaidia kupunguza ajali licha ya kutokutoa takwimu kuonesha kupungua huko.
Makungu anawataka wananchi kutoa taarifa ya vitendo viovu vinavyofanywa barabarani ili jeshi liweze kuchukua hatua na kwamba ipo namba ya simu iliyotolewa kwa ajili ya kushirikiana nao katika utekelezaji wa majukumu kama hayo hivyo wasikae kimya.
“Tunataka wananchi wahudumiwe vizuri, hatuwezi kufumbia macho vitendo viovu vinavyofanyika katika vizuizi vyetu, wananchi watoe taarifa ili sheria ziweze kuchukua mkondo wake,” anasema Makungu.
Pamoja na kauli ya Kamanda Makungu, suala la vizuizi kuwekwa katika barabara hiyo halijazuia kutokea kwa ajali za mara kwa mara.
Taarifa kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, zinabainisha kuwa kwa mwaka 2023 pekee, kulikuwa na majeruhi 408 na vifo tisa vilivyotokana na ajali za barabarani na hadi kufikia Agosti, 2024 tayari kulikuwa na majeruhi 411 na vifo vya watu wanane.
Kadhalika takwimu za hali ya uhalifu na matukio ya usalama barabarani ya Januari mpaka Desemba 2023, katika mikoa ya kipolisi Tanzania, mkoa wa Kigoma ulikuwa na matukio ya ajali 61, ajali na vifo 40, ajali za majeruhi 19 na ajali za kawaida mbili, katika ajali hizo walifariki watu 52 na waliojeruhiwa kuwa 78.
Taarifa hiyo imeeleza chanzo cha ajali kuwa ni kuchangiwa na ubovu wa magari kwa asilimia 4.1, hali inayoonesha kuwa vyombo hivyo havikaguliwi ipasavyo.
Kuhusu ukaguzi wa magari kila asubuhi, Ofisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Usafiri Ardhini (LATRA) Mkoa wa Kigoma, Addo Msigala, anasema wanafanya hivyo mara kwa mara ili kuhakikisha sheria ya usalama barabarani zinazingatiwa.
Anasema kutokana na ukaguzi huo kwa kipindi cha Januari hadi Novemba 2024 madereva walikokiuka sheria waliadhibiwa kwa makosa mbalimbali yanayohatarisha usalama barabarani yakiwamo kuvaa sare chafu (12) kuchanganya mizigo na abiria(saba) na abiria,kutotoa tiketi(14) na kusimamisha abiria (20).
Kanuni za ukaguzi wa magari ya mwaka 2023 zinaelekeza kuwa mkaguzi anatakiwa kutoa orodha ya kasoro na muda wa kuzirekebisha, lakini hali ni tofauti kwenye barabara ya Kasulu ambako askari anasimamisha gari na kumsubiri dereva ashuke na kumfuata alipo.
TAKUKURU YATHIBITISHA
Mkuu wa Kitengo cha Elimu kwa Umma kutoka TAKUKURU Mkoa wa Kigoma, Ibrahim Sadick, anasema asilimia 67 ya maoni ya wananchi yaliyokusanya kwa kipindi cha Machi, 2023 hadi 2024, yanaonesha rushwa imetawala utendaji wa polisi wa usalama barabarani.
Kadhalika, ripoti ya Kupambana na Rushwa Barabarani kwa Mwaka 2023 kipengele cha rushwa barabarani, Jeshi la Polisi lilirekodi matukio 1,250 ya rushwa barabarani, ikilinganishwa na matukio 1,100 yaliyoripotiwa mwaka 2022.
Pia utafiti wa uliofanywa na TAKUKURU 2022/23 ulilitaja Jeshi la Polisi kuwa msatari wa mbele likiwa na 55.6 kati ya vinara wanne.
MADEREVA WANG’AKA
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wa habari hii, baadhi ya madereva ambao hawakupenda kutajwa majina yao na wadau wengine wa usalama barabarani, wanasema rushwa inaathiri maisha ya jamii na kukiuka misingi ya utwala bora.
Dereva wa kwanza analalamika kuwa anapata kipato kidogo na hivyo kushindwa kuhudumia familia yake ipasavyo na kuzua ugomvi nyumbani kwake huku mke wake akimtuhumu kwa matumizi mabaya ya pesa.
“Kwa mzunguko mmoja tunapata Sh. 112,000 ambayo nalipa pesa ya chama Sh. 2,000, mafuta naweka ya Sh. 60,000, mwenye gari namlipa Sh. 40,000, ushuru Sh. 1,000/= na ‘ushirikiano’ Sh. 15,000. Pesa yote inaisha ili nipate ziada inabidi nijaze abiria zaidi au nipakie mizigo,” anasema dereva huyo.
Dereva mwingine anasema wanaposhindwa kulipa pesa ya ‘ushirikiano’, askari wanawalipa visasi na kuwaita majina magumu kama “jiwe” au “nati” na hata kuwabambikia makosa ili walipe faini ya Sh. 30,000 kwa kosa ambalo lingehitaji elimu peke yake.
Katibu Tawala Msaidiai anayeshughulikia Mipango na Uratibu Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Frank Makua, anasema kutokana na rushwa serikali inaweza kupoteza wawekezaji ambao wataingia mkoani Kigoma na kuufanya mkoa huo kuwa kitovu cha biashara kama inavyokusudiwa.
Pia anasema wafanyabiashara wengi watakimbia kufanya biashara ambazo zinawaingizia hasara na kuanza kufanya biashara za mitandao ambapo serikali itapoteza kodi na hivyo kuathiri miradi ya maendeleo.
“Mapato yanayochepushwa yanachangia kutofikiwa kwa malengo ya utekelzaji wa miradi ya maendeleo na kuondoa umaskini kama ilivyoanishwa katika Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG) lengo la kwanza la kutokomeza umaskini kwa kila hali.
Itaendelea...
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED