RIPOTI MAALUMU DAWA ZA KULEVYA: Mbinu mpya za wauzaji zashtua mamlaka

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 10:29 AM Dec 10 2024
Mtumiaji wa dawa za kulevya.
Picha:Mtandao
Mtumiaji wa dawa za kulevya.

WAUZAJI dawa za kulevya wamebadili mbinu, wakiibuka na njia mpya, zikiwamo za medani za kivita, ili kukwepa kukamatwa, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imethibitisha.

Kwa mujibu wa mamlaka hiyo, hivi sasa wauzaji wa dawa hizo pamoja na mbinu zingine, wanawasiliana kwa mitandao ya siri (dark webs), wanasafirisha dawa kwa ndege nyuki (drones), vipuri vya magari, nguo za asili, vinyago, simu na vikapu.

Vilevile, imebainika wauzaji wa dawa hizo wana boti maalumu za usafirishaji wa dawa ambazo zina mwendo mkali kulinganishwa na boti za mamlaka za udhibiti, hivyo kutowakamata kirahisi.

Kamishna wa DCEA, Peter Patric amemwambia mwandishi wa habari hii kuwa wamebaini mbinu hizo baada ya mamlaka hiyo na Jeshi la Polisi kuweka mikakati ya kukomesha matumizi na usambazaji wa dawa hizo nchini.

Anasema kuwa mbali na kubadili mbinu za usafirishaji, wauzaji dawa za kulevya sasa wanaingiza sokoni aina mpya za dawa ambazo haziko kwenye majedwali ya wadhibiti. Anabainisha kuwa kuna dawa mpya 1,184.

"Kwa msingi huo, mataifa mbalimbali, ikiwamo Tanzania, yameanza kuziongezea uwezo maabara za sayansi jinai pamoja na maofisa wanaohusika na vitengo hivyo ili wawe na uelewa wa utambuzi wa aina hizo mpya za dawa ambazo zinaingizwa sokoni kinyume cha sheria.

"Hivi sasa dawa za kulevya si tu zinasafirishwa kwa ndege, boti na meli kama zamani, bali pia zinauzwa katika mataifa mbalimbali kupitia dark webs (mitandao ya kijicho/siri).

"Kupitia mitandao hiyo, mtu anaweza kusema 'mimi ninataka kete tano za Heroin', kisha akatuma fedha kwa njia ya mtandao na dawa hizo zikasafirishwa kama bidhaa nyingine kumfikia aliyeagiza. Kwa hiyo, mtu anapokea mzigo, ukiangalia unadhani ni simu, kumbe ni dawa za kulevya," anafafanua. 

Kamishna Patric anasema wamekamata kiwango kikubwa cha dawa zinazotoka nchini kwenda nje kwa kutumia vifaa kama vile vipuri vya magari, vyuma, vikapu na nguo za kiasili.  

Anaeleza kuwa katika uwanja wao huo, upelelezi wa aina hiyo ya uhalifu ni mgumu na unahitaji vyanzo vingi na ushirikiano mkubwa na mataifa mengine kujua dawa husika imetoka wapi ili kuhakikisha unaidhibiti. 

Kuhusu aina mpya za dawa za kulevya, Kamishna Patric anabainisha kuwa kati ya dawa hizo, zimo zinazoitwa "New Psychotropic Substances - NPS", akiwa na ufafanuzi kwamba awali zilikuwa zinalimwa shambani mithili ya bangi, lakini hivi sasa zinatengenezwa viwandani na zinakuwa na ladha sawa na zilizokuwa zinalimwa shambani. 

"Ripoti ya Hali ya Dawa za Kulevya kwa Mwaka 2023, inaonesha kulikuwa na aina mpya ya dawa hizo 1,184 zilizoingia katika soko la dunia," anasema. 

Kamishna Patric ana lingine la ziada; wamebaini meli zinazotumika kusafirisha dawa hizo zinapokuwa katikati ya maji ya kimataifa, boti za wahalifu hutoka nchi kavu na kuzifuata huko kuchukua dawa. 

Anaeleza sifa za boti hizo kwamba zina uwezo mkubwa wa kukimbia kushinda boti za wakaguzi, hali inayowawia ugumu kuwakamata wahalifu hao. Wanahitaji vifaa vya kisasa na wataalamu wenye uwezo mkubwa kukabiliana na uhalifu huo. 

Mfano wa waendesha mtandao wa ‘dark web’.

MATUMIZI YA DAWA 

Kamishna Patric anasema dawa za kulevya zinazotumika zaidi nchini ni bangi, mirungi, Heroin, Cocaine na tiba zenye asili ya kulevya ambazo zinatumika pia hospitalini. 

Anasema asilimia 85 ya Heroin inayotumika duniani kote inatoka Afghanistan. Matarajio yao kiwango cha uingizaji dawa hizo nchini kitashuka kutokana na kundi la Talbani kuchukua madaraka. Kundi hilo limepiga marufuku kilimo cha ‘Pop Plant’, zao linalozalisha Heroin. 

"Hii dawa huletwa nchi za mashariki na kusini mwa Afrika kuanzia Somalia, Kenya (hasa Mombasa), Tanzania (hasa Tanga, Mtwara na Lindi), Msumbiji mpaka Afrika Kusini (hasa Cape Town) kupitia Bahari ya Hindi kwa sababu zikizalishwa Afghanistan zinakwenda Iran au Pakistani. 

"Utafiti unaonesha kwamba, kati ya tani 50 na 100 za dawa za kulevya aina ya Heroin zinapita katika ukanda huu wa mashariki na Afrika, lakini kiasi kinachotumika nchini ni chini ya tani 10. 

"Hali hii haina maana kwamba sisi ni wazembe wa kudhibiti, hapana! Ni kutokana na uhalisia wa jiografia ya nchi yetu. Hivyo, iwe jua au mwezi, ni lazima wapitishe hapa ili kwenda Ulaya, China, Marekani na Australia," anasema Kamishna Patric. 

Anabainisha kuwa ripoti za matumizi ya dawa za kulevya zinaonesha mwaka 2022 kulikuwa na watu milioni 292 duniani wanaotumia dawa hizo. Kati yao, milioni 228 wanatumia bangi na milioni 13.9 wanatumia dawa zingine kwa njia ya kujidunga. 

Kamishna Patric anafafanua zaidi kuwa kati ya watu milioni 13.9 wanaojidunga dawa hizo, milioni 6.8 wanaishi na virusi vya homa ya ini na milioni 1.6 wanaishi na Virusi vya Ukimwi (VVU). 

"Kwa Tanzania utafiti uliofanyika mwaka 2014, unaonesha kulikuwa na watu 250,000 hadi 500,000 waliokuwa wanatumia dawa za kulevya aina ya Heroin. Kati yao, 30,000 walikuwa wanatumia kwa njia ya kujidunga. 

"Wakati huo, watu wengi waliokuwa wanatumia dawa hizo walikuwa wanaishi Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya na Dodoma ambayo hivi sasa inakuja juu kwa kuwa na idadi kubwa. Utafiti unaonesha asilimia 36 ya watu wanaotumia dawa kwa njia ya kujidunga, wanaishi na VVU. 

"Hali ni mbaya zaidi kwa wanawake. Utafiti unaonesha kuwa, kati ya wanawake 100 wanaojidunga nchini, 60 walikuwa wanaishi na VVU. Pia asilimia 90 ya kundi hilo wanafanya biashara ya ngono ili kupata fedha ya kununulia dawa hizo," Kamishna Patric anafafanua. 

Mfano wa ndege zisizokuwa na rubani zinazotumika kusafirisha vitu mbalimbali.

MADHARA KIAFYA

Dk. Saidi Kuganda, Bingwa wa Afya na Magonjwa ya Akili katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Idara ya Afya na Magonjwa ya Akili, anasema dawa za kulevya zina madhara mengi kiafya ya mwili kulingana na aina ya dawa, kiwango cha matumizi na muda wa matumizi. Pia zina madhara kwa akili na kijamii.  

Dk. Kuganda ambaye pia Mwenyekiti wa Chama cha Wataalam wa Afya ya Akili Tanzania (MEHATA), anayataja madhara kwa mwili, akisema: 

"Yanajumuisha magonjwa ya mfumo wa upumuaji; kuvuta dawa kama bangi au Cocaine husababisha matatizo ya mapafu, saratani ya mapafu na magonjwa ya upumuaji kama pumu. 

"Pia kupata magonjwa ya ini. Matumizi ya dawa kama heroin yanaweza kusababisha ugonjwa wa ini (cirrhosis) na kushindwa kufanya kazi kwa ini. 

"Magonjwa ya moyo; dawa kama Cocaine na Methamphetamine husababisha shinikizo la damu, mapigo ya moyo kutokuwa ya kawaida, na hatari ya mshtuko wa moyo. 

"Kuna kupata maambukizi; matumizi ya sindano zisizo safi husababisha maambukizi ya magonjwa kama vile HIV na hepatitis (homa ya ini). Pia kupungua uzito kupita kiasi kwa sababu dawa nyingi hupunguza hamu ya kula na kusababisha utapiamlo.

 "Madhara mengine ni magonjwa ya ngozi na kinywa, dawa za kulevya kama Heroin husababisha hitilafu katika mfumo wa umeme wa ubongo na kuleta kifafa ikiwa itatumika nyingi kupita kiasi au wakati wa kujaribu kupunguza au kuacha ghafla."

 MADHARA KIUCHUMI

Mfano wa waraibu wanaotumia dawa za kulevya kwa njia ya kujidunga.

Mhadhiri na Mtaalamu wa Biashara na Uchumi katika Chuo cha Biashara (CBE), Dk. Mariam Tambwe, anasema matumizi ya dawa za kulevya yana madhara makubwa kiuchumi kwa kuwa waraibu wakishatumia dawa, hawawazi kwenda kufanya kazi badala yake wanafikiria kwenda kuiba na kupora. 

Anasema wengi wao wakishatumia dawa, wanakuwa wanasinzia na kutokujihusisha na shughuli za uzalishaji, huku wengine wakifikia hatua ya hata kwenda kuiba majumbani mwao ili kupata fedha ya kununulia dawa hizo, jambo ambalo linachangia kurudisha nyuma uchumi wa familia.

 "Ushauri wangu kwa mamlaka husika, waongeze kasi katika kuzuia uingizwaji dawa za kulevya nchini, viongozi wa dini wasaidie kuwapa elimu ya kiimani vijana na watanzania kwa ujumla juu ili wajiepushe na matumizi ya dawa hizo.

 "Vilevile, wale vijana wote waliothirika kutokana na matumizi ya dawa hizo, wapewe usaidizi wa matibabu hospitalini, wakishapona wawezeshwe mitaji ya kufanya shughuli za kimaendeleo, pia wakasaidie kutoa elimu kwenye jamii juu ya madhara ya dawa hizo na kujiepusha nazo," anasema Dk. Mariamu.       

Katika kukabiliana na madhara hayo, Kamishna Patric anasema wanayo mikakati mikuu minne, ukiwano wa kuhakikisha wanapunguza uingizaji, uzalishaji na usambazaji dawa za kulevya nchini.

 Anataja mkakati wa pili ni kupunguza mahitaji kwa kutoa elimu kwa jamii kuhusu madhara yake ili watu wasijiingize katika matumizi ya dawa hizo na kuwezesha jamii kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini.

 Kamishna Patric anataja mkakati wao wa tatu ni kupunguza madhara yanayotokana na dawa za kulevya kwa kusimamia na kutoa ushauri kwa watumiaji kuhakikisha wanatumia dawa sahihi ili wasipate madhara.

 "Kwenye kupunguza madhara tunatibu na kusimamia matibabu ya waraibu wa dawa za kulevya katika maeneo mbalimbali kama nyumba za matibabu kwa waraibu na hospitalini ili kuhakikisha kwamba waathirika wanapata matibabu," anasema Kamishna Patric.

 Anataja mkakati wao wa nne ni kuimarisha ushirikiano wa kitaifa na taasisi mbalimbali zinazojihusisha na udhibiti wa dawa za kulevya kikanda na kimataifa kwa lengo kuhakikisha wanawadhibiti wauzaji wa dawa hizo ambao hawana mipaka.