Serikali yatoa billion 143.9 kuboresha maisha ya wananchi Magu

By Neema Emmanuel , Nipashe
Published at 05:31 PM Dec 24 2024
Mbunge wa Jimbo la Magu, Boniventura Kiswaga.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mbunge wa Jimbo la Magu, Boniventura Kiswaga.

Serikali imetoa Shilingi Bilioni 143.9 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani Magu, mkoani Mwanza.

 Akizungumza kuhusu utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kipindi cha 2020 hadi 2024, Mbunge wa Jimbo la Magu, Boniventura Kiswaga, alisema zaidi ya Shilingi Milioni 336.7 zilitumika kupitia Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo, ambapo miradi 52 ilifadhiliwa, ikiwa ni pamoja na 28 ya afya, 20 ya elimu, 3 za utawala, na moja ya barabara.

Miradi ya barabara ilipokea zaidi ya Shilingi Bilioni 78.8, huku Shilingi Bilioni 7.1 zikitumika kwa ajili ya matengenezo ya barabara katika Wilaya ya Magu. 

Miradi mingine ni ujenzi wa kivuko cha Ijinga-Kahangara unaogharimu Shilingi Bilioni 5.3, na utaratibu wa maji ulipokea Shilingi Bilioni 12.1, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa tenki la Bujora-Kisesa lenye uwezo wa lita milioni 5, ambalo linatarajiwa kukamilika Februari 2025.

Kwa upande wa elimu, Jimbo la Magu lilipokea Shilingi Bilioni 31 kutekeleza miradi ya shule na vyuo vya ufundi, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vyuo viwili vya ufundi, mmoja katika kijiji cha Nsola cha VETA na mwingine kwa ajili ya watu wenye ulemavu.

Zaidi ya bilioni 21 zilitumika kutekeleza miradi ya elimu sekondari, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vyumba vya madarasa, nyumba za walimu, na matundu ya vyoo katika shule mbalimbali. 

Katika elimu ya msingi, Halmashauri ya Magu ilitekeleza miradi yenye thamani ya zaidi ya bilioni 7.3, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa shule mpya za msingi na vyumba vya madarasa.