MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, wamepata ushindi mkubwa zaidi kwa mara ya kwanza, wakiibamiza Fountain Gate mabao 5-0 katika mechi ya upande mmoja muda mwingi wa mchezo iliyochezwa, Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam jana.
Ni mechi ya tano mfululizo kwa Yanga kupata ushindi tangu ilipofungwa kwa mara ya mwisho na Tabora United mabao 3-1, Novemba 7, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Ushindi huo pia umeifanya Yanga kuwa timu inayoongoza kwa kufunga mabao mengi kwenye Ligi Kuu, kwani imefikisha jumla ya mabao 32, ikiiacha Simba ikiwa na mabao 31 ya kufunga, lakini kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa zikiwa zimelingana.
Yanga imeruhusu jumla ya mabao sita wakati Simba ikiruhusu matano nyavuni kwake zote zikicheza mechi 15 kila moja.
Hata hivyo, pamoja na ushindi huo, Yanga inaendelea kuwa nafasi ya pili baada ya kufikisha pointi 39, nyuma ya Simba iliyo kileleni na alama zake 40.
Yalikuwa ni mabao mawili ya Pacome Zouzoua, Mudathir Yahaya, Clement Mzize na moja la kujifunga na Jackson Shiga, yalitosha kuwafanya mashabiki wa Yanga kutoka uwanjani maeneo ya Mwenge kwa furaha.
Mechi ilianza taratibu kama vile timu zote zilikuwa zinasomana na hakukuwa na shambulizo lolote hadi dakika ya 14, Pacome alipokosa bao akiwa ndani ya eneo la hatari kwa shuti lake la mguu wa kushoto kutoka nje akiwa amepata pasi mpenyezo kutoka kwa Mudathir.
Dakika moja baadaye kiungo mshambuliaji huyo raia wa Ivory Coast, alisawazisha makosa yake alipofunga bao la kwanza, akiunganisha krosi kutoka wingi ya kushoto iliyopigwa na Shadrack Boka.
Salum Kihimbwa aliikosesha Fountain Gate bao dakika ya 18, alipowalamba chenga, Kibwana Shomari na Dickson Job, lakini alipiga shuti dhaifu lililodakwa na kipa Aboutwalib Mshery.
Faulo iliyopigwa na Stephane Aziz Ki, dakika ya 27, nusura itinge nyavuni, lakini mpira ukagonga nguzo ya pembeni na kutoka nje, huku ukiwa ameshampita kipa, John Noble.
Mnigeria huyo, alifanya kazi ya ziada dakika ya 31, alipofanikiwa kudaka shuti la ana kwa ana la Pacome, alipolipiga akiunganisha mpira wa kona uliopigwa na Aziz Ki.
Kama angekuwa makini, straika Edgar William, angeweza kuipatia Fountain Gate bao dakika ya 34, baada ya kutengenezewa nafasi nzuri na Kihimbwa, akiwa anamtazama kipa Mshery, alichelewa kupiga, na wakati alipoamua kufanya hivyo, beki Ibrahim Hamad 'Bacca' alikuwa amefika na mpira ukambabua na kuwa kona.
Dakika ya 40, Yanga iliandika bao la pili likiwekwa wavuni na Mudathir, likiwa bao lake la kwanza msimu huu. Bao hilo lilipatikana baada ya kutokea kizaazaa kwenye lango la Fountain Gate, kabla ya Prince Dube hajaurudisha ndani mpira uliokuwa unataka kutoka, mfungaji akaukwamisha wavuni.
Pacome, aliiandikia Yanga bao la tatu, likiwa ni la tano kwake msimu huu akipokea pasi kutoka kwa Aziz Ki, ambaye aliukimbilia mpira ulioachwa kizembe na wachezaji wa Fountain Gate.
Kipindi cha pili kila timu ilifanya mabadiliko ya wachezaji kwa nyakati tofauti, lakini haikuisaidia Fountain Gate ambayo ilikuwa ikicheza nyuma ya mpira hata ilipokuwa imefungwa idadi hiyo ya mabao.
Shiga, alijifunga dakika ya 53 na kuipa Yanga bao la nne, akiusindikiza kwa kifua mpira uliokuwa unarudi uwanjani baada ya shuti la Pacome kugonga mwamba wa juu na kuwa bao la tano, wachezaji wakijifunga wenyewe kwenye Ligi Kuu.
Dakika tatu kabla ya mechi kumalizika, Mzize alipachika bao la tano kwenye mchezo huo, likiwa la sita kwake msimu huu akiwa sasa anaongoza kwa ufungaji mabao kwenye kikosi cha Yanga.
Aliwazidi mbio mabeki wa Fountain Gate na kuubetua mpira mbele ya kipa Noble aliyekuwa ametoka langoni kumkabili, mpira ukaelekea wavuni licha ya jitihada za Laurian Makame kutaka kuuokoa.
Kipigo hicho kinaiacha Fountain Gate ikiwa na pointi 20, ikiwa kwenye nafasi ya sita ya msimamo wa ligi ambayo imeanza kuingia mzunguko wa pili kwa baadhi ya mechi, huku Yanga ikimaliza mzunguko wa kwanza kwa kukusanya pointi 39.
Baada ya kipigo hicho, taarifa kwa umma iliyotolewa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Fountain Gate, ilieleza kuwa umeamua kulivunja benchi lote la ufundi lililokuwa likiongozwa na Kocha Mkuu, Mohamed Muya.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED