Camara bado chache kumkamata Matampi

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:17 AM Feb 07 2025
golikipa wa Wekundu wa Msimbazi, Moussa Camara
Picha: Mtandao
golikipa wa Wekundu wa Msimbazi, Moussa Camara

KABLA ya mchezo wa jana, kati ya Simba dhidi ya Fountain Gate, golikipa wa Wekundu wa Msimbazi, Moussa Camara, alikuwa amebakisha mechi mbili za kusimama langoni bila kuruhu bao ili kumfikia kipa bora wa msimu uliopita, Ley Matampi, aliyekuwa akiichezea Coastal Union.

Matamp alibeba tuzo ya Kipa Bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2023/2024, akiwa na 'clean sheets' 15.

Mechi ya Jumapili iliyopita dhidi ya Tabora United ambayo Simba ilishinda mabao 3-0, iliyochezwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani, Tabora, aliyotoka bila kuruhusu wavu wake kuguswa, ilimfanya kufikisha 'clean sheets' ya 13.

Nafasi ya pili katika makipa ambao wamelinda vyema vyavu zao inashikiliwa na Djigui Diarra wa Yanga ambaye juzi aliruhusu bao la jioni walipocheza dhidi ya KenGold FC kutoka Mbeya.

Camara, raia wa Guinea, aliyesajiliwa mwanzoni mwa msimu akitokea, Horoya FC, amekuwa kwenye kiwango bora kabisa ikiwa ni mara kwanza akicheza Ligi Kuu ya Tanzania, akiwa amekaa langoni mara zote 16 ambazo timu yake imeshuka dimbani.

Idadi kubwa ya michezo iliyosalia ndiyo inayotajwa huenda ataendelea kung'ara zaidi kwenye msimu huu.

Kwa mujibu wa dawati la takwimu la michezo Nipashe, Camara ameruhusu mabao katika michezo mitatu tu kati ya 16 ambayo amekaa langoni.

Alifanya hivyo Oktoba 4, mwaka jana, aliporuhusu mabao mawili, Simba ikitoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Coastal, Union, mechi ikipigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam na Oktoba 19, mwaka jana, timu yake ikipata kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Yanga.

Mechi nyingine ilikuwa Desemba 21, mwaka jana, aliporuhusu mabao mawili dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, mkoani Kagera, Simba ikishinda magoli 5-2.

Ubora wa Matampi, uliifanya Coastal Union kumaliza katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara na kupata tiketi ya kushiriki katika michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Patrick Munthary, Mtanzania anayeichezea Mashujaa FC, pia amesimama langoni katika mechi nane bila kuruhusu bao akifuatiwa na Metacha Mnara wa Singida Black Stars mwenye 'clean sheets' saba huku Mohamed Mustafa wa Azam FC, raia wa Sudan, akiwa nazo sita.