MAMENEJA wa hifadhi za bahari na wakuu wa doria wametakiwa kushirikiana na jamii kudhibiti uvuvi haramu visiwani hapa.
Wito huo ulitolewa jana na Mkurugenzi wa Idara ya Uhifadhi wa Bahari, Dk. Makame Omar Makame wakati wa kikao cha tathmini ya doria ya Novemba mwaka huu kilichofanyika visiwani hapa.
Dk. Makame, alisema licha ya kuwepo kwa vitendo vya uvuvi haramu, kiasi kikubwa bahari imerudi katika hali yake ya ubora kutokana na kudhibiti zana haramu za uvuvi katika maeneo ya hifadhi za bahari.
Alisema hatua zaidi zitaendelea kuchukuliwa kwa wavuvi watakaoendelea kuvua samaki na mazao ya bahari ndani ya mwamba na nyavu za utari na madema ya waya.
Alisema uvuvi haramu unachangia uharibifu wa mazingira na mazalia ya samaki, hivyo ni vyema kila mmoja kuwajibika kudhibiti uvuvi huo.
Nuru Said kutoka Taasisi ya Mwambao, alisema wataendelea kushirikiana na Serikali kuimarisha uhifadhi wa bahari, rasilimali na mazingira.
Nuru, alisema bahari ni rasilimali muhimu kwa maendeleo ya taifa, hivyo ni vyema itunzwe na kuhifadhiwa ili kukabiliana na uharibifu na uchafuzi wa bahari.
Ofisa Uvuvi wa Wilaya ya Kati Unguja, Ali Mwalim Mahafoudh, alisema elimu zaidi ya umuhimu wa matumizi mazuri ya bahari na ukataji wa leseni kwa wavuvi na vyombo vyao itaendelea kutolewa kwamujibu wa sheria.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED