Watumishi wa umma Dar kufanyia kazi nyumbani

By Christina Mwakangale , Nipashe Jumapili
Published at 03:34 PM Jan 26 2025
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dk. Moses Kusiluka
Picha: Mtandao
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dk. Moses Kusiluka

WAKATI Tanzania ikipata fursa na heshima ya kuwa nchi mwenyeji wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika Kuhusu Nishati (Africa Energy Summit), unaofanyika jijini Dar es Salaam, serikali imeagiza Januari 27 na 28, 2025, watumishi wa umma katika mkoa wa Dar es Salaam, wafanyie kazi nyumbani isipokuwa wale ambao mazingira yao hayaruhusu.

iTaarifa iliyotolewa na Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dk. Moses Kusiluka, imesema mkutano huo unaandaliwa baina ya serikali ya Tanzania, Benki ya Dunia (WB) na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB). 

Amesema Rais Dk. Samia Suluhu Hassan; marais wa nchi za Afrika 24; wawakilishi wa wakuu wa nchi na serikali za Afrika 21; wakuu wa taasisi za kimataifa sita wakiwamo marais wa benki hiyo; taasisi ya Rockefeller na washirika wa maendeleo watano, watashiriki mkutano huo. 

Kadhalika, amesema, jumla ya washiriki wengine 2,600 wa ndani na nje ya Tanzania, wamejisajili kwa ajili ya mkutano huo.

“Kufuatia ugeni huu mkubwa, baadhi ya barabara muhimu za Jiji la Dar es Salaam zitafungwa kama ilivyotangazwa na Jeshi la Polisi. 

Hivyo, ili kuepuka usumbufu ambao unaweza kusababishwa na kufungwa kwa barabara hizo, serikali inaelekeza kuwa tarehe 27 na 28 Januari, 2025 watumishi wa umma katika Mkoa wa Dar es Salaam wafanyie kazi nyumbani

“Isipokuwa wale ambao mazingira yao ya kazi yanawataka kuwapo katika vituo vya kazi kama vile watumishi wa vyombo vya ulinzi na usalama, sekta ya afya na sekta ya usafiri na usafirishaji. 

“Vilevile, Benki hazitafungwa na biashara katika Soko la Kariakoo zitaendelea kufanyika. Hoteli namigahawa nayo haitafungwa,” amesema Balozi Dk. Kusiluka.

Aidha, amesema kwamba waajiri katika sekta binafsi wanashauriwa kuruhusu watumishi wao katika mkoa wa Dar es Salaam, kufanyia kazi nyumbani au kuweka utaratibu ambao hautasababisha changamoto ya usafiri kutokana na kufungwa kwa barabara hizo.