Kuingiza Jeshi mitaani kufanya usafi wapi na wapi?

By Ida Mushi , Nipashe Jumapili
Published at 08:07 AM Jan 22 2024
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,  Albert Chalamila.
PICHA: MTANDAONI
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila.

VIONGOZI! Viongozi! Viongozi! Nimekuiteni mara tatu! Nimekuiteni nikitaka mtwambie, hivi Jumatano ijayo ya Januari 24, mwaka huu, tunaandamana au tunafagia mitaa?

Viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mnawaambia wafuasi wenu kuwa siku hiyo ni maandamano ya kushinikiza kuondolewa miswada mibovu bungeni, kulalamikia gharama za maisha na kuheshimu maoni ya wananchi.

Ni maandamano yanayohanikizwa kufanyika katika Jiji la Dar es Salaam ambako wafuasi wa chama hicho tayari wameambiwa maeneo ya kukusanyika kupita na kumalizia maandamano hayo, yanayosemekana kuwa ya amani.

Kwa kuwa yamepangwa kufanyika Dar es Salaam, Gavana wa Mkoa huo, Albert Chalamila, naye amewaambia wakazi wa jiji hilo, kuwa siku hiyo kutakuwa na usafi utakaofanywa na wanajeshi.

Hajaishia hapo akasema yeyote atakayekuwa mtaani akijifanya ni takataka, atazolewa na wanajeshi hao na kuishia dampo. Hapo sasa ndipo tunapochanganyikiwa na kujikuta njia panda.

Kwamba kama kuna maridhiano, ni vipi wakuu hawa wa pande hizi mbili wanashindwa kukaa pamoja na kukubaliana nini kianze kati ya usafi na maandamano!

Kama kweli kuna watu wamejiandaa kusafisha mitaa, inawezekana ni kwa ajili ya kuwezesha waandamanaji kupita bila kunukiwa na takataka, basi ingekubaliwa siku moja kabla usafi ufanyike na siku inayofuata maandamano yafanyike.

Au kama hilo haliwezekani, basi maandamano yafanyike siku moja kabla ya usafi, ili takataka zitakazokuwa zimetupwa mtaani na waandamanaji, zizolewe na wazoaji ili kuacha jiji likiwa safi.

Lakini unaweza kujiuliza, ni kwa nini basi wanajeshi watumike kufanya usafi wa Jiji wakati tuna kampuni zimesajiliwa kwa kazi hiyo, na zinalipwa na sisi wananchi tunaozalisha takataka hizo!

Mathalan kama ndivyo, kuwa sasa wanajeshi wetu wanataka kutumika kufanya usafi, sijui ni kwa sababu hatuna vita au nini? Mbona shuleni tulifundishwa kuwa kunapokuwa na amani hakuna vita, wanajeshi hutumika kuokoa raia kwenye majanga.

Juzikati tumemaliza kuwashuhudia wakiwa Hanang, Manyara wakiokoa na kuopoa waliokumbwa na maporomoko ya ardhi, likiwa ni moja ya majukumu yake ya kusaidia jamii. Lakini kama usafi wa mitaa ni sehemu ya kusaidia jamii, sawa.

Mwaka 2020 mwito wa maandamano kama haya, ulitolewa ukihamasishwa na mwanaharakati Mtanzania aishie Marekani, Mange Kimambi, akidai yangekuwa yasiyo na ukomo na kuitikisa serikali ya mkoa wa Dar es Salaam.

Mtikisiko huo ukamfikia Mkuu wa Mkoa wa wakati huo, Paul Makonda, akatangaza kuwa siku hiyo ya Novemba 2 ingekuwa ya usafi ukifanywa na wanajeshi. Hata hivyo hofu hiyo ilikuwa ya bure, hayakufanyika.

Chalamila anapita mlemle, akionya waandamanaji watarajiwa kuwa siku hiyo atakayekuwa mtaani kama takataka akimaanisha waandamanaji atajikuta amezolewa na kupelekwa dampo, maana yake lupango.

Mpaka sasa nashindwa kuelewa ni kwa nini jeshi linahusishwa na masuala haya ya kisiasa kwamba kiongozi mwenye dhamana ya kulinda usalama wa raia anapotaka kuzuia jambo hasi basi ahusishe jeshi kweli?

Siku zote masuala kama haya ya mikusanyiko, Jeshi la Polisi limekuwa likibeba dhamana kwa kuwa na jukumu la kulinda usalama wa raia na mali zao ikiwa ni pamoja na maandamano ambapo waandamanaji hupaswa kutoa taarifa za kuwapo mipango hiyo.

Jeshi la Polisi linapoona kuwapo ukakasi na viashiria vya uvunjifu wa amani na usalama, huwasiliana na watoa taarifa na kuwaeleza nini kimejiri na nini kifanyike na kuelewana, vinginevyo hutakiwa kutoa ulinzi kwa waandamanaji.

Kama Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Rais Samia Suluhu Hassan alishafungulia mikutano ya hadhara na maandamano ya amani, kuna sababu gani ya kusingizia usafi, ilhali hakuna viashiria vya uvunjifu wa amani?

Hivi kweli mwaka 1978 majeshi ya Uganda yalipovamia Tanzania na kufanya uharibifu, kama Chalamila angekuwa Rais na kubaini mapema kuwapo mipango ya uvamizi huo, angethubutu kuwaambia wanajeshi wakafanye usafi mkoani Ziwa Magharibi au wakabiliane na wavamizi? 

Rais wakati huo, Mwalimu Julius Nyerere, alitoka hadharani na kusema: “sababu, nia na uwezo wa kuwapiga tunao” wala hakuzunguka mbuyu. Sasa  kwa nini CHADEMA wasiachwe wakaandamana na mwishowe wakasikilizwa hoja zao?

Au kwa nini wasiambiwe ukweli tena kwa ushahidi, sababu za kuzuia maandamano yao badala ya kusingizia usafi wa mitaa, ambao haumo hata kwenye majukumu ya Jeshi?  Mungu tusaidie Watanzania.