Kinondoni yatarajia kukusanya bilioni 82.3 za kodi Desemba 2024

By Pilly Kigome , Nipashe
Published at 08:27 PM Dec 19 2024
Mkuu wa Wilaya  Kinondoni, Saad Mtambule.
Picha:Pilly Kigome
Mkuu wa Wilaya Kinondoni, Saad Mtambule.

MANISPAA ya Kinondoni inatarajia kukusanya mapato ya Sh. Bil.82.3 kwa makusanyo ya kodi kwa mwezi Disemba katikankipindi cha robo ya nne ya mwaka katika mikoa ya kikodi Kinondoni na Tegeta.


Mkuu wa Wilaya  Kinondoni, Saad Mtambule ameyasema hayo Desemba 18 mkoani Kinondoni alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari.

Wakati huo huo ametaja maeneo korofi vinara yanayoongoza kwa kupitisha bidhaa za magendo katika Manispaa hiyo inayofanya kupungua kwa mapato ni pamoja na Mbweni, Kunduchi na Kawe.

Amesema kuwa bidhaa zinazoongoza kwa kupitisha magendo ni pamoja na mafuta, sukari, nguo, vifaa vya majumbani, baiskeli na TV.

Mtambule amesema katika msako uliofanywa na Manispaa hiyo tayari wafanyabiashara watano wameshakamatwa kutokana na muenendo huo ambao unarudisha nyuma maendeleo ya nchi kwa kukwepa ulipaji kodi na tayari hatua stahiki zinachukukiwa kwa waharifu hao.

Aidha aliwaonya wafanyabiashara wote wanaojihusisha na biashara za magendo kwa kukwepa kulipa kodi na kuwataka wafanyabiashara wote ambao bado wanadaiwa kodi katika kipindi hiki cha robo ya nne walipe pasipo usumbufu.

Ikiwemo na kuwataka wafanyabiashara na wananchi wote watumie mashine za kieletroniki za EFD katika utoaji risiti wakati wa manunuzi ili kukwepa upotevu wa mapato.

Meneja  TRA Mkoa wa Kinondoni, Aziz Soka alisema mkoa huo haujawahi kushindwa katika ukusanyaji kodi kwakuwa wanafanya juhudi kubwa kupambana na wakwepaji kodi kwani bila kodi hakuna elimu, afya wala huduma muhimu zinazotegemea makusanyo ya kodi.
Kwa upande wake Meneja TRA Mkoa wa Tegeta  aliwataka wafanyabiashara walipe kodi kabla ya Disemba 31,2024 kwakuwa tarehe hiyo ndio mwisho wa makusanyo ya kodi kwa kipindi hiki cha robo ya ya mwaka.