Familia yafichua siri ndugu yao alivyopigwa hadi kufariki dunia

By Allan Isack , Nipashe
Published at 11:33 AM Sep 26 2024
Familia yafichua siri ndugu yao  alivyopigwa hadi kufariki dunia
Picha:Mtandao
Familia yafichua siri ndugu yao alivyopigwa hadi kufariki dunia

MAPYA yameibuka kuhusiana na kifo cha utata cha mfanyabiashara wa vyuma chakavu katika Kata ya Muerieti, Johnson Josephat, maarufu kama Sonii (39), anayedaiwa kufariki dunia baada ya kutoroshwa na kundi la watu waliokuwa wakipinga kukamatwa kwake baada ya kufungwa pingu mkono mmoja na Polisi.

Sonii, Mkazi wa Unga Limited jijini Arusha, alifariki dunia Septemba 23, mwaka huu, katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru, wakati akipatiwa matibabu. 

Akizungumzia tukio hilo lililoibua simanzi katika viunga vya jiji la Arusha, mke wa marehemu, Nasra Bakari, alisema mtoto wake alishuhudia tukio zima la baba yake kupigwa na askari polisi, na ndiye aliyekwenda akikimbia kumpa taarifa kwamba baba anapigwa. 

“Nilitoka nje nikakuta wamemnyonga, kichwa kwenye mapaja, mkono nyuma. Walikuwa askari wawili, nikaingia hapo tukawa tunaparangana nao, tukahangaika nao, (marehemu) akachomoka akakimbia akaanguka, akaangukia kichwa. 

“Baada ya kuanguka, wakatokea tena watu wengine maana kulikuwa hakuna wanaume, ni wanawake tu. Wakaendelea kupambana na wale askari wawili, yule baba akakimbia tena akaingia uchochoroni na wale askari tena wakamkimbiza wakamfuata huko uchochoroni. 

“Huko uchochoroni kuna mabanzi, hiyo nyumba ina mabanzi, wakawa wamemchukua wamemwingiza kwenye hayo mabanzi, kichwa kikawa kimeingia huko, ukabaki mwili. Hatukufika pale kwa sababu kulikuwa hakuna wanaume, tulikuwa tunaparangana na wale maaskari wakamkanyaga kichwa,” alisema. 

Kutokana na vuta ni kuvute hiyo, mke wa marehemu alisema bahati nzuri, baada ya wanawake wale kuona hali ilivyo, walikwenda kuita wanaume ambao walifika sehemu walipokuwa wameingiza kichwa chake kwenye mabanzi na kubaini kwamba  ameshapoteza fahamu, ndipo wakampeleka hospitalini. 

 Nasra, kupiti video iliyosambaa mtandaoni, alifafanua zaidi mkasa huo ulivyokuwa akisema: “Sasa wenyewe wanavyojielezea wanasema kuna mtu alikamatwa yuko huko Central (Kituo Kikuu cha Polisi Arusha), aliiba kompresa akamuuzia yeye (marehemu). Sasa tulivyofika eneo la tukio, nikawaambia haya masuala si ya kuongea kama mnaye. 

“Wakasema hatutaki kuongea tunataka tumpeleke polisi. Baada ya tukio, walikuja askari wengine, ndiyo wakampeleka Mount Meru, tangu hapo alikuwa ameshafariki (dunia). 

“Maana yake walihangaika kufungua ile pingu tangu tukiwa huku nyumbani. Tulipofika Mount Meru wengine wakarudi Central kutafuta funguo nyingine wakafungua ile pingu, ndio wakamwingiza hospitalini. Alikuwa ameshafariki tangu akiwa nyumbani.” 

Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa Septemba 24 na Kamanda wa Polisi, Kamishna Mwandamizi Msaidizi wa Polisi (SACP) Justine Masejo, tukio hilo lilitokea Septemba 23, saa 11:30 jioni.

 Taarifa hiyo ilisema askari polisi ambaye hajatajwa jina wala namba yake ya kijeshi, alifika maeneo ya Unga Limited kwa ajili ya kumkamata mtu huyo kuhusiana na tukio za kuvunja stoo na kuiba.

 Iliongeza taarifa hiyo kwamba wakati wa ukamataji, askari alifanikiwa kumvisha pingu mkono mmoja, ndipo lilipojitokeza kundi la watu na kumshambulia askari kumkamata mtu huyo na kumtorosha kwa kutumia pikipiki.

 Kwa mujibu wa SACP Masejo, taarifa za awali zinaonyesha kuwa katika harakati za kumtorosha mtu huyo, alianguka na baadaye ndugu walimfikisha hospitalini.

 Kamanda Masejo alisema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea ili kubaini kilichosababisha kifo na wote waliohusika watachukuliwa hatua za kisheria.