Uboreshaji sekta ya afya wasogeza huduma za kibingwa kwa wananchi

By Elizabeth John , Nipashe Jumapili
Published at 09:13 AM Sep 22 2024
Prof. Mkenda azindua wa Kituo cha Afya Makoga
Picha:Mtandao
Prof. Mkenda azindua wa Kituo cha Afya Makoga

SERIKALI imesema uboreshaji miundombinu na kuwapo vifaa tiba katika sekta ya afya umesaidia kuokoa maisha ya wanaotaka huduma za kibingwa kama upandikizaji figo na upasuaji wa moyo.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda aliyasema hayo jana wakati akizindua Kituo cha Afya Makoga, wilayani Wanging'ombe, mkoani Njombe kilichojengwa kwa Sh. milioni 500.

Mkenda alisema kuwa awali  watu walikuwa wanafariki dunia kutokana na kushindwa kwenda kutibiwa nchi za nje kwa kukosa fedha.

Alisema uboreshaji huduma, ukiwamo ufungaji vifaa umerahisisha upatikanaji wake maeneo mbalimbali nchini.

"Uwekezaji uliofanyika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) unasababisha hivi sasa hospitalini hapo kupokea wagonjwa kutoka nchi za Zambia, Malawi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Burundi kupata huduma za afya na hii ni juhudi za makusudi za Rais Samia Suluhu Hassan," alisema Prof. Mkenda.

Alisema kwa sasa mtu akipata tatizo la figo utaalamu wa kubadilisha na kuwekewa nyingine unapatikana nchini.

"Leo ukienda pale Dodoma, Hospitali ya Benjamin Mkapa tuna uwezo. Serikali imewekeza, unachukua figo ya mtu mwingine unapandikiziwa wewe na unapona na unakuwa imara kabisa.

"Nimeona mtu amefanyiwa upasuaji huo wa kuwekewa figo, mtu wa kwanza kabisa bado yupo hai mpaka leo hii," alisema Prof. Mkenda.

Prof. Mkenda alisema ujenzi wa Kituo cha Afya Makoga na kuwapo vifaa tiba vya kisasa, kutawasaidia wananchi kuacha kutembea umbali mrefu hadi mjini Njombe kufuata huduma za afya, zikiwamo za upasuaji.

"Kuletwa kwa vifaa na huduma hii katika kituo chenu inamaanisha ukiwa mjamzito unataka kufanyiwa upasuaji au dharura yoyote, huna haja ya kukimbilia mjini Njombe, huduma zote zitapatikana hapahapa," alisema.

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Njombe, Julius Peter, alisema yote yanayofanyika ni utekelezaji ilani; waliahidi Watanzania watasogeza huduma karibu na makazi yao. 

Mbunge wa Wanging'ombe ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais - Tawala za Miko ana Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia afya, Festo Dugange, alisema miaka minne iliyopita wananchi hao walikuwa wanatibiwa katika zahanati ndogo licha ya kata hiyo kuwa na idadi kubwa ya watu.

Mkuu wa Wilaya ya Wanging'ombe, Zakaria Mwansasu, alisema serikali imepeleka vifaa vyenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni 185 pamoja na Sh. bilioni sita kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwamo ya shule na afya.

Mganga Mfawidhi wa kituo hicho cha afya, Joseph Chota, alisema kilipokea Sh. milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la mama na mtoto, maabara, upasuaji, jengo la kufulia, jengo la kuhifadhia maiti, nyumba ya mtumishi na kichomea taka. 

Baadhi ya wananchi wa Kata ya Makoga, akiwamo Ruth Chaula, walisema kabla ya ujenzi wa kituo hicho, wajawazito walikuwa wanapata adha kubwa pindi wanapohitaj huduma ya upasuaji.

"Dharura ilipotokea ya upasuaji, lazima uende mjini Njombe au Ikonda, Wilaya ya Makete ambako ni zaidi ya kilometa 30. Baadhi walipoteza maisha njiani,"" alisema Ruth.