Saudi Arabia kuipa mbinu za kisasa Polisi kudhibiti uhalifu

By Romana Mallya , Nipashe Jumapili
Published at 09:38 AM Sep 22 2024
Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhandisi Hamad Masauni (kushoto), akizungumza na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Saudi Arabia, Mwanamfalme Abdul Aziz Bin Saudi Al- Saudi, nchini humo jana, kabla ya kutiliana saini hati ya makubaliano ya ushirikiano.
PICHA: WMNN
Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhandisi Hamad Masauni (kushoto), akizungumza na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Saudi Arabia, Mwanamfalme Abdul Aziz Bin Saudi Al- Saudi, nchini humo jana, kabla ya kutiliana saini hati ya makubaliano ya ushirikiano.

TANZANIA imetia saini hati ya makubaliano na Serikali ya Saudi Arabia inayogusa sekta mbili muhimu za usalama ya udhibiti wa uhalifu kwa kutumia utaalamu na teknolojia ya hali ya juu kwa Jeshi la Polisi. Makubaliano hayo pia yanagusa udhibiti wa majanga mbalimbali, yakiwamo ya moto, ajali za barabarani na maporomoko kupitia Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.

Hati hiyo ya makubaliano kwa upande wa Tanzania imetiwa saini na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni na kwa upande wa Saudi Arabia, imetiwa saini na Mwanamfalme Abdul Aziz Bin Saudi Al- Saudi, huku pande zote mbili zikionesha nia ya kubadilishana uzoefu na vifaa mbalimbali vinavyotumia teknolojia katika udhibiti wa matukio ya uhalifu.

"Ninachukua fursa hii kumshukuru Waziri wa Mambo ya Ndani wa Saudi Arabia kwa kunipa ushirikiano mkubwa katika ziara hii ambayo leo hii imepelekea kukamilisha utiaji saini kuhusu hati za makubaliano mbili.

"Tunakwenda kufungua milango ya kushirikiana kwa mapana zaidi katika maeneo hayo mawili. Itakwenda kufanya sasa nchi yetu kupitia Jeshi la Polisi kufaidika na fursa mbalimbali za ushirikiano, zikiwamo katika kujenga uwezo wa askari wetu katika maeneo mbalimbali na kubadilishana uzoefu na teknolojia ya jeshi letu," alisema.

Waziri Masauni alisema amefarijika kuona serikali ya Saudi Arabia imeweka msisitizo katika maeneo ambayo Tanzania imeweka nguvu kuimarisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kutoa huduma bora kwa wananchi," alisema Waziri Masauni.

Katika hafla hiyo, waziri huyo pia aligusia usalama wa kimtandao, akisisitiza kuwapo kipengele hicho katika hati ya makubaliano ili kudhibiti uhalifu wa mitandaoni ambao hivi sasa umeanza kushika kasi nchini.

"Tumeona wenzetu wameweza kuimarika sana katika matumizi ya teknolojia kudhibiti uhalifu wa kimtandao, hivyo ni imani yangu kwamba, kupitia ushirikiano ambao tumetia saini kwenye hati ya makubaliano, tunakwenda kufanikisha dhamira njema ya Rais Samia Suluhu Hassan kuimarisha Jeshi la Polisi katika eneo hilo.

"Kama mnakumbuka serikali imewekeza fedha nyingi kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 100 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya kisasa mbali na vifaa vingine ambavyo tayari vishaingia nchini mwaka huu ambavyo vinahitaji askari wetu wawe na uwezo na weledi wa kuvitumia, sambamba na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ambao tayari walishaanza kupokea magari," alisema Masauni.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Saudi Arabia, Mwanamfalme Saudi Al- Saudi, alisema wako tayari kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kudhibiti matukio ya uhalifu.

Waziri huyo pia alieleza namna Saudi Arabia ilivyodhibiti matukio mbalimbali ya uhalifu, akisema kuwa kila mwaka maelfu ya waumini wa dini ya Kiislamu na wageni kutoka mataifa mbalimbali hufika nchini humo.