KOCHA Mkuu mpya wa Yanga, Miloud Hamdi, ameweka wazi falsafa yake kuwa anapenda soka la kushambulia zaidi na kupatikana mabao mengi iwezekanavyo, akiwa tayari ameshawaelekeza wachezaji wake kufanya hivyo kwenye mchezo wa leo dhidi ya JKT Tanzania, utakaopigwa Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam.
Yanga itakuwa ugenini leo ikicheza mchezo wa 18 wa Ligi Kuu, ikiwa kileleni na pointi zake 45, ikijua kabisa kuwa nyuma yake kuna watani zao wa jadi, Simba wenye pointi 44, ambao kesho watashuka Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam kwenye mchezo dhidi ya Prisons.
Miloud, ambaye atakuwa anakiongoza kikosi hicho kwa mara ya kwanza akiwa ametoka Klabu ya Singida Black Stars kuchukua nafasi ya Sead Ramovic, aliyetimkia CR Belouizdad ya Algeria, amesema anapenda soka la kushambulia zaidi na mpira ni kufunga mabao na kuzuia wapinzani wanapokuja, huku akiwa hapendi kupoteza.
"Kutokana na ukubwa wa Yanga inapaswa kushinda makombe, kazi kubwa inafanywa na washambuliaji kufunga kila mechi na mabeki kuweza kulinda ushindi huo.
"Tutafanya kila linalowezekana kujaribu kushinda michezo yetu, nilikuwa jukwaani tulipocheza na KenGold, kuna wachezaji wazuri, wanapambana, tumeshinda idadi kubwa ya mabao, lakini kuna mapungufu nimeyaona kiufundi na mapema nimefanyia kazi kwa sababu nilikuwa na siku chache za maandalizi ya mchezo huu dhidi ya JKT Tanzania," alisema.
Akiizungumzia mechi ya leo, alisema anaifahamu JKT Tanzania kuwa ni timu nzuri na ngumu, lakini pamoja na kwamba hana muda mrefu akiwa na kikosi cha Yanga, kuna vitu vichache alivyoviongeza ambavyo vitaiwezesha timu yake kuwa bora zaidi na huenda kuvuna mabao mengi kwenye mchezo wa leo.
"Naifahamu timu hii, ni nzuri, tutajitahidi kucheza soka letu, tunajua tutakuwa na mechi ngumu, lakini sisi ni Yanga na siku zote timu zinazocheza na sisi zinataka kutoa kila kitu ilichonacho.
"Mimi sitokuwa na kazi kubwa sana, najua ni mgeni, lakini Yanga ni timu kubwa, ina wachezaji wazuri wenye ubora, kwa hiyo nimeongeza vitu vichache tu vya kuanzia kwa ajili ya mchezo huu, wameshinda mechi sita mfululizo, huu utakuwa mwendelezo tu," alisema.
Kocha Mkuu wa JKT Tanzania, Ahmad Ally, alisema katika mchezo wa leo kitu wanachohitaji ni kuwa bora tu uwanjani, pia kutumia udhaifu wa wapinzani wao.
"Tunachokihitaji ni kuwa bora tu uwanjani, tunajua tunacheza na timu ambayo ni nzuri yenye uwezo wa kucheza ikiwa na mpira na isipokuwa nao, pamoja na ubora huo lakini wana udhaifu wao pia, sisi tunatakiwa kuwa makini kutumia yale madhaifu yao. Tunajua kabisa kuwa tunakwenda kucheza na wachezaji wenye ubora mkubwa zaidi kuliko sisi, hivyo tunatakiwa kuwa makini," alisema.
JKT Tanzania ipo nafasi ya tisa ya msimamo wa Ligi Kuu, ikiwa imejikusanyia pointi 19 kwa michezo 17 iliyocheza.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED