Siku kadhaa zilizopita, serikali ya Tanzania ilitangaza mlipuko wa ugonjwa wa ‘Red Eyes’ yaani macho mekundu. Ni macho yaliyopata wekundu, yanayowasha na kuwa na viashiria vya damu (bloodshot).
Wataalam wa afya nchini wanasema wekundu huu hutokea pindi mishipa midogo ya damu chini ya uso wa jicho inapotanuka au kuvimba.
Kwamba mara nyingi, ni athari ya ukereketaji (irritation) au maambukizi (infection) ya kwenye jicho.
Macho mekundu yanaweza kuathiri jicho moja au yote mawili. Halafu si mambo yanayoibuka kimazingira mazingira kama baadhi ya watu wanaoamini ushirikina wanavyodhani.
Madaktari bingwa wa macho wanaeleza kwamba ni hali ambayo inaweza kutokea taratibu au kwa ghafla, kama vile kwa matatizo ya mzio au jeraha la jicho.
Nataka kusema nini? Nitajikita kuzungumzia hatari ninayoiona kuhusu baadhi ya Watanzania, hasa walioko pembezoni au vijijini, kupuuza tahadhari iliyotolewa na Wizara ya Afya namna ya kujikinga na maradhi haya.
Wako ndugu zetu huko pembezoni na hata mjini, ambao wanajikinga eti kwa kutumia dawa zisizo rasmi, wakiamini wameangaliwa vibaya na mahasimu wao kiuchumi, majirani na wasiopenda maendeleo yao.
Aisee, acha huo ujinga. Hakuna uhusiano wowote wa ugonjwa huu na ushirikina. Ukiona dalili nilizozitaja, nenda hospitalini daktari akusikilize, afanye yanayompasa kitabibu na akuandikie dawa ili kuepuka madhara kwa kuwa dawa za macho ni tofauti na kwa matumizi tofauti.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Tiba katika Wizara ya Afya, Prof. Pascal Ruggajo, maambukizi ya ugonjwa huo kwenye ngozi ya juu ya gololi ya jicho yajulikanayo kitaalam kama viral ‘keratoconjunctivitis’. Ni maambukizi yanayosambaa kwa kasi kubwa.
Hakuna tiba maalum kwa ugonjwa huu na hata bila tiba, dalili huisha zenyewe ndani ya wiki mbili.
Taarifa zaidi zilizochapishwa katika tovuti ya Wizara ya Afya, zinaeleza kwamba kutokana na tabia ya ugonjwa huo kusambaa kwa kasi, maambukizi hayo huleta mlipuko unaosambaa kupitia kirusi kwa zaidi ya asilimia 80.
Kanzidata yao inaeleza kwamba kati ya Desemba 22 na Januari 11, mwaka huu, mkoa wa Dar es Salaam peke yake ulikuwa na wagonjwa waliojitokeza katika vituo vya kutolea huduma ya afya wapatao 869.
Iko hivi! katika maisha,poteza vyote ila usipoteze matumaini. Ukipoteza matumaini, umepoteza sababu ya kuishi kwa sababu, hasira ya mwanadamu haiwezi au kuathiri hitaji lake.
Ni muhimu kufanya uchunguzi wa afya yako, kwa kadiri utakavyoshauriwa na wataalam wa afya.
• Godfrey Mushi ni Mwandishi Mwandamizi wa Gazeti la Nipashe, Kanda ya Kaskazini. Anapatikana kwa barua pepe: [email protected]. Simu ya mkononi: +255 715 545 490
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED