Mikoa 17 kufanyiwa tathimini kaya masikini

By Faustine Feliciane , Nipashe Jumapili
Published at 11:31 AM Sep 22 2024
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemedi Suleiman Abdulla
Picha: Mpigapicha Wetu
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemedi Suleiman Abdulla

SERIKALI kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF) unajiandaa kufanya tahimini ya upimaji wa matokeo mpango huo katika mikoa 17.

Akizungumza mjini hapa jana wakati wa uzinduzi wa tathimini ya mwisho ya kupima matokeo ya kipindi cha pili ya  cha mpango wa kunusuru kaya masikini ya mwaka 2024, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemedi Suleiman Abdulla, amesema jumla ya mikoa 14 ya Tanzania Bara na mikoa mitatu ya Zanzibar yenye jumla ya shehia, vijiji na mitaa 434 itatembelewa kwa ajili ya tathmini hiyo.

Alisema kati ya hiyo, vijiji na mitaa 376 ni kutoka Tanzania Bara na shehia 58 ni kutoka Zanzibar.

"Madhumuni ya Tathmini hii ni kuweza kupima endapo Mpango huu unafikia malengo yaliyokusudiwa ya kuondoa umaskini kwa kaya zilizoainishwa kuishi katika umaskini uliokithiri," alisema Abdullah.

Aidha, alisema tathmini kama hizi hufanyika katika nchi mbalimbali zinazotekeleza mipango kama huo duniani kupitia taasisi za fedha na maendeleo za kimataifa.

"Katika nchi yetu, mpango huu unahusisha mikakati zaidi ya mmoja katika utekelezaji ili kuhakikisha kwamba walengwa wanafaidika na kutoka katika hali ya umasikini mapema zaidi. Hivyo basi, ni matarajio yetu kwamba, tathmini hii itaweza kutoa taswira halisi ya hali ilivyo na kuiwezesha Serikali kuona ni eneo lipi tunafanya vizuri zaidi na eneo lipi linahitaji kuongeza mkazo," alisema.

Kwa upande wake Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Salum Kassim Ali,  alisema matokeo ya tathimini ya mwisho ndio yatakuwa msingi wa kufanya maamuzi ya kuboresha zaidi hali ya upatikanaji wa huduma za kijamii na vile vile kuweka mikakati zaidi ya kupunguza umasikini hapa nchini.

"Tathimini hii ni muhimu ili kufikia lengo la mpango huu, kama ilivyoelezwa kwa awamu hii mikoa 17 tahusika na tayari mafunzo yametolewa kwa wale atakaofanya tathimini hiyo," alisema Ali.

4