MAKALA MAALUM: Dawa wanaokojoa kitandani hizi hapa

By Neema Emmanuel , Nipashe Jumapili
Published at 09:19 AM Sep 22 2024
Mtu aliyekojoa kitandani.
Picha:Mtandao
Mtu aliyekojoa kitandani.

KAMA una mtazamo hasi kiasi cha kumzodoa anayekojoa kitandani, basi unakosea! Wataalamu wa afya wamesema ni jambo la kawaida linalohitaji tiba ya kisaikolojia.

Wapo wanaokumbwa na changamoto hiyo kuanzia umri wa utoto hadi wanapoingia katika ndoa, na mara kadhaa imekuwa ikisambaratisha ndoa.

Daktari Steven Katwale kutoka Hospitali ya Rubya, wilayani Ukerewe, mkoani Mwanza, anasema watoto wengi wanakumbana na changamoto ya kukojoa kitandani, hasa wakati wa usiku.

Anasema hali hiyo ni ya kawaida japo imekuwa inawashtua wazazi, akisisitiza kuwa ni muhimu kuelewa sababu zake na namna ya kukabiliana nazo.

Mtaalamu huyo anataja baadhi ya sababu ambazo zinachangia mtoto kukojoa kitandani ni pamoja na mabadiliko ya kisaikolojia na matatizo ya kiafya.

"Sababu nyingine zinaweza kuwa msongo wa mawazo. Watoto katika umri huu mara nyingi wanahitaji muda zaidi ili kujifunza kudhibiti mkojo wao, na ni muhimu kwa wazazi kuwa na uvumilivu na kuelewa kwamba hii ni hatua ya kawaida katika ukuaji," anasema.

Dk. Katwale anasema sababu nyingine zinazowagusa wanaokojoa kitandani hadi utu uzima, ni pamoja na unywaji pombe kupitiliza.

"Nyingine ni kunywa maji kupitiliza muda mfupi kabla ya kulala, matumizi ya baadhi ya dawa za kuondoa chumvi mwilini (diuretic drugs) na uwezo mdogo kibofu kuhifadhi mkojo - mara nyingi husababishwa na uvimbe katika kibofu," anafafanua.

Daktari huyo pia anasema kuziba kwa kibofu, maambukizi katika kibofu, pia kuwapo matatizo ya kiafya, mfano kisukari, shinikizo la damu na tezi dume kunaweza kusababisha mtu kuwa kikojozi.

"Kuna vyanzo vingi sana, hata kupata mimba za utotoni, malezi ya mtoto - kutokumwamsha kukojoa akiwa na umri mdogo, homoni hazijakaa sawa na maambukizi kwenye njia ya haja ndogo (U.T.I) ni tatizo pia," anasema.

Mtaalamu huyo anasema katika kuwasaidia watoto wenye hali hizo, wazazi wanaweza kuchukua hatua kama vile kuanzisha ratiba ya kwenda msalani kabla ya kulala, kuhamasisha unywaji maji wakati wa mchana na kuepuka vinywaji vyenye vileo usiku.

Pia anasema ni lazima wazazi au walezi wajifunze namna ya kuzungumza kwa upole na mtoto wao kuhusu hali hiyo ili kumsaidia kujiamini na kujifunza kudhibiti.

Vilevile, Dk. Katwale anashauri wenye changamoto hiyo waepuke kumeza dawa zinazosababisha kukojoa wakati wa usiku, badala yake wanywe mchana au saa sita kabla ya kulala, wapate muda wa kulala mchana angalau saa sita hadi nane.

Vilevile daktari huyo anasema ni lazima watu wabadili mfumo wa maisha, akitolea mfano kupunguza unywaji pombe kupindukia na kuwahi hospitalini kwa ajili ya kupima pale wanapoona tatizo limezidi.

 WAZAZI WALONGA 

Baadhi ya wazazi wenye watoto walio na changamoto hiyo, wanaeleza namna walivyoendelea na tatizo hilo hadi umri mkubwa, huku waathirika wakijichukia.

Stella Julian, mzazi wa watoto wawili, mkazi wa Jiji la Mwanza, anasema mtoto wake wa kiume alikuwa na changamoto ya kukojoa kitandani kwa muda mrefu.

"Nilifanya kila jitihada ikiwamo kumpa maji yaliyolowekwa katika sufuria ya ugali, maji ya mchele na dawa mbalimbali ambazo watu walikuwa wakiniambia, lakini sikufanikiwa.

"Mawazo yaliongezeka pale alipoingia kidato cha kwanza, alitakiwa kwenda shule ya bweni, aisee usiombe...! 

"Nilinunua godoro nikalazimika kuvalisha mfuko wa plastiki. Nilipata mawazo sana, mwanangu pia alikuwa anajisikia vibaya sana. Alianza kujichukia lakini nilimpa moyo, sikumtenga! 

"Nilifanya sana maombi, nilimwombea mwanangu, hakika Mungu alisikia kilio changu, aliacha tu mwenyewe kukojoa kitandani," anasema.

Elizabeth Kennedy, mkazi wa jijini Mwanza, ni mzazi wa watoto wanne; wote wana changamoto ya kukojoa kitandani, hasa wanapokunywa vimiminika vingi nyakati za usiku - maji, juisi, soda au chai.

"Mtoto anaweza kupitisha siku tatu hadi nne, anakojoa kitandani. Sijawahi kutumia dawa yoyote. Kuna ambaye ninayemfamu alikuwa anakojoa mpaka darasa la saba, alipofaulu kwenda kidato kwanza, wazazi walishindwa kumpeleka shule ya bweni kwa kuhofia kuchekwa na wanafunzi wenzake," anasema.

Jothamu Radiance, pia mkazi wa Mwanza, anasema mke wake amekuwa akimwamsha mtoto wao mara mbili au tatu usiku na asipofanya hivyo, hukuta amejikojolea.

"Tumejaribu kutafuta tiba hatujafanikiwa, japokuwa tunapata maelezo mengi, wengine wanasema ni ugonjwa wa kurithi, mapepo machafu na mambo mengi, bado hatujapata tiba mpaka sasa, yuko kidato cha nne.

"Kuna watu walitushauri tumbebeshe godoro apitiswe mitaani, niliona huo ni udhalilishaji, nilimkataza mama yake asifanye hivyo, imani yangu ninaona ipo siku ataacha mwenyewe," anasema Radiance.

WASAIKOLOJIA TIBA

Msaikolojia Tiba kutoka Somedics Polyclinic Health Centre, Saldin Kimangale, anasema tatizo la kukojoa kitandani kitaalamu wanaliita ‘enuresis’.

"Ni tatizo la kibaiolojia na kisaikolojia, huwapata  watoto na watu wazima ambapo mtu anashindwa kudhibiti haja ndogo wakati amelala. 

"Linatambuliwa kwa watu wenye umri wa zaidi ya miaka sita. Husababisha aibu na wasiwasi. Sababu za kibaiolojia ni kama vile kuchoka au kuzeeka kwa mfumo wa mkojo na kurithi kwa njia za vinasaba.

"Kisaikolojia (vyanzo vya tatizo hili) ni pamoja na kuwapo msongo, wasiwasi... Ziko pia sababu za kimaumbile katika mfumo wa mkojo. Sababu za kimazingira ni pamoja na kunywa vimiminika nyakati za usiku," anasema.

Kimangale anasema athari zake ni pamoja na aibu, kujiona duni na hata kujitenga; kwa watu wazima aibu na hisia za kutokuwa na uwezo zinaweza kuwa kali zaidi.

"Kwa watoto, wazazi hukosa uvumilivu, hali inayoweza kuzidisha msongo wa mtoto na hasa wakiwachapa kama njia ya kukomesha tabia hiyo.

"Kwa watu wazima, kukojoa kitandani kunaathiri uhusiano wa kimapenzi au kijamii kutokana na aibu na kujihisi kutojiweza. Njia za kutibu ni pamoja na kufanya mazoezi ya kibofu, kuzuia kunywa vinywaji kabla ya kulala na matumizi ya 'alarms' (kengele za kuamsha)," anasema.

Mtaalamu huyo anaeleza zaidi kuwa zipo pia tiba kwa njia ya mazungumzo zinazofanywa na wanasaikolojia tiba ili kumsaidia mwenye tatizo hilo kuondokana nalo.