Soko la Maduka Kibaha kuingiza Sh. milioni 660 kwa mwaka

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 08:32 PM Dec 06 2024
Soko la Maduka ya Kisasa (Shopping Mall).
Picha: Mpigapicha Wetu
Soko la Maduka ya Kisasa (Shopping Mall).

SHILINGI Milioni 660 zinatarajiwa kukusanywa kwa mwaka katika Soko la Maduka ya Kisasa (Shopping Mall) linalozinduliwa kesho Jumamosi Desemba 07,2024 Mjini Kibaha.

Afisa Mapato wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Luna Kakuru ameeleza hayo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusiana na uzunduzi wa soko hilo.

Amesema soko hilo ni kati ya miradi ya kimkakati iliyotekelezwa na serikali ambalo hadi kukamilika limegharimu  Sh.bilioni 8.

Luna amesema wanategemea baadae mapato kuongezeka zaidi kutokana na huduma zitakazoendelea kutolewa ikiwepo maeneo ya maegesho ya magari.

Naye Afisa Masoko wa soko hilo Sabrina Kikoti amesema ufunguzi wa Kibaha Shopping Mall unakwenda kufungua uchumi wa Mji wa Kibaha kutokana na huduma za kisasa za kibiashara zitakazokuwa zinatolewa.

Sabrina ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha hizo ambazo zimetekeleza mradi huo unaokwenda kutoa huduma nyingi  huduma nyingi ambazo wananchi walikuwa hawazipati kwa wakati.

Amesema katika ufunguzi huo wafanyabiashara mbalimbali wakubwa watashiriki wakiwemo wasanij kutoka ndani na nje ya Mji wa Kibaha.

Charles Chandika ni mmoja wa wafanyabiashara wa soko hilo ambaye amesema uwepo wa soko hilo ni fursa kwa wafanyabiashara kutoa huduma mbalimbali kwa wakazi wa mji huo kwa gharama nafuu.

Naye Lidya Vicent mfanyabiasha wa nguo katika soko hilo amesema uwepo wa soko hilo umewawezesha kupata fursa ya mahali sahihi pa kuuzia bidhaa zao .

Kabla ya ujenzi wa soko hilo wananchi wengi walikuwa wanafuata bidhaa mbalimbali katika soko la Kariakoo ambapo kwasasa watazipata hapo na wataokoa fedha za nauli na muda mwingi waliokuwa wakiutumia awali.