WAFUGAJI takribani 20 katika kijiji cha Maguruwe, kata ya Msimbu, wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani, wamepatiwa mafunzo ya ufugaji kuku wenye tija, ili kukabiliana mabadiliko ya tabianchi, magonjwa na kujikwamua kiuchumi.
Ofisa Kilimo katika kijiji hicho, Safina Kisaka, akizungumza, jijini Dar es Salaam, alisema mafunzo yatawaongezea uelewa wafugaji hao, kwa kuwa miongoni mwa changamoto za ufugaji eneo hilo ni ukosefu wa mitaji na kushindwa kumudu bei za dawa hasa chanjo.
Pia alisema kwamba changamoto zingine ni wakazi wa eneo hilo kuzingirwa na Hifadhi ya Misitu ya Kazimzumbwi, jambo linalosababisha mifugo kuvamiwa na wanyama wakali kama vile nyoka, kutokana na ujenzi wa mabanda ya kufugia kuwa duni.
“Wafugaji wengi kwenye kijiji hiki wako mmoja mmoja, kwa hiyo mradi huu unapokwenda kuanza utarahisisha kuwa na kikundi cha wafugaji na kuwafikia kwa urahisi, ili kuwapa elimu. Huwa ninawatembelea, lakini utakuta mfugaji mmoja hadi mwingine kuna umbali mrefu kumfikia.
“Suala lingine ni tupo jirani na hifadhi, inachangia kuwapo wadudu wakali kama nyoka na mifugo kuliwa. Sasa kwa elimu hii na namna ambavyo watawezeshwa wafugaji itawasaidia kuwa na banda bora la kuku ambalo si rahisi kuvamiwa na wadudu au wanyama kutoka hifadhini,” alisema Safina.
Aliongeza kwamba ufugaji kwenye eneo hilo pia unaathiriwa na mabadiliko ya tabianchi, na kusbabisha chakula cha kuku kuuzwa ghali na pia kijiji hicho kuwa kwenye mwinuko husababisha mvua zinaponyesha maji kushindwa kutumika kwenye mahitaji ya kilimo.
“Kuna wakati hata wataalamu wa kilimo tunashindwa tuwape ushauri ipi watu wetu, ardhi yetu ya mlimani na sehemu chache zina rutuba, hali ya hewa ni joto kali. Mabadiliko ya tabianchi yanasababisha kushindwa kuwaambia wapande mazao ya muda mrefu au mfupi.
“Mvua kuna wakati hunyesha kidogo, hivyo tutawambia angalau wapande mihogo, ili wasikose kabisa chakula, maana wakipanda kama mahindi mvua zisiporudi kwa wakati yatakauka, tofauti na mihogo hustahimili ukame,” alisema mtaalamu huyo.
Daktari wa Mifugo kutoka Kitengo cha Kutumia Mbegu Bora Interchick, Dk. David Comalla, alisema kwamba kufuga kuku kwa faida pia hutegemeana na mbegu pamoja na mazingira.
“Kuzingatia ujengaji bora wa mabanda na kuzuia magonjwa na jinsi ya kupambana na mgonjwa huongeza tija na ni muhimu pia kufuata njia sahihi ya kutoa chanjo na kufuata utaratibu wa tarehe za chanjo na muda unaotakiwa kutoa chanjo kwa kuku.
“Wafugaji wanapaswa kujua mbinu ya ufugaji kisasa na kuzingatia eneo la kufugia kuku kulingana na ukubwa wa banda linalopitisha hewa na lisiloingiliwa na wadudu wakali kama vile nyoka,” alisema Dk. Comalla.
Mshauri wa asasi hiyo, Dk. Elikana Kalumanga, (technical advisor Volunteer) wa Asasi ya Tanzania Landscapes Restoration Organization (TaLRO), alisema mradi huo unafadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kupitia miradi midogo chini ya mfuko wa Mazingira (GEF-Small Grants Programme);
Alisema malengo ya mradi huo ni kuwafikia wakazi wanaoishi jirani na hifadhi, ili wawe na shughuli mbadala wa uchumi, kupunguza utegemezi na athari kwa rasilimali za asili kama vile msitu uliopo eneo hilo wa hifadhi ya Kazimzumbwi.
“Kunapokuwa na watu wa eneo kama hilo wanaotegemea chanzo kimoja kama kilimo na ikitokea wanakwama, kutokana na mabadiliko ya tabianchi kama mafuriko, kitakachofuata ni kutegemea msitu. Ila asasi hii inakuja na shughuli mbadala wa kiuchumi na rafiki kwa mazingira bila kuwa na ujuzi mkubwa, mtaji mkubwa na shirikishi kwa makundi yote kwa vijana, wanawake na wazee, ukabuniwa mradi wa kuku.
“TaLRO pia wameungana na Interchick, ili kuwafikia wananchi hawa hata maradi ukiisha watakuwa na soko la kuuza kuku wao, baada ya kupata elimu ya ufugaji wenye tija,” alisema Dk. Elikana.
Happiness Temu, mmoja wa wafugaji hao, alisema anatarajia baada ya kupata mafunzo hayo pamoja na kuwezeshwa mtaji kutoka taasisi za kifedha, atafuga kwa tija, ili kuongeza kipato kwenye familia.
Pastory Msuka, mfugaji pia alisema kwamba bei ya dawa za chanjo kuuzwa kwa bei kubwa, kunawasababishia kununua dawa moja kwa kuchangishana fedha.
“Dawa moja ya chanjo ya ndui ya kuku inauzwa Sh. 12,000 utakuta hiyo fedha mimi peke yangu sina au nina kuku wachache, hitaji la dawa hiyo ni kuwa na kuku 100 nami sina, nitawatafuta wenzangu wafugaji wa kuku, ili kutimiza namba hiyo, tuchange fedha kununua dawa moja.
“Sasa ninachojiuliza hiyo dawa tunapogawana tunagawana kwa vipimo sahihi? Au ndio sababu magonjwa kwa kuku hayaishi na baadhi hufa. Ila mafunzo haya yametufungua macho,” alisema Pastory.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED