KLABU ya Yanga bado imeendelea kumng'ang'ania mchezaji Yusuph Kagoma, ikisema ni mchezaji wao halali na alisaini mkataba wa miaka mitatu, Machi 28, mwaka huu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Sheria wa Klabu ya Yanga, Mwanasheria, Simon Patrick, amesema tayari suala hilo wamelipeleka kwenye Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ila bado halijafanyiwa kazi ili kutoa uamuzi.
Amesema lengo la kuliweka hadharani jambo hili ni kutaka wanachama, mashabiki wa wadau wengine wa soka walielewe kwani limekuwa na sintofahamu kubwa.
Kagoma kwa sasa ni mchezaji wa Simba aliyesajiliwa kutoka Fountain Gate na yupo nchini Libya kukitumikia kikosi hicho ambacho Jumapili kitacheza mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Ahly Tripoli.
Mwanasheria ambaye alionyesha karatasi za malipo ya pesa kwa klabu ya Singida Fountain Gate na mkataba wa mchezaji huyo, aliitaka kamati hiyo kuamua mambo matatu, kutamka kuwa Kagoma ni mchezaji wa Yanga, pili isimamie kanuni zake kwamba mchezaji anayesaini zaidi ya klabu moja afungiwe, au watoe adhabu na fidia ya kuvunjwa mkataba wao kihuni.
"Machi 4, mwaka huu klabu ya Yanga kupitia kamati ya utendaji walianzisha mchakato wa kumnunua kutoka Singida Fountain Gate, baada ya muda mwafaka kufika Fountain Gate ilitoa masharti kuwa ni lazima ilipwe Shilingi milioni 30.
Kipengele kinasema Yanga italipa kwa awamu mbili, awamu ya kwanza shilingi milioni 15 na mwisho ilikuwa mwezi Aprili na awamu ya pili ni mwezi Juni," alisema.
Alisema, Yanga walifanya hivyo na rasmi mchezaji huyo kuwa mali ya Yanga, na iliruhusiwa kufanya mazungumzo na mchezaji.
"Tarehe 27, Machi mwaka huu ilimtumia tiketi ya ndege kutoka Kigoma hadi Dar es Salaam kwa ajili ya kufanya maongezi na Machi 28 alisaini mkataba wa miaka mitatu mbele ya mwanasheria wake na ulitakiwa kuanza kufanya kazi Julai Mosi mwaka huu," alisema.
Hata hivyo alidai baadaye ilipokea barua kutoka Singida Fountain Gate ikisema malipo yale yabadilishwe yawe ya mchezaji Nickson Kibabage ambaye yupo Yanga kwa mkopo.
" Julai 6 tuliwaingizia Shilingi milioni 30 kwa ajili ya mchezaji Kibabage, pesa ya Kagoma ikabaki pale pale.
Kwa maana hiyo Kagoma ana mkataba na klabu mbili na sababu ya kupeleka Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ilikuwa ni kuvunja mmoja ili mchezaji awe wa timu moja, suala hili halijasikilizwa.
Hivi karibuni klabu ya Fountain Gate ilisema ilishamalizana na Simba, ambapo wanavyojua Kagoma ni mchezaji halali wa klabu hiyo baada ya kutimiza matakwa yote ya mkataba.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED