Tanzania yatamba kufanya vizuri kufuzu mashindano ya Kriketi

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 10:24 AM Sep 22 2024
Kocha wa timu ya taifa ya mchezo wa Kriketi, Muthumudalige Pushpakumara (kushoto) akiwa na nahodha wa timu hiyo, Abhik Patwa, wakizungumzia jana maandalizi ya timu hiyo kuelekea mashindano ya kufuzu fainali za Dunia za ICC yanayofanyika Dar es Salaam.
PICHA: MPIGA PICHA WETU
Kocha wa timu ya taifa ya mchezo wa Kriketi, Muthumudalige Pushpakumara (kushoto) akiwa na nahodha wa timu hiyo, Abhik Patwa, wakizungumzia jana maandalizi ya timu hiyo kuelekea mashindano ya kufuzu fainali za Dunia za ICC yanayofanyika Dar es Salaam.

KOCHA wa timu ya taifa ya Kriketi, Muthumudalige Pushpakumara, amesema wamejipanga kuhakikisha wanapata nafasi moja wapo kati ya mbili za kufuzu kwenda kusaka tiketi ya kucheza michuano ya dunia ya mchezo wa Kriketi.

Tanzania ni mwenyeji wa michuano ya wanaume ya kufuzu mashindano hayo ya dunia kutoka nchi za Afrika ambayo yameanza jana jijini Dar es Salaam na kushirikisha nchi sita za Cameroon, Ghana, Lesotho, Malawi, Mali na wenyeji.

Akizungumza na Nipashe jana, Pushpakumara alisema amekiandaa vizuri kikosi chake kwa ajili ya kushindana na kuhakikisha wanafanya vizuri kwenye mashindano hayo yanayofanyika jijini Dar es Salaam.

"Nimewandaa vizuri wachezaji wangu, nataka wawe frii kucheza lakini wacheze kwa malengo, tunawachezaji ambao wamecheza pamoja kwa muda mrefu na wamezoeana hii inanipa matumaini ya kufanya vizuri ukiangalia na namna tulivyojiandaa," alisema Pushpakumara.

alisema kikubwa anataka wachezaji wake wafurahie kucheza mashindano hayo na kuonyesha uwezowake kwa kuwa wana uwezo wa kufanya hivyo.

Nahodha wa timu ya hiyo, Abhik Patwa,alisema wachezaji wote wapo katika hali nzuri tayari kuanza mashindano hayo na wana hofu na timu yoyote.

"Hatuangalii viwango vya timu nyingine kwenye orodha ya timu bora, kikubwa ni maandalizi mazuri na wao wamejiandaa vizuri kuhakikisha wanafikia malengo yao," alisema Patwa.

Alisema kwa sasa mchezo wwa kriketi unazidi kukuwa Afrika na anaamini ni zamu ya Tanzania sasa kufanya vizuri na kufuzu kwa fainali hizo za dunia kama zilivyobaadhi ya nchi za jirani ambazo zimewahi kufuzu fainali hizo.

Mashindano hayo yanaandaliwa na kusimamiwa na Shirikisho la mchezo huo Duniani (ICC) na Tanzania kwa mara nyingine inakuwa mwenyeji baada ya hivi karibuni pia kuwa mwenyeji wa michuano ya vijana chini ya miaka 20 iliyofanyika jijini Dar es salaam kwenye viwanja vya Gymkhana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.