Kampuni ya Puma yaunga mkono azimio gesi safi ya kupikia, kuwezesha upatikanaji Afrika

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:39 AM May 20 2024
Kutoka kushoto ni Omar Zaafrani, Mkuu wa Mawasiliano na Mazingira, Jamii na Uongozi Bora wa kampuni ya Puma Energy duniani,Fatma Abdallah, Meneja Mkuu wa Puma Energy Tanzania, na Carina Schacherl, Kiongozi Mkuu wa kampuni ya Puma Energy duniani.
Picha: Mtandaoni
Kutoka kushoto ni Omar Zaafrani, Mkuu wa Mawasiliano na Mazingira, Jamii na Uongozi Bora wa kampuni ya Puma Energy duniani,Fatma Abdallah, Meneja Mkuu wa Puma Energy Tanzania, na Carina Schacherl, Kiongozi Mkuu wa kampuni ya Puma Energy duniani.

Kampuni ya Puma Energy imethibitisha dhamira yake ya kuwezesha upatikanaji wa nishati na ufumbuzi wa upikaji safi wakati wa Mkutano wa Kimataifa wa Upikaji Safi Barani Afrika (IEA) uliofanyika jijini Paris, Ufaransa.

Mbali na serikali, kampuni kutoka sekta binafsi, mashirika ya kimataifa na asasi za kiraia zilihudhuria Mkutano huo uliofanyika Paris Mei,14, Puma Energy iliunga mkono Azimio la Upikaji Safi, ambalo limejizatiti kuifanya 2024 kuwa mwaka muhimu kwa upikaji safi.

Kwa kushiriki katika azimio hilo, Puma Energy imeahidi "kuchukua hatua madhubuti katika kuendeleza ajenda ya upikaji safi, kupitia hatua madhubuti, kuongeza uelewa, na kukuza ushirikiano zaidi miongoni mwa wadau muhimu."

Mkuu wa Afrika wa Puma Energy, Fadi Mitri, alisema : "Tunajivunia kuunga mkono na kuendeleza suluhisho la upikaji safi katika jamii tunamofanyia kazi,"

Aliongeza kuwa; "Tunaamini kwamba gesi safi (LPG) ya kupikia ni suluhisho muhimu kwa mabadiliko ya nishati barani Afrika - ikitoa njia mbadala za kupikia zenye manufaa ya kiafya na safi ambayo inanufaisha watu na mazingira."

Kulingana na makadirio ya IEA, takriban watu milioni 970 hawana uwezo wa kupata nishati safi ya kupikia na teknolojia katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara. Kaya nyingi zinategemea kuni na mkaa, au mafuta ya taa, na zinazopelekea hatari za kimazingira na kiafya.

Puma Energy inatoa suluhisho la nishati salama, kutegemewa na nafuu katika nchi zote za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, na inahimiza mabidiliko ya nishati safi na bora ya kupikia kupitia upatikanai wa gesi safi ya kupikia (LPG). Gesi hii inayopatikana katika mitungi ni safi zaidi, salama na inabebeka, na inaweza kufikia jamii za mijini na za maeneo ya vijijini yasiyofikika kwa urahisi.

Kampuni hiyo imeongeza ufumbuzi wa LPG katika miaka iliyopita, kwa kuanzia na uzinduzi wa biashara ya LPG nchini Tanzania, ambapo Puma Energy inatumia teknolojia kurahisisha upatikanaji wa LPG kwa watumiaji na wasambazaji na inaweza kufuatilia taarifa zake ili kusaidia kupunguza upotevu wa mitungi na kuboresha mzunguko wa upatikanaji wake.

Ahadi ya Puma Energy ya kuwezesha upikaji safi inaenda sambamba na Mkakati wa Upikaji Safi wa Tanzania wa 2024-2030, uliozinduliwa mapema mwezi Mei na Rais Samia Suluhu Hassan ambaye alikuwa mwenyekiti wa Mkutano wa Wakuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati (IEA) kuhusu Upikaji Safi uliofanyika jijini Paris.

Mkakati wa Upikaji Safi wa Tanzania unalenga kubadilisha asilimia 80 ya watu kuhamia katika upikaji safi na inatoa wito kwa sekta binafsi kuongeza uwekezaji katika upatikanaji wa gesi safi (LPG).  Fatma Abdallah, Meneja Mkuu wa Puma Energy Tanzania amesema, “Gesi safi ni njia salama, rahisi na ya gharama nafuu ya kuziwezesha jamii zetu; kuwezesha upikaji safi na kupunguza athari zinazotokana na nishati asilia za kupikia. Zaidi ya matumizi ya nyumbani, gesi safi pia ni chanzo muhimu cha nishati kwa matumizi ya kibiashara na viwandani, ikiwemo hoteli, migahawa, hospitali, shule na maduka makubwa ya manunuzi ya bidhaa mbalimbali. 

Kampuni hiyo ilipanua zaidi upatikanaji wa LPG mwaka 2023 kwa kuinunua Ogaz ambayo inasambaza asilimia 18 ya soko la LPG nchini Zambia. Pia kwa ushirikiano na benki kubwa zaidi ya Zambia, Zanaco, Puma Energy ilizindua mpango wa mikopo midogo midogo ili kutoa suluhisho kwa watumiaji wapya wa LPG ambao hawawezi kumudu gharama ya awali ya ununuzi wa vifaa muhimu vinavyohitajika.