Jeneza lakutwa shambani, ladaiwa kufichwa na mganga wa kienyeji

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 12:03 PM Sep 26 2024
Mkazi wa Mtaa wa Mwime-Makungu, Kata ya Mwendakulima, wilayani Kahama, mkoani Shinyanga, Kumalija Budeba (kushoto), akijiandaa kulipakia jeneza kwenye gari la polisi, baada ya kukamatwa akiwa ameliweka shambani kwake jana na kusababisha taharuki.
PICHA: SHABAN NJIA
Mkazi wa Mtaa wa Mwime-Makungu, Kata ya Mwendakulima, wilayani Kahama, mkoani Shinyanga, Kumalija Budeba (kushoto), akijiandaa kulipakia jeneza kwenye gari la polisi, baada ya kukamatwa akiwa ameliweka shambani kwake jana na kusababisha taharuki.

WAKAZI wa mtaa wa Mwime - Makungu, kata ya Mwendakulima, Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, mkoani Shinyanga, wamepatwa na taharuki baada ya Kumalija Budeba (55) anayedaiwa kuwa ni mganga wa jadi kukutwa akiwa ameficha jeneza tupu kwenye kichaka kilichoko karibu na shamba lake huku akiwazuia watu kupita karibu na eneo hilo.

Tukio hilo lilitokea jana baada ya vijana waliokuwa wakichunga mifugo kuona jeneza hilo kisha kutoa taarifa kwa uongozi wa mtaa; nao ulitoa taarifa polisi waliofika na kumchukua Budeba kwa hatua za kisheria.

Kiongozi wa walinzi wa jadi katika mtaa huo, Someke John alisema kuwa baada ya kufika eneo la tukio walilazimika kulifungua ili kujiridhisha kama kulikuwa na mwili wa binadamu kutokana na taarifa awali kudai kuwamo maiti ndani ya jeneza hilo, lakini lilikuwa tupu.

Alisema kuwa walipomhoji alikiri kulifahamu na kudai kuwa lilikuwa linatumiwa na msanii (jina lake tunalo) aliyefika nyumbani kwake kumfundisha kijana wake namna ya kuimba nyimbo za asilia kwa ajili ya kutumbuiza kwenye matamasha ambayo wamekuwa wanafanya na aliweka shambani mwezi Julai mwaka huu ili watu wasipite.

Mkazi wa Mtaa wa Mwime, Matha Mihambo, alisema jeneza hilo limewashangaza kwani katika uwasilishaji sanaa ya muziki wa nyimbo za asili, hakuna kipengele cha kutumia jeneza, hivyo Kumalija alipaswa kuwa na kibali cha kulitumia na kuliweka nyumbani ili kutoibua maswali kwa wananchi.

Alisema hawajawahi kuona sanaa ya nyimbo za asili za jamii ya kisukuma ikitumia jeneza katika matamasha ya muziki na badala yake wamezoea kuona ikitumia nyoka wakubwa na kuomba serikali kumbana zaidi ili kujua alikuwa na maana gani kuwa na jeneza hilo shambani.

Budeba akiwa kwenye gari la polisi, baada ya kukamatwa. PICHA: SHABAN NJIA
Awali akieleza kuwapo jeneza hilo shambani kwake, Kumalija Budeba alikiri kufahamu kuwapo jeneza hilo, akidai walikuwa wanalitumia kwenye matamasha ya muziki wa asili tangu mwaka jana.

"Msanii wangu ... (anataja jina la msaani wa Kanda ya Ziwa) aliliacha hapa baada ya kumaliza matamasha ya ngoma za asili. Nimeshangaa kuona kundi la watu wakivamia nyumba yangu, wakihoji juu ya uhalali wake na nina kibali kutoka Manispaa ya Kahama," alidai Budeba.

Hata hivyo, Ofisa Utamaduni wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, Felix Ntibabara, alisema hawajawahi kutoa kibali cha matumizi ya jeneza kwa ajili ya shughuli za sanaa za asili na katika uwasilishaji maudhui ya nyimbo za asili ni kosa kutumia aina hiyo ya sanaa kwani ni kuwatisha wananchi badala ya kuwaburudisha.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, ACP Kennedy Mgani alithibitisha kukamatwa kwa Budeba na kuwa uchunguzi wa tukio hilo unaendelea ili kujua chanzo cha jeneza hilo kuwa shambani kwa mganga huyo.

Kamanda Mgani alisema jeneza hilo hivi sasa liko Kituo cha Polisi Kahama na ikibainika alikuwa analitumia kwenye vitendo viovu, atawajibishwa kwa mujibu wa sheria.