MWENYEKITI wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, ameibua hoja mpya kwa madai kwamba wabunge wamejiongezea mishahara kutoka Sh. milioni 13 hadi Sh. milioni 18 kwa mwezi.
Amesema wabunge wamejiongezea mishahara hiyo wakati wananchi wanataabika na upandaji wa bei za bidhaa na hali ngumu ya maisha.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika mji wa Babati, mkoani Manyara, Mbowe amesema: “Mpaka tunatoka bungeni (mwaka 2020), mimi na (Godbless) Lema tulikuwa wabunge tunajua tunalipwa mshahara wa Sh. milioni 13 kwa mwezi. “Hiyo ni bila ya posho ya siku ya kikao. Posho ya kikao kimoja kwa siku ilikuwa Sh. 220,000,” amesema.
Kwa mujibu wa Mbowe, wabunge walijiongezea mishahara mwaka jana wakati wananchi wakiendelea kupata shida ya mfumuko wa bei.
Amesema uchumi wa nchi ulivyo kwa sasa unakuwa wa watu wachache na kwamba kuna watu wanaishi peponi na kuna wengine kama wanaishi jehanamu.
“Wananchi asilimia 70 wanaishi maisha ya umaskini na tofauti ya kipato imekuwa kubwa mno. Gharama za chakula, mafuta na tozo vinapanda. Maisha yanazidi kuwa magumu na sisi tusiposema nani atasema?” amehoji Mbowe.
Wakati huohuo, Mbowe ametangaza kuanza kwa maandamano kila makao makuu ya mkoa ya Tanzania Bara.
Kwa mujibu wa Mbowe, CHADEMA imekita kambi Babati, Manyara, kwa ajili ya kuandaa maandamano hayo ya amani, yanayotarajiwa kuanza Aprili 22, mwaka huu hadi Aprili 30.
“Tutaandamana kwa amani, tunataka wananchi ambao wanaona gharama za maisha ni kubwa tuingie barabarani ili tudai kupungua kwa mfumuko wa bei,” amesema Mbowe.
KAULI ZA WABUNGE
Mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Kasheku 'Musukuma' alipoulizwa kuhusiana na madai hayo, amesema : “Hilo nadhani ungempigia Spika. Kwanza mimi sijawahi kuona mshahara, sijawahi hata kufungua akaunti kwa ajili ya mshahara.”
Mbunge wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina, majibu yake hayakutofautiana na mwenzake ambaye amesema ,:“Maslahi ya wabunge ungemuuliza Spika ndiye angekueleza.
“Mbunge ana taasisi yake ambayo ndiyo yenye majibu. Hupaswi kumuuliza mbunge individual (binafsi). Unavyoniuliza ni kama mwandishi ambaye hujui taratibu tangu lini Mbunge akazungumzia maslahi yake?” amehoji
Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CHADEMA), Aida Khenani, alipoulizwa kuhusu madai hayo, amesema, “Mimi sijui. Niliulizwa nikasema silijui kwa hiyo siwezi kuwa na neno la kusema kuhusu hilo.”
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED