WAANDISHI wa habari wametakiwa kufanya uwiano wa maisha yao binafsi na kazi ili kuboresha ustawi wao wa kimwili na kiakili kuepuka magonjwa yasiyoambukiza ukiwamo wa afya ya akili.
Akitoa mafunzo kwa wafanyakazi wa Kampuni ya The Guardian Limited jana, Mwanasaikolojia kutoka Tanzania Health and Medical Education Foundation (TAHMEF), Paul Ndemanisho, alisisitiza umuhimu wa wafanyakazi kutathmini vipaumbele vyao na kujitahidi kudumisha uwiano mzuri kati ya kazi na maisha binafsi.
Alisema ni muhimu kupanga ratiba inayowapa nafasi ya kupumzika, kuwekeza muda kwenye familia, na kujitathmini ili kupunguza athari za uchovu wa mwili na msongo wa mawazo unaosababishwa na changamoto za kazi.
TAHMEF inatoa mafunzo na huduma ya kisaikolojia kupitia wataalamu wake wenye leseni ya kutoa ushauri kwa mtu mmoja mmoja na vikundi kupitia video, kupiga simu na mafunzo ya ana kwa ana.
Ndemanisho alisema, ingawa uandishi wa habari ni kazi yenye mchango mkubwa kwa jamii, ni muhimu wakatoa kipaumbele kwa afya zao, kwa kuwa ustawi wao binafsi ni muhimu kwa kuboresha utendaji kazi wao.
“Waandishi wa habari wanahitaji kutafuta muda wa kupumzika na kuwekeza katika familia zao, hii sio tu itaboresha ustawi wa maisha yake binafsi, bali pia itasaidia kuboresha utendaji kazi wake, kuwa na uwiano na maisha binafsi ili kuondoa athari za uchovu na msongo wa mawazo,” alisema Ndemarisho.
Mhariri Mtendaji wa gazeti The Guardian, Wallace Maugo, alisisitiza kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa waandishi wa habari, kwa kuwa yanawasaidia kuelewa ustawi mzuri wa kimwili na kiakili.
Aliwashauri viongozi wa vyombo vya habari kujengewa uwezo ili waweze kusaidia wafanyakazi wao kutengeneza ratiba inayowezesha kufanya kazi kwa ufanisi huku pia wakidumisha uwiano na maisha yao binafsi.
“Majukumu ya waandishi ni makubwa na mara nyingi yanawafanya kushindwa kujumuika na jamii zao, lakini hii si kwa sababu hawataki, ni muhimu kwa viongozi kujua jinsi ya kuwasaidia waandishi kuwa na muda wa kupumzika na kushirikiana na familia zao,” alisema Maugo.
Mwanasaikolojia Catherine Kisarika, alisema changamoto za kifedha zimekuwa chanzo kikubwa cha matatizo ya afya ya akili kwa waandishi wa habari.
Alihimiza matumizi ya teknolojia ya huduma za afya ya akili zinazoweza kuwasaidia waandishi na watu wengine kuboresha ustawi wao wa kiakili, hasa kwa wale wanaokutana na changamoto za kifedha na za kijamii.
“Programu tumizi (Application) zinazotoa huduma za afya ya akili zinajitahidi kufikia watu wengi, na zinasaidia kutoa majibu ya haraka kuhusu matatizo ya kiakili.
Alisema ni muhimu kwa waandishi wa habari, kwa kuwa wengi wao wanakutana na msongo wa mawazo unaotokana na kazi zao,” alisema Kisarika.
Mafunzo ya afya ya akili yanatoa fursa ya kujifunza namna ya kudumisha ustawi mzuri katika mazingira ya kazi yanayowabana.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED