Zitto atamba kutatua mgogoro wa ardhi Mbarali kwa dakika 10

By Halfani Chusi , Nipashe Jumapili
Published at 09:09 AM Sep 22 2024
KIONGOZI mstaafu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe
Picha:Mtandao
KIONGOZI mstaafu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe

KIONGOZI mstaafu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe ametaja mbinu za kutatua mgogoro wa ardhi unaoendelea Mbarali, mkoani Mbeya.

Amesema mgogoro unaweza kutatuliwa kwa kung'oa nguzo za mipaka (bikoni) zilizowekwa katika makazi ya wananchi zinazowaonesha wamo katika eneo la hifadhi.

Zitto amesema kuwa kama angekuwa ameshika dola, angetumia dakika 10 tu kutatua mgogoro huo.

Akizungumza na wananchi wa Mbarali jana ikiwa ni mwendelezo wa ziara za viongozi wakubwa wa chama hicho waliojigawa kikanda, Zitto alisema:

"Kinachoitwa mgogoro wa ardhi ulioko Mbarali ni kitu kidogo tu. Ni kuzitoa bikoni kutoka katika makazi ya wananchi na mashamba na kuzirudisha katika mpaka wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) na mgogoro utakuwa umekwisha, njia ni ndogo kabisa."

Zitto alisema njia nyingine ni serikali kuunda tume ya kijaji kwa ajili ya kupitia mipaka yote iliyo karibu na hifadhi na kuchora upya ramani ya matumizi ya ardhi.

Akisimulia uzoefu wake katika migogoro ya Mbarali alipochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma ambayo jukumu lake lilikuwa kuchunguza kuhusu ubinafsishaji mashamba, Zitto alisema kazi yao ya kwanza walianzia Mbarali Estate na Kapunga.   

"Moja ya mambo ambayo kila wakati ninayaeleza kwa wananchi, ni namna ambavyo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilikuwa kimechoka na bado kimechoka, ni namna walivyoendesha mchakato wa ubinafsishaji.

"Tulipokwenda katika Kijiji cha Kapunga kukutana na wananchi, walitueleza kuwa mwaka 1984, serikali ilikwenda kwao kuwaomba ardhi kwa ajili ya mradi wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) na kuipatia hekta 3,000 kwa ajili ya mradi wa umwagiliaji.

"Ilipofika mwaka 1999, serikali ikashindwa kuendesha mradi ule, ikaamua kuubinafsisha, wakatangaza tangazo la kubinafsisha. Katika tangazo lile wakatangaza kwamba wanabinafsisha hekta 3,500.

"Wao walipewa hekta 3,000, hekta 500 ndio zilikuwa sehemu ya Kijiji cha Kapunga. Nilikwenda bungeni nikauliza serikali kwamba mmeamua kuwauza wanakijiji na mashamba yao?  

"Bahati nzuri wakati ule Bunge lilikuwa Bunge kwelikweli. Nikapeleka ile ripoti bungeni, nikaeleza haya yote, wabunge wakabubujikwa machozi.

"Spika palepale (Samwel Sitta) Mwenyezi Mungu alaze roho yake mahali pema, akaagiza yafanyike marekebisho ya mkataba wa mauzo, wanakijiji warejeshewe ardhi yao. Ndivyo ambavyo tuliwaokoa wananchi wa Kapunga," alisema.

Zitto aliwasifu aliowaita "mashujaa wa Mbarali" kwa kufikisha malalamiko yao mahakamani kupingwa na kupokwa ardhi ambayo ni haki yao na kuahidi chama chake kitawapa tuzo.

Alisema hatua hiyo imesaidia mpaka leo wako katika eneo hilo kwa sababu serikali ilishindwa kuthibitisha kwamba maeneo yale ni maeneo ya hifadhi na wananchi walithibitisha ni maeneo yao.

"Hii ni nchi ya wakulima, wafugaji, wavuvi na wafanyabiashara. Tunaposema taifa la wote na maslahi ya wote, tunataka kila mtu aweze kuishi ndani ya nchi hii na kufaidi matunda ya nchi hii na siyo wachache waishi kama wanyama na kuuawa ovyo," alitamka Zitto kwa hisia kali.

Aliwaomba wananchi wa Mbarali kuchagua viongozi wanaotokana na chama cha ACT-Wazalendo, ili wawasaidie kutatua changamoto zao.

Msingi wa tatizo hilo umeelezwa kusababishwa na mchakato wa kuwahamisha wakulima na wafugaji katika kata tisa na jaribio la kutangazwa kufutwa vijiji vitano lililofanywa kuanzia mwaka 2022.

Ni mwendelezo wa utekelezaji Tangazo la Serikali (GN) Na. 28 la mwaka 2008, lilolenga kupanua eneo la Hifadhi ya Taifa Ruaha kwa kumega maeneo ya wananchi. 

Hata hivyo, tangazo hilo lilipingwa vikali na wananchi, Zitto akiwaomba kuendelea kushirikiana kulinda haki yao.