DAWASA yafunga mita 150 za malipo ya kabla Dar na Pwani, zoezi linaendelea

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 06:13 PM Jun 02 2024
Mafundi wa DAWASA wakimfungia mteja mita ya malipo ya kabla (prepaid meters).
Picha: DAWASA
Mafundi wa DAWASA wakimfungia mteja mita ya malipo ya kabla (prepaid meters).

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) inaendelea na zoezi la ufungaji wa mita za malipo ya kabla (prepaid meters) kwenye maeneo mbalimbali hadi kufikia Mei 31,2024 jumla ya Mita 150 zimefungwa katika Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

Utekelezaji wa zoezi hili unafuatilia agizo la Rais la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan alitoa kwa Wizara ya Maji kuanza matumizi ya teknolojia ya mita za malipo ya kabla  kwa wateja ili kuboresha huduma na kupunguza changamoto za ankara kwa Wananchi.

Akiongea juu ya zoezi hilo, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA- DAWASA, Charles Kayuza amesema kuwa lengo la kufunga mita za malipo ya maji kabla inalenga kuboresha huduma, kusaidia kupunguza changamoto za kihuduma za mara kwa mara kutoka kwa wateja na hivyo kuleta ufanisi wa huduma zitolewazo na Mamlaka.

Mafundi wa DAWASA wakimfungia mteja mita ya malipo ya kabla (prepaid meters).


Ameongeza kuwa teknolojia hiyo inasaidia kukuza mapato ya Serikali moja kwa moja na kwa Mamlaka kwa kuwa mteja atakuwa analipia huduma ya maji kwa wakati sambamba na matumizi yake.

“Hadi sasa tumefunga mita za malipo ya kabla kwa wateja wakubwa na wadogo, katika Hoteli kubwa , Taasisi za Serikali mbalimbali, Mabalozi na nyumba za viongozi wa Serikali katika Wilaya za Kinondoni na Ilala na katika Mkoa wa Pwani tumefunga katika Halmashauri ya Chalinze” amesisitiza Kayuza.