Serikali yasisitiza kukua utalii hifadhi za taifa

By Ibrahim Joseph , Nipashe Jumapili
Published at 02:50 PM Jan 26 2025
Msemaji wa Serikali, Gerson Msingwa
Picha: Mtandao
Msemaji wa Serikali, Gerson Msingwa

SERIKALI imetaja mambo manane ya maendeleo yaliyotekelezwa na kusisitiza kwamba, utalii kwenye Hifadhi za Taifa umeendelea kukua na mapato kuongezeka.

Msemaji wa Serikali, Gerson Msingwa, akizungumza jana katika mkutano wake na waandishi wa Habari uliofanyika Hifadhi ya Mikumi, mkoani hapa, alisema takwimu zinaonesha mwaka 2023/24, watalii 1,863,108 walitembelea Hifadhi za Taifa.

Msigwa alisema idadi hiyo imeongezeka ikilinganishwa na watalii 1,618,538 waliotembelea Hifadhi za Taifa mwaka 2022/23 ambalo ni ongezeko la watalii 244,570, sawa na asilimia 15.1.

Kuhusu maendeleo ya Shirika la Reli Tanzania (TRC), alisisitiza kwamba linatekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati na mingine imefikia hatua ya kuanza kutoa huduma kwa wananchi na kuonesha mafanikio.

Msigwa alisema hadi mwisho wa mwezi Desemba, 2024 mapato yalifikia Sh. bilioni 37.6.

Kwa upande wa Maendeleo ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) alisema mpaka sasa shirika limefikisha ndege 16 na limeongeza safari za ndani ya nchi na kimataifa kwa kufikia 25.

Alisema serikali imeendelea kuwekeza kwenye miundombinu ya anga na kuboresha mifumo katika viwanja vya ndege vya Arusha, Kahama, Mpanda, na Songwe.

Msigwa alisema mwaka 2026 wanatarajia kukamilisha viwanja vya ndege vya Iringa, Mtwara, Songea, Kigoma, Msalato, Musoma, Shinyanga na Sumbawanga.

Katika mkutano huo pia, alizungumzia mwenendo wa ukusanyaji wa mapato nchini katika sekta ya mawasiliano, huduma ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na mkutano wa nishati wa wakuu wa nchi za Afrika.

Alitaja maandalizi ya uenyeji wa michuano ya CHAN 2025, AFCON 2027 na kupanda kwa ubora wa Ligi Kuu ya Tanzania.