Simba: Tunaenda kufunga hesabu

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 08:46 AM Jan 09 2025
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids.
Picha:Mtandao
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids.

HAKUNA kulala, tayari kikosi cha Simba kimeondoka nchini leo alfajiri kuelekea Angola ili kuifuata, Bravos do Maquis, kwa ajili ya mechi ya raundi ya tano ya michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika itakayochezwa Jumapili mjini Luanda.

Katika mechi ya kwanza Simba yenye pointi tisa kibindoni kwa sasa, ikiwa mwenyeji, ilipata ushindi wa bao 1-0.

Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, alisema kikosi chake kinaenda Angola kwa kazi moja ya kumaliza 'kazi' ya kusaka pointi tatu muhimu ili kujihakikisha tiketi ya kucheza hatua inayofuata ya robo fainali.

Fadlu alisema kila mchezaji wa Simba yuko tayari kupambana ili kufikia malengo na anaamini msimu huu watapata mafanikio katika mashindano yote wanayoshiriki.

Kocha huyo pia amemtetea winga wake, Ellie Mpanzu, ambaye mechi iliyopita ugenini dhidi ya CS Sfaxien, alionyesha kiwango kizuri, alisema bado hajawa fiti na utimamu wa mwili wa kucheza dakika zote 90.

Alisema wanatarajia mengi kutoka kwa winga huyo ambaye kwa sasa hana utimamu wa mwili kamili, ndiyo maana amekuwa akimfanyia mabadiliko katika kila mechi aliyocheza.

"Ana wiki tatu tu tangu aanze kucheza mechi za ushindani, nimekuwa nikimpa dakika kadhaa za kucheza, mimi hapa nina furaha sana kwa kile anachokionyesha ndani ya uwanja, kiufundi amekuwa na athari chanya kwa wapinzani wetu kwa jicho la kitaalamu, huwezi kuliona hilo kama si mwalimu, mpira una vitu vingi zaidi ya 'asisti' na mabao uwanjani.

Ili upate hivyo kuna mchakato unafanyika ndani, amekuwa akifanya kazi kwa usahihi na kufuata maelekezo, tatizo hajawa na pumzi na utimamu wa mwili wa kumaliza dakika 90 akiwa na ubora ule ule," Fadlu alisema.

Aliongeza taratibu anaanza kuwa fiti, na kila mechi atakuwa akimwongezea muda  mpaka atakapoweza kumaliza dakika zote 90.

"Najua akishakuwa na uwezo wa kucheza dakika 90, atakuwa hatari zaidi ya hivi alivyo, uzuri sisi tunamfahamu, tunafahamu kipaji chake na uwezo wake mkubwa, hivyo haitupi wasiwasi tunajua atafanya makubwa tu," alisema kocha huyo.

Naye nahodha wa Simba, Mohamed Hussein 'Zimbwe Jr', alisema wanakwenda kupambana kusaka ushindi au sare, matokeo ambayo yataiwezesha timu yao kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo kutoka Kundi A.

"Mchezo utakuwa mgumu kwa sababu wenzetu wametoka kupoteza dhidi ya CS Constantine, nao jicho lao litakuwa katika mchezo huo, kama wachezaji tutakwenda kupambana kuhakikisha tunapata matokeo mazuri, matumaini yetu ni kupata matokeo mawili, ushindi au sare, tukifanikiwa hapo tutakuwa tumefuzu tayari.

Sisi kama wachezaji tuna ari kubwa na ile presha ya mwanzo imetuondoka, unajua mnavyozidi kucheza na kupata ushindi inawaondolea presha na kuwapa nguvu ya kujiamini," alisema beki huyo.

Wakati huo huo Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema katika dirisha dogo lililofunguliwa, klabu hiyo mpaka sasa imemsajili mchezaji mmoja tu ambaye ni Elie Mpanzu, huku akisema hawatasajili kwa fasheni.

Ahmed alisema hawatasajili mchezaji wa kujaza idadi au mchezaji wa kukaa benchi, bali wanahitaji nyota ambaye moja kwa moja anaingia katika kikosi cha kwanza.

"Hakuna mapungufu makubwa sana katika kikosi chetu, hao wengine wacha wakusanye wachezaji, sisi kama tutafanya usajili basi utakuwa wa mchezaji mmoja au wawili, na wawe wa viwango vya juu, hata wakija basi moja kwa moja wanaingia kwenye kikosi cha kwanza," alisema Ahmed.

Kimahesabu Simba yenye pointi tisa, inahitaji sare tu ili kusonga mbele, pointi ambazo hazitafikiwa na Bravo do Maquis au CS Sfaxien.