DUNIA inaendelea na Siku 16 za Harakati za Kupinga Ukatili wa Kijinsia kwa namna mbalimbali, watetezi wa haki za wanawake, wasichana na watoto wanasema ukatili na unyanyasaji umezidi.
Akizindua kampeni hizo nchini Sudan wiki iliyopita, Tom Fletcher, Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Dharura (OCHA), ana ujumbe kwa wanaume wanaowakatili kingono wanawake na watoto akisema:
“Nawaambia iwapo unadhani unafanya hivyo kwa sababu una nguvu, unakosea. Unafanya hivyo kwa sababu wewe ni dhaifu.” Wanaume wanaofanya hayo ndiyo ujumbe wenu huo.
Kazi ya kupamba na ukatili, hapa nchini inaeleza kuwa upo mijini na vijijini ndani ya familia na ndugu wa karibu ndiko kwenye unyanyasaji zaidi.
Jamii inaamini kuwa nyumbani ni mahali salama kwa wanawake, wasichana na watoto lakini sivyo. Kuna shida. Ni kutokana na kuongezeka kwa ukatili kama unajisi wa watoto unaofanywa na wazazi, walezi na ndugu wa karibu kama baba mdogo na wajomba.
Udhalilishaji watoto wa kike na kiume, kukatili wanawake na wasichana kuwaua, baadhi wakikatishwa maisha na wapenzi au wenza ni matukio ya kila wakati.
Mkoani Pwani, Asasi ya ‘Initiative for Domestic Workers’, inafanya uhamasishaji wa ulinzi wa mtoto dhidi ya ukatili katika kata za Yombo na Fukayosi wilayani Bagamoyo.
Wakiwatembelea wanavijiji wa Matimbwa na Fukayosi kuhimiza ulinzi wa mtoto, anasema Ofisa Miradi Farida Jackson, akiongeza kuwa vitendo vya ukatili na jinai vinazidi.
Anaiambia Nipashe kuwa zama hizi watoto wa kiume wapo katika hatari ya kulawitiwa, wasichana nao wakinajisiwa na kuingiliwa kinyume cha maumbile nyumbani na kwenye jamii.
Anasema wamefanya mikutano ya mafunzo na wazazi na walezi wa Kata za Fukayosi na Yombo, wakiwahimiza kuwakagua watoto miili yao, kuangalia mabadiliko ya tabia na akili ili kugundua kama wanafanyiwa ukatili wa kijinsia mapema na kuwatafutia tiba.
“Pamoja na hayo tunawakumbusha anapokuja mgeni awe mjomba, baba mdogo au kaka asilale na watoto wao. Anaweza kuwadhalilisha,” anasema Farida.
Anaongeza kuwa wapo ndugu wa karibu na wazazi ambao wametuhumiwa kunajisi watoto wa jamaa zao kwa kuwalawiti na kuwabaka na taasisi yao imepokea malalamiko ya mgeni anayeishi mjini anayefika Bagamoyo na kurubuni watoto kuwafanyia unyanyasaji.
Farida Ofisa Miradi anasema kazi hizo zinafanyika kwenye mradi wa kuwajengea uwezo wanawake, wasichana, watoto na jamii kuhusu kazi za staha kwa wafanyakazi za ndani ulioanza mwaka huu ukitarajiwa kukamilika Januari mwakani, ukidhaminiwa na Tanzania na Shirika linalofadhili miradi ya maendeleo ya wanawake (WFT-T).
Anasema kwenye mikutano wanawasisitiza wanavijiji waepuke mazoea ya kuruhusu watoto kwenda likizo kwa jamaa zao mikoani kwani mzazi au mlezi hajui mtoto wake anakutana na nani au nini na huenda anafanyiwa unyanyasaji kingono, kufunzwa uhalifu kama kutumia dawa za kulevya au pombe.
“Tumezungumzia madhara ya kuruhusu watoto kuishi na baba au bibi tukiwaambia leeni watoto wenu wenyewe, maisha ya sasa si kama ya zamani. Watu wanaweza kutumia mwanya wa uzee au hali ya kushindwa kufuatilia maendeleo ya watoto na kuwadhuru.”
Anasema uhamasishaji unawataka wazazi au walezi waonyeshe msimamo katika malezi kwa kuwa wakali na kusimamia majukumu ya elimu, malezi na gharama wasiwaachie watu wengine.
KAZI ZA NDANI MIJINI
Akizungumzia mradi wa kuwajengea uwezo wanawake, wasichana, watoto na jamii kuhusu kazi za staha kwa wafanyakazi za ndani, Farida anasema wakazi wa vijiji vya Fukayosi na Yombo, ni miongoni mwa maeneo ambayo watoto wanakwenda kufanya kazi mijini baada ya kumaliza shule.
Anasema hilo nalo linazungumziwa na kuwambusha wazazi na walezi kuwa wengi hawatambui watoto wao wanafanya kazi kwa nani na katika mazingira gani.
“Zama hizi kuna kampuni zinatafutia mabinti kazi za ndani na kuwawapeleka kwa wanaowahitaji. Wazazi wanafuatilia? Wanawafahamu waajiri au aliyewasafirisha kutoka kijijini? ”
Wanawahimiza wazazi kuwafahamu wanaowaajiri watoto wao tena kuthibitisha majina na vitambulisho vyao kwa kuingia mikataba na waajiri hao kwa ushahidi mahususi kwa viongozi wa serikali za vijiji na mitaa mahali walipo na vijijini walipotoka.
Anasema tumehimiza: “Tusione usumbufu, ni lazima kuwalinda watoto wetu, hata kama mzazi au mlezi hawezi kwenda, wanandugu wasaidiane, walimu wana maarifa mbalimbali wanaweza kutumika kutoa msaada na dawati la jinsia la kata na polisi kata na maofisa maendeleo ya jamii.”
KUJALI
Farida anasema wazazi vijijini wanawageuza watoto wao kuwa vitega uchumi bila kujali madhira wanayopitia kwenye kazi wanazofanya mijini, mathalani, hawaulizi kuhusu mshahara, kazi wanazozifanya, na wengine hawana mawasiliano.
“Tuanze sasa kujua haya mambo kwa sababu nyakati zimebadilika, tusing’ang’anie kutumiwa mishahara kila mwezi, wala kutaka simu, mavazi na zawadi ambazo zinawaumiza mabinti wetu,” anasema Ofisa Miradi Farida.
Anasema wanawahimiza wajali malalamiko ya watoto wao, mfano kufanyakazi bila mikataba, kunyanyaswa kingono, kutumikishwa kinyume na sheria, ujira mdogo au kukosa mshahara, vipigo na matusi.
Glady Kimathi, mwanaharakati wa kujitolea anayefanyakazi na Initiative for Domestic Workers, akizungumzia harakati hizo, anasema tafiti zimebaini kuwa baadhi ya wazazi wanawahamasisha watoto kufeli mitihani ya darasa la saba ili waende kufanya kazi za ndani mijini.
Anasema wametembelea shule za Fukayosi na Matimbwa kuwahimiza kufanya vizuri kwenye masomo yao ili kutimiza ndoto zao, wasome zaidi.
Anasema wanafunzi wamehimizwa kuripoti matendo ya unyanyasaji yanayofanywa nyumbani kwa walimu na wanapofanyiwa ukatili shuleni waripoti nyumbani.
Aidha, atika kata hizo, wanavijiji wametakiwa kuacha kufichiana siri za kihalifu hasa za udhalilishaji watoto, wanawake.
Anatoa mfano kuwa yapo mazoea kuwa mwanafamilia akinajisi mtoto, akishtakiwa itavunja undugu hivyo kuleta migogoro kwenye familia na kutengana.
“Tumewaambia wananchi wakumbuke, anayedhalilishwa na kuharibiwa maisha ni mtoto wao. Ikiwa baba mdogo au mjomba anafanya hayo hakuthamini undugu. Kwa hiyo kuendeleza kusalimiana au kuvunja undugu, hakutamsaidia, sheria lazima ichukue mkondo wake, waripoti visa na mikasa hiyo kwenye vyombo vya sheria,” anasema Glady.
Anaongeza kuwa shuleni pia wamewahamasisha wanafunzi kukataa kuingizwa kwenye mazingira hatarishi ambayo yatasababisha kunajisiwa au kubakwa, na wakifanyiwa vitendo hivyo maeneo ya shule waripoti nyumbani na ikiwa nyumbani waripoti shuleni.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED