KIVUMBI cha uzinduzi wa kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa kilianza rasmi jana katika maeneo mbalimbali kwa viongozi wa vyama vitatu vya siasa ambao wametawanyika kila kona.
Vyama hivyo ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ACT-Wazalendo.
Katika kampeni hizo, CCM ilizindua kwa viongozi na makada wakiwa katika mikoa tofauti huku CHADEMA ikifungua pazia kwa Makamu Mwenyekiti kufanya hivyo Ikungi mkoani Singida.
Aidha, viongozi wengine wa chama hicho watakuwa katika maeneo mbalimbali kuanzia leo huku Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, akitazamiwa leo kufufua kampeni leo mkoani Mbeya.
CCM NA 4R
CCM katika kampeni zake imejivunia kutumia falsafa ya 4R ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanya kampeni hizo kistaarabu na haihitaji kufanya kejeli wala matusi.
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla, alisema jana mkoani Dar es Salaam kuwa kampeni zitafanyika kistaarabu kwa sababu ni chama tawala kinachoongoza, hivyo kina ajenda na hoja nyingi za kushawishi Watanzania waichague.
Akizindua kampeni hizo kwa mkoa wa Dar es Salaam akiwa Temeke, Makalla alisema: “Mtu ambaye hana hoja ataendelea kutukana na kutoa vitisho, sisi tutawajibu kwa kampeni za hoja ili wananchi wapime wenyewe nani anapaswa kupewa kura.
"Tunaamini uchaguzi utakuwa huru na haki, CCM haihitaji mbeleko, tunaomba kila aliyejiandikisha akapige kura. Viongozi wanaowachagua wataonesha maeneo ya kujenga madarasa, zahanati na huduma nyingine za kijamii.
“Hatuwezi kumchagua mtu anayesema komaa kamanda, hatuwezi kuchagua kiongozi ambaye sera yake si kujenga shule na zahanati.”
Makalla aliagiza kampeni ya mtaa kwa mtaa, nyumba kwa nyumba, kitanda kwa kitanda, mtu kwa mtu ifanywe ili CCM ishinde.
Naye Mlezi wa CCM Mkoa wa Katavi na Naibu Katibu Mkuu wa Chama Zanzibar, Dk. Mohamed Said Dimwa, amelisihi wananchi wa mkoa huo bila kujali tofauti za kisiasa, kidini na kikabila, kuweka mbele maslahi ya maendeleo yao kwa kuwachagua wagombea wote wa chama hicho.
Akizungumza katika Kijiji cha Ikola A, Dk. Dimwa alisema ushindi kwa CCM katika uchaguzi huo una tija na manufaa makubwa kwa wananchi wote si kwa wanachama wa CCM pekee kwa kuwa fursa za maendeleo zinapatikana kutokana na mipango mizuri ya viongozi wanaotokana na chama hicho.
Kwa mujibu wa Dimwa, wagombea wote wa CCM watakaoshinda, watakuwa na kazi ya kuendeleza mikakati ya maendeleo iliyoachwa na viongozi waliomaliza muda wao ambao wamefanya mambo makubwa.
Dk. Dimwa pia alisema CCM imeendelea kuwa chama kiongozi katika ubobezi wa kisiasa hasa katika kutekeleza kwa vitendo ahadi zake kupitia utekelezaji wa ilani ya CCM ya mwaka 2020 -2025 kwa manufaa ya wananchi wote mijini na vijijini katika maeneo yote ya mkoa wa Katavi.
"Wito wangu kwenu wananchi nyote katika kata zote 58 zilizoko katika mkoa huu, jitokezeni Novemba 27, 2024 mkawapigie kura nyingi wagombea wote wa CCM ili wakatekeleze mahitaji yenu kwa vitendo,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Katavi, Idd Kimanta, alisema CCM imejipanga vizuri kuhakikisha wagombea wote wa chama hicho wanashinda katika maeneo yao.
WATAKAOSHINDA WAONYWA
Mkoani Dodoma, CCM imewataka wagombea watakaoshinda uchaguzi wa serikali za mitaa kutovimba kama maharagwe na kutanguliza maslahi binafsi kwa kuwa haitasita kuwaondoa katikati ya muhula wa uongozi.
Pia imeonya kuwa diwani atakayepoteza mtaa kwenye uchaguzi huo, atatakiwa kujitafakari kabla ya kugombea uchaguzi mkuu ujao.
Akizindua kampeni mkoani hapa kwa niaba ya Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango ambaye ni Mlezi wa Dodoma, Mwenyekiti wa CCM Mkoa huo, Adam Kimbisa, alisema wagombea wa nafasi za wenyeviti wa vijiji, mitaa na vitongoji hawapaswi kujigeuza kuwa miungu watu baada ya kuchaguliwa bali wahakikishe wanawahudumia wananchi na kusaidia kukivusha chama kwenye uchaguzi mkuu.
Alisema sera zinazotekelezeka na nidhamu ya chama ndio siri ya chama hicho kuendelea kuwapo madarakani na kuwaomba wananchi kuendelea kukiamini na kuchagua viongozi wake.
Pia aliwahimiza viongozi wa chama na jumuiya zake katika ngazi zote za mkoa, wabunge wa viti maalum na wale wa kuchaguliwa na wagombea wenyewe kushiriki ipasavyo kwenye kampeni ili chama hicho kipate ushindi.
‘PASSWORD’ YA CCM
Katibu wa Halmashauri Kuu, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (SUKI) ya CCM, Rabia Hamid, alisema vyama vya upinzani visitegemee mbinu iliyotumika katika uchaguzi wa serikali za mitaa kuwapiku kisiasa, itatumika kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Rabia ambaye ni mlezi wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, alisema wakati akizindua kampeni hizo kwenye viwanja vya Pasua Sokoni, Manispaa ya Moshi kuwa hizo ni salamu kwa wapinzani kwamba atambue CCM inatambua umuhimu wa kuweka serikali za mitaa madarakani. Alisema viongozi wa mitaa ni watu muhimu wanaokaa na wananchi na kuwataka kutotabiri kuwa mbinu inayotumika sasa itatumika tena mwakani.
Alisema kishindo cha CCM katika kampeni hizo ni ishara kwamba chama hicho hakina jambo dogo.
CHADEMA MOTO
Baada ya Lissu kuzindua rasmi kampeni hizo jana. CHADEMA inatarajiwa kuonesha makala yake zaidi leo wakati Mbowe akiwa Mbeya na Lissu atakuwa Tarime mkoani Mara.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chama hicho, John Mrema, Naibu Katibu wa CHADEMA Zanzibar, Salum Mwalimu, atakuwa Bunda Mjini.
Aidha, Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema, atanguruma Kilombero mkoani Morogoro na Lucas Ngoto atakuwa Tarime.
ACT KIGOMA, PWANI
Viongozi waandamizi wa Chama cha ACT-Wazalendo, wametawanyika katika maeneo mbalimbali kunadi wagombea wake, kuanzia jana.
Ofisa Habari wa ACT-Wazalendo, Abdallah Hamisi, alisema jana kuwa kiongozi wa chama hicho, Dorothy Semu, ataendesha kampeni mkoani Pwani wakati kiongozi mstaafu, Zitto Kabwe, atapiga kambi Kigoma.
“Viongozi wetu wote pamoja na wajumbe wa Kamati Kuu wametawanyika maeneo mbalimbali. Makamu Mwenyekiti, Isihaka Mchinjita, atakuwa Morogoro, Naibu Katibu Mkuu (Bara), Ester Thomas yuko Mwanza na Ismail Jussa yuko Tanga,” alisema.
Alisema Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho, Juma Duni Haji, atanadi wagombea wa Dar es Salaam wakati Katibu Mkuu wa chama, Ado Shaibu, atakuwa Tunduru.
Imeandikwa na Romana Mallya, Elizabeth Zaya, Restuta James (Dar), Marry Mosha (Moshi) na Augusta Njoji (Dodoma)
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED